Wengi tunafanya kazi za kuajiriwa ila siku tukifukuzwa katika kazi hizo, hatuna uwezo wa kwenda kufanya kazi zingine ngumu kama vile ya kulima. Hii ni kutokana na kujifungia kwenye kazi moja, ikatufanya tusiwaze kufanya kitu kingine cha kutuingizia kipato zaidi ya hiyo ajira.

Leo mtu akichishwa kazi aliyokuwa anaifanya hawezi kwenda kufanya kazi nyingine ya kuweza kumwingizia kipato, kutokana na kuona aibu. Anajifikiria watu watamwonaje akiwa anauza nyanya, akiwa anatembeza nguo za mitumba, akiwa anauza mkaa, akishafikiria hayo hawezi kufanya chochote.

Maisha yanakuwa magumu zaidi sio kwa sababu ya kuachishwa kazi, sababu haswa ni kuona aibu kufanya kazi zingine tofauti na ile iliyokuwa inampa heshima mbele za watu.

Tunapaswa kufikiri njia nyingine mbadala ya kujiongezea kipato, hata kama tumeajiriwa sehemu nzuri sana, hata kama tunalipwa mshahara mkubwa sana. Tunapaswa kuwa na njia nyingine ya kutuingizia kipato, maana ipo siku hiyo kazi itakuwa na mwisho, muda mzuri wa kuanza kujizoeza kufanya kitu kingine pembeni ni wakati ukiwa kwenye ajira yako.

Ufanye nini sasa unapojikuta kwenye wakati wa kutakiwa kufukuzwa kwenye kazi uliyokuwa unaifanya, unapojikuta kwenye wakati kama huo unapaswa kukaa chini kufanya jambo la kukusaidia ubaki kwenye nafasi yako.

Hili tunajifunza kwa wakili aliyeajiriwa na bwana wake, bwana wake alifika mahali akaona makosa ya wakili wake aliyoyafanya kwenye mali zake. Kulikuwepo na hasara kubwa iliyosababishwa na wakili huyu, alivyoona kibarua chake kinaenda kwisha, alitafuta njia mbadala ya kumsaidia akaribishwe nyumbani mwao, pale atapoondolewa kwenye uwakili wake.

Rejea: Yule wakili akasema moyoni mwake, Nifanyeje? Maana, bwana wangu ananiondolea uwakili. Kulima, siwezi; kuomba, naona haya. Najua nitakalotenda, ili nitakapotolewa katika uwakili, wanikaribishe nyumbani mwao. LK. 16:3‭-‬4 SUV.

Unaona hapo nilichokuwa nakueleza hapo juu, huyu wakili alikiri wazi moyoni mwake kuwa hana uwezo wa kulima, wala hawezi kwenda kuombaomba msaada mtaani. Akaona anapaswa kufanya jambo litakalomfanya akaribishwe nyumbani mwao wale atakawaotendea mema, kama itatokea akaondolewa kwenye nafasi yake, kwa sababu alikuwa anaona kinachofuata ni hicho.

Alichokifanya wakili huyu ni kuwaita mmoja mmoja watu wote aliowakuposha vitu kwa riba kubwa, ili waweze kumrudishia haraka mali za bwana wake, aliwaambia walete kile kiasi alichowakopesha bila kuweka na riba.

Rejea:Kwa hiyo akawaita wadeni wote wa bwana wake, mmoja mmoja. Akamwuliza wa kwanza, Deni lako kwa bwana wangu ni kiasi gani? Akajibu, Galoni 800 za mafuta ya mizeituni. Msimamizi akamwambia, Chukua hati ya deni lako, ibadilishe upesi, uandike galoni 400. Kisha akamwuliza wa pili, Wewe deni lako ni kiasi gani? Akajibu, Vipimo 1,000 vya ngano. Yule msimamizi akamwambia, Chukua hati yako, andika vipimo 800! Luka 16:5‭-‬7 NEN.

Baada ya zoezi lile kuisha, bwana wake alimsifu sana huyu wakili dhalimu alivyotenda kwa busara. Mpaka bwana wake kumsifu wakili huyu na wakati alishamwona ni mtu ambaye hafai, ujue alifanya jambo ambalo lilikuwa la kushangaza, na lisilotarajiwa kabisa kutendeka.

Rejea: Yule bwana akamsifu wakili dhalimu kwa vile alivyotenda kwa busara; kwa kuwa wana wa ulimwengu huu katika kizazi chao wenyewe huwa na busara kuliko wana wa nuru. LK. 16:8 SUV.

Tunaongezewa kitu kingine kikubwa sana, Yesu anatueleza kuwa wana wa ulimwengu huu huwa wana busara kuliko wana wa nuru, yaani wana wa nuru ni wale watu waliokoka. Kumbe wakati mwingine tunaweza kushindwa akili na wale wasiomjua Kristo kabisa, ndio maana unaweza kushangaa wanazidi kustawi kwenye kazi zao.

Usishindwe akili na watu wasiomjua Kristo, hata wewe unaweza kufanya jambo kwa watu ambao watakukumbuka na kuwa msaada kwako wakati huna kitu.

Unaweza kuokoa kazi yako kwa kutumia mbinu ambayo utaipata kwenye ufahamu wako, mbinu hiyo ikakufanya ukaendelea kubaki kwenye cheo chako kama tulivyoona kwa wakili huyu.

Hii ndio faida ya kusoma Neno la Mungu, unajua mengi na unakuwa na uwezo mkubwa wa kufanya maamzi magumu zaidi, na yakaleta matokeo mazuri kwako.

MUHIMU; kuna darasa letu la kusoma Neno la Mungu kila siku kwa njia ya whatsApp group, una kiu ya kukua kiroho kwa kusoma Neno la Mungu, una changamoto ya kushindwa kujijengea nidhamu ya kusoma Biblia. Chapeo Ya Wokovu ni jibu lako, tuma ujumbe wako kwenda namba hii +255759808081, tutakuunganisha kwenye darasa letu.

Mungu akubariki sana.

Ndugu yako katika Kristo,

Samson Ernest.

www.chapeotz.com