Vinavyotokea kwa watu wengi, vichache sana huwa ni bahati mbaya, na vichache sana huwa ni hila tu dhidi yao, vingi vinavyowatokea watu huwa wanavuna yale walipanda wao wenyewe.
Matokeo mengi mazuri wanayopata watu, huwa sio kwa sababu wana bahati sana katika maisha yao, matokeo mengi mazuri yamelipiwa gharama kubwa mno na wahusika mpaka kuja kupata matokeo mazuri.
Vitu vidogo vidogo vizuri unavyofanya katika maisha yako, vina matokeo makubwa mazuri siku za mbele, yale yale mambo madogo madogo unayoyazingatia katika maisha yako ya kila siku. Yanaumba kitu kikubwa sana mbeleni kama hutopuuza hatua zako ndogo ndogo unazopiga.
Ubaya unaouopanda leo, tena ubaya wenyewe unaupanda kidogo kidogo, ipo siku utavuna matunda ya ubaya wako. Ule ubaya mdogo uliouona huna tatizo sana, kesho utazaa kitu kikubwa sana.
Ule wema wako mdogo mdogo unaowafanyia watu wengine, hata kama kwa sasa huoni matokeo makubwa sana. Ipo siku utavuna matunda ya wema wako, tena utavuna wakati ambao ulishasahau kama umewahi kufanya jambo jema la kumsaidia mtu.
Yule anayetafuta kutenda mema ipo siku atapata ukarimu/fadhili kwa mema yake, na yule anayeutafuta ubaya utamjia kwake tu.
Rejea: Yeye atafutaye mema hupata ukarimu, bali ubaya huja kwake yeye autafutaye. Mithali 11:27 NEN.
Haijalishi umetengezwa mpango mbaya kiasi gani kwako juu ya maisha yako, ukisimama vizuri na Mungu wako, uhusiano wako ukawa vizuri na Mungu wako. Uwe na uhakika mabaya yaliyopangwa kwako yatawarudia wale wale waliyoyapanga.
Unaweza kuona haiwezekani, unaweza kuona ndio mwisho wako wa maisha, unaweza kuona kazi yako ndio mwisho, unaweza kuona biashara yako ndio mwisho. Nakwambia haitakuwa mwisho kwako mtenda mema au mtafuta mema kama sio mpango wa Mungu iwe mwisho.
Tengeneza bomu lako vizuri kabisa kwa ajili ya kumwangamiza mtu usiyempenda wewe, acha chuki zako zikuhamasishe kutengeneza kitu kibaya juu ya mtu asiye na hatia yeyote. Uwe na uhakika hilo bomu litakulipukia wewe mwenyewe mtengenezaji, ni kama haiwezekani kutokana na ulivyojipanga ila kwa Mungu itawezekana.
Kama huamini haya, basi yupo mtu ambaye na yeye alijua haiwezekani, tena hakujua mtego alioutengeneza kwa ajili ya mtu mwingine kuangamizwa. Ule ule mtego ndio ungekuja kutumika kumwangamiza yeye mwenyewe, mtu huyo si mwingine bali ni Hamani.
Rejea: Basi wakamtundika Hamani juu ya mti aliomwekea tayari Mordekai. Ghadhabu ya mfalme ikatulia. EST. 7:10 SUV.
Kanuni ipo pale pale, ukitenda mema utavuna matunda ya mema yako, na ukitenda ubaya utavuna matunda ya ubaya wako. Hakuna namna unaweza kukwepa hili, hata kama itachukua muda sana, uwe na uhakika utavuna matunda yake.
Neno la Mungu linatusaidia sana kujiweka vizuri, linatusaidia kuendelea kumfurahia Mungu hata katikati ya taarifa mbaya juu yetu. Maana tunakuwa na uhakika mabaya waliyoyapanga maadui zetu, hayo mabaya yatawarudia wao wenyewe, kazi yetu ni kwenda mbele za Mungu kumweleza.
Kama ulikuwa kwenye kundi la watu wanaotengeneza mipango mibaya kwa ajili ya kuwangamiza wengine, ondoka haraka kwenye familia hiyo kabla hasira ya Bwana haijakushughulikia. Huenda umefanikiwa kuwatendea mabaya watu kadhaa, Mungu amekuvumilia na kukupa muda utubu na ubadilike, ukiwa na shingo ngumu utashughulikiwa kisawasawa.
Ulikuwa unatenda mema ila ukajikuta umekatishwa tamaa na mambo fulani, hakikisha unaendeleza huduma yako. Usiache kutenda mema utavuna matunda ya kazi yako.
Mungu akubariki sana.
Rafiki yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com