Watu wasiojulikana wapo pia kwenye eneo la kiroho, watu hawa ni wale wanaosambaza mafundisho potofu, mtu akishakutana na mafundisho hayo potofu. Mtu huyo akayakubali hayo mafundisho potofu, huyo mtu anakuwa mateka moja kwa moja.

Mafundisho potofu au elimu potofu haiangalii upo mahali sahihi pa kusali, unaweza ukawa mahali sahihi pa kusali ila ukajikuta unakuwa mateka. Watu wanaweza kukuona kama upo pamoja nao, ila moyoni mwako unakuwa unajua kabisa hampo pamoja nao.

Elimu potofu au mafundisho potofu yanaendana na mafundisho/elimu sahihi, mtu anaweza kupata mafundisho sahihi akatoka kule ambapo palikuwa sio mahali sahihi. Na mtu anaweza kupata mafundisho yasiyo sahihi, akaondolewa mahali ambapo palikuwa sahihi kwake, na akahamia mahali ambapo sio sahihi.

Mafundisho potofu na mafundisho sahihi, ni watu wawili tofauti ambao kila mmoja anatafuta wafuasi wake, na kila mmoja ukikutana naye atakwambia yupo sahihi na yule mwingine ni muongo.

Ukikutana na mwenye mafundisho/elimu sahihi anaweza kukupa kile sahihi na wewe ukabaki kusema kama vile hii ndio sahihi? Na ukikutana na mwenye mafundisho/elimu potofu naye ataonekana kwako aongea ukweli, mafundisho ya mwanzo ambayo ni sahihi, unaanza kuyaona hayafai.

Usipopata wa kukung’amua kwenye utata huo, utabaki unatanga tanga, na mwisho wa siku utajikuta umeangukia sehemu ambayo inaamini mafundisho potofu. Maana mafundisho potofu yana utamu fulani ambao hukufungi sana kwenye tamaa za mwili, yapo huru kukufanya ufanye lolote isipokuwa usizidi sana kiasi.

Unaweza kujiuliza sasa nitawezaje kujua hapa nipo mahali sahihi, na hapa sipo mahali sahihi; na nitawezaje kujua hii ni elimu sahihi, na hii ni elimu potofu? Usiogope utaelewa tu, endelea kuwa pamoja nami katika somo hili.

Umakini unahitajika sana kwako, maana usipokuwa makini utapotelea pasipojulikana na watu wataendelea kujiuliza ni kitu gani kimekupoteza. Kumbe kilichokuteka na kukufanya upotee ni mafundisho potofu.

Kumbuka kila mmoja anavutia upande wake, elimu potofu hataki kukuona ukiwa upo mahali sahihi, na elimu sahihi hataki kukuona ukiwa mahali sio sahihi. Hawa watu wawili wanafanya kazi kubwa pamoja, ukizumbaa kidogo tu unachotwa ufahamu wako na mmoja wapo.

Neno la Mungu linasemaje kuhusu hili, kabla sijafika kwenye hitimisho la somo hili, hebu tusome andiko hili takatifu;

Rejea: Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya Kristo. KOL. 2:8 SUV.

Utawezaje sasa kuepuka kuchotwa na mafundisho potofu? Ni kwa kuwa na Neno la Mungu la kutosha moyoni mwako. Neno la Mungu litakusaidia kujua hii ni elimu sahihi, na hii ni elimu potofu, na haya ni mapokeo ya wanadamu yenye udanganyifu mwingi ndani yake.

Shida kubwa ya elimu potofu au mafundisho potofu yakitangulia kuingizwa kwa mtu kabla ya elimu sahihi, uwe na uhakika mtu huyu atahitaji neema ya Mungu iingilie kati. Maana huwezi kumwondoa kienyeji, wala huwezi kumwondoa haraka kama unavyotaka wewe.

Mtu yeyote anayepanda mafundisho potofu kwa watu, anawekeza nguvu kubwa haswa, kiasi kwamba kuja kung’oa hiyo mizizi unahitaji uwe umejipanga kisawasawa. Maana kila eneo ambalo unafikiri unaweza kuligusa mtu akajua ukweli, eneo hilo linakuwa limewekewa hoja zake za msingi, ukijaribu kuligusa tu utakutana na majibu ya kutosha.

Kinachoweza kutusaidia katika hili ni Neno la Mungu, na fundisho lolote linapaswa kupimwa kwa Neno la Mungu. Haijalishi hilo fundisho ni zuri kiasi gani, lazima tulitazama kimaandiko ‘lipo sawa? Kama halipo sawa hatupaswi kulifurahia.

MUHIMU; kama unapenda kukua kiroho kwa kusoma Neno la Mungu, lipo darasa letu la kusoma Neno la Mungu kila siku kwa njia ya whatsApp group. Kama unahitaji kuunganishwa katika group hili la whatsApp, tuma ujumbe wako kwenda namba +255759808081.

Mungu akubariki sana.

Ndugu yako katika Kristo,

Samson Ernest

www.chapeotz.com