Mtu mwaminifu haanzi kupimwa na mambo makubwa, anaanza kupimwa kwa mambo madogo madogo. Ndipo watu humwona na kumwamini sana, anapoaminiwa kwa madogo anapewa nafasi ya kufanya mambo makubwa zaidi.
Ukimwona mtu hayupo makini kwa mambo madogo kwa kisingizio cha hawezi kuwa makini na mambo madogo, anaweza kuwa makini kwa mambo makubwa. Mtu huyo atakuwa anajidanganya, na mtu huyo atakuwa anakudanganya pia.
Anayekuomba shilingi elfu moja na kukuhaidi atakurudishia, alafu baada ya hapo akaidharau kuwa ni kiasi kidogo na akaona haina haja kukurudishia. Uwe na uhakika ukimpa kiasi kikubwa nacho atakipuuza vile vile.
Umepanga kwenye nyumba ya mtu, alafu huwi makini na nyumba hiyo, unaacha watoto wanaichafua hovyo, kitu kikiharibika hushtuki na huoni umhimu wa kukirekebisha. Uwe na uhakika hata ukipewa nyumba yako mwenyewe hutokuwa makini nayo.
Umakini wa mtu huanza na mambo madogo, wakati mwingine hayo mambo huwa sio ya kwetu. Lakini kupitia hayo tunatengeneza picha nzuri au mbaya kwa watu, kuwa ni watu wa namna gani.
Asikudanganye mtu kuwa anafanya hivyo kwa sababu kitu sio chake, huyo mtu hata akiwa na kitu chake atakiharibu. Maana ndani yake hana umakini, wala sio mwaminifu, anaweza kujiharibia kitu alichokitafuta kwa jasho lake mwenyewe.
Mtu aliyeshindwa kulea watoto aliyekabidhiwa na ndugu zake, usifikiri akipata watoto wake ataweza kuwalea vizuri. Anaweza kufikiri kwa kuwa sio wa kwake hawezi kuwa na uzito sana ila awe na uhakika hata akiwa na wa kwake watamshinda.
Mtu akishindwa kutunza pesa zake, usifikiri ukimpa pesa zako ataweza kuzitunza. Uwe na uhakika atazitapanya tu, nidhamu ya mtu kwa vitu vya wengine, huanza kwa vitu vidogo vidogo vinavyoonekana vya kawaida sana.
Uaminifu huanzi kwa vitu vikubwa, wala kuaminiwa na watu hakuanzi na mambo makubwa, huanza na mambo madogo madogo. Ambayo yanaonekana sio muhimu sana, kupitia hayo mambo madhaifu, yanapofanywa vizuri na kwa uaminifu mkubwa. Humweka mtu katika nafasi nzuri ya kuaminiwa na wengine.
Mpaka mtu apewe nafasi ya uhasibu kwenye vikundi mbalimbali, inaweza ikawa kanisani, shuleni, mtaani, chuoni, kambini, ukiacha kuwa ni taaluma. Uaminifu wa mtu humfanya apewe hiyo nafasi ya uhasibu, yaani mtunza fedha.
Neno la Mungu lipo wazi kwa hili, sio kana kwamba watu wametengeneza tu. Hii ni kanuni ya asili tena ipo kibiblia kabisa, huwezi kuivunja wala huwezi kuirekebisha, itabaki kama ilivyo.
Rejea: Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana, huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia; na aliye dhalimu katika lililo dogo, huwa dhalimu katika lililo kubwa pia. LK. 16:10 SUV.
Haleluya, unaona hilo andiko takatifu, ile b yake linasema hivi; na aliye dhalimu katika lililo dogo, huwa dhalimu katika lililo kubwa pia. LK. 16:10(b) SUV
Unaona vile udhalimu wa mtu huanzi na mambo makubwa, udhalimu wa mtu huanza na mambo madogo madogo. Na tunaona uzuri wa mtu huletwi na kufanya mambo makubwa sana, uzuri wa mtu huanza kutengenezwa na mambo madogo madogo.
Hata kwenye huduma, huduma ya utumishi ndani ya mtu huanza kuonekana vizuri kwa mtu anayejibidiisha katika mambo madogo mbele za Mungu. Anakuwa mwaminifu kwenye ibada za kanisani, anazingatia utakatifu, anajibidisha kwenye Neno la Mungu, anajibidisha kwenye maombi.
Huwezi kusema nina maono makubwa sana ya kumtumikia Mungu, wakati huonyeshi chochote kinachothibitisha unachoongea au unachofikiri. Hata usipoongea matendo yako yataonyesha huyu ndugu anaelekea wapi.
Ukitaka watu waanze kukuamini sasa kama walikuwa hawakuamini vizuri, anza kuwa mwaminifu kwa mambo madogo madogo. Tena uwe mwaminifu kweli, haijalishi hayo mambo hakuna anayeyazingatia sana, wewe kuwa mwaminifu bila kujalisha nani anakutazama. Baada ya muda fulani utaona mabadiliko makubwa sana, watu wataanza kukuamini.
Muhimu, unapenda kukua kiroho kwa kusoma Neno la Mungu kila siku? Jibu lipo CHAPEO YA WOKOVU, karibu katika darasa letu la kusoma Neno la Mungu kila siku kwa njia ya whatsApp group. Tutumie ujumbe wako kwenda +255759808081, utaunganishwa.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com