Kusamehe ni wajibu wa kila mwamini kufanya hivyo, bila kuangalia mara ngapi mtu amekukosea, wala bila kuangalia ukubwa wa kosa ulilotendewa. Maana pasipo kusamehe unafunga milango yako mbele za Mungu, Mungu hawezi kukusamehe makosa yako kabla hujamsamehe aliyekukosea.

Yapo mambo ambayo utapaswa kuyapuuza na kuachilia moyoni mwako bila hata mhusika kuja kukuomba msamaha, hii ni kwa ajili ya usalama wa roho yako. Maana sio kila aliyekukosea ataweza kukujia na kukuomba msamaha, ndio maana ni muhimu sana kumpuuza na kumwachilia moyoni mwako.

Pamoja na tunapaswa kusamehe, je kila mmoja wetu anafanya hivyo? Jibu linaweza kuwa hapana na kwa wachache inaweza ikawa ndio. Wanaojua madhara ya kutosamehe, huwa hawakai na hasira mioyoni mwao, wale wasiojua madhara ya kutosamehe au wanajua ila wanapuuza, huwa wanakuwa na madhara mengi sana kulinganisha na yule aliyesamehe.

Baada ya kuona hayo sasa tuone upande mwingine, upande mwingine ni kwamba kabla hujamsamehe aliyekukosea unapaswa kufanya hichi kitu kwake. Unapaswa kumwonya huyo aliyekukosea, ndio ni muhimu sana kumwonya yule aliyekukosea.

Ukishamwonya aliyekukosea, alafu huyo mtu akakubali na kukuomba umsamehe, hatua ya pili unapaswa kumsamehe na kumwachilia moyoni mwako bila kuangalia ukubwa wa kosa lake, wala bila kuangalia mara ngapi amekukosea.

Rejea:Jilindeni; kama ndugu yako akikosa, mwonye; akitubu msamehe. Luka 17:3 SUV.

Unaona hapo, jambo la msingi ni kumwonya, ajue alichokufanyia sio sahihi, ajue ulichukia kweli, sasa baada ya kumweleza mambo yote uliyokuwa nayo. Mwachie nafasi na yeye, kuna mambo mawili hapo, anaweza kukuomba msamaha, au anaweza asikuombe msamaha.

Labda unajiuliza sasa itakuwaje umsamehe mtu ambaye yeye mwenyewe hataki kukuomba msamaha, mtu ambaye hataki kutubu makosa yake?

Jibu lipo, tunarudi sasa kwenye kanuni ya Mungu inasemaje au inatulazimisha tufanyaje kwa mtu ambaye hataki kutubu makosa yake. Tutapaswa kusemehe, mambo mengine ya kulipiza kisasi tunamwachia Mungu mwenyewe, lakini sisi sharti tusamehe kwanza ili kulinda uhusiano wetu na Mungu.

Rejea: Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu. [ Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.] Marko 11:25‭-‬26 SUV.

Unaona hapo, inatulazimisha tusamehe, kwa maana nyingine hatuna namna tunaweza kutengeneza mazingira ya kushindwa kuwasamehe waliotukosea ila tunapaswa kufanya jambo hili kwao.

Jambo la kufanya ni kuwaonya wale wanaotukosea, tukishawaonya, alafu wakatuelewa na kutuomba radhi/kutubu, tunapaswa kuwasamehe bila kujihoji mara mbili mbili. Kufanya hivyo tutakuwa tumefanya kama Neno la Mungu linavyotuelekeza.

Usiwe na dukuduku na mtu anayekutendea mabaya, wala usisemee pembeni bila mhusika kujua, mweleze ukweli, mwonye kuhusu tabia yake. Ukishafanya hivyo subiri akuambie na yeye.

Kama utamwona anaendelea kukutendea mabaya, hadi anafika hatua anatishia uhai wako, unaona maisha yako yapo hatarini, unaweza kumpeleka kwenye vyombo vya sheria. Kufanya hivyo hufanyi dhambi, vyombo vya sheria ni mamlaka ambazo zipo kiMungu.

Mwisho, hili ni muhimu sana kwako, tuna darasa letu la kusoma Neno la Mungu kila siku, hili darasa linakujengea nidhamu ya kusoma Biblia yako katika mtiriko mzuri. Unahitaji kukua kiroho kwa kusoma Neno la Mungu? Jibu lipo CHAPEO YA WOKOVU, tuma ujumbe wako kwenda +255759808081, tumia WhatsApp tu kutuma sms yako.

Mungu akubariki sana.

Ndugu yako katika Kristo,

Samson Ernest

www.chapeotz.com