Vita kwa mambo ya Mungu haijaanza leo, hii vita imeanza siku nyingi sana, unapoona unakutana na upinzani mkubwa sana kwa mambo ya Mungu. Ujue ni kitu ambacho kilikuwepo na kitaendelea kuwepo mpaka pale Yesu Kristo atakaporudi kuchukua kanisa lake.

Unapokutana na upinzani kwa mambo ya Mungu, unapaswa kujua anayepingwa sio wewe bali yule uliyembeba ndani yako, ambaye ndiye mwenye mamlaka yote hapa Duniani na mbinguni.

Kumekuwa na malalamiko kuwa wakristo wana makelele sana, haya makelele yanayosemwa sio makelele ya kugombana, sio makelele ya watu waliochanganyikiwa au waliorukwa akili, haya makelele sio ya watu waliolewa pombe. Bora yangekuwa hayo tungesema ni makelele yasiyofaa, maana wanaopiga hizo kelele wanahitaji msaada wa kusaidiwa kutokana na hali zao.

Kelele za watoto wa Mungu, ni za kumsifu Mungu wao, kumtukuza kwa nyimbo zao, kumshukuru kwa maombi ya nguvu, haya ni matokeo ya furaha kwa mkristo kwa yale Mungu amewatendea mambo makubwa katika maisha yao.

Kusikika kelele za maombi makubwa ni kiashiria kizuri cha watu wanapeleka mahitaji yao sehemu husika, wanapeleka kwa Baba yao anayeweza kuwasaidia shida zao. Watu hawa wangeonekana wa ajabu kama wangekuwa wanapiga kelele za kuomba sanamu inawasaidie shida zao.

Kwahiyo ukiwa kama mkristo ambaye umetoa maisha yako kwa ajili ya Bwana, unapokutana na vipingamizi kama hivi vya kuambiwa unatupigia kelele. Ujue unatimiza tu andiko, hili zuio alikutana nalo Yesu Kristo katika huduma yake.

Mwanadamu bado ni yule yule hajabadilika, na shetani bado ni yule yule hajabadilika, bado anaendelea kupanda chuki kwa watawala mbalimbali, watu mbalimbali. Ili kuhakikisha jina la Yesu Kristo halitukuzwi kwa sauti kubwa.

Rejea: Hata alipokuwa amekaribia matelemko ya mlima wa Mizeituni, kundi zima la wanafunzi wake walianza kufurahi na kumsifu Mungu kwa sauti kuu, kwa ajili ya matendo yote ya uwezo waliyoyaona, wakasema, Ndiye mbarikiwa Mfalme ajaye kwa jina la Bwana; amani mbinguni, na utukufu huko juu. Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa katika mkutano wakamwambia, Mwalimu, uwakanye wanafunzi wako. Akajibu, akasema, Nawaambia ninyi, wakinyamaza hawa, mawe yatapiga kelele. LK. 19:37‭-‬40 SUV.

Kama umeokoka na bado unajisikia vibaya unapoona watu wanaomba kwa sauti, bado unajisikia vibaya unapoona watu wanaimba kwa sauti, ujue ndani yako kuna roho ya Mafarisayo inakutesa. Unapaswa kujichunguza upya na kujiuliza ni wokovu wa namna gani unao ndani yako, wakati unachukia unapoona jina la Yesu Kristo linasifiwa kwa nguvu kubwa.

Ukiona una hali hiyo ya kuzuia watu wasimsifu Mungu wao na umeokoka, ujue una mapokeo ya dini yako, una mafundisho ya mapokeo ya wanadamu. Laiti kama ungekuwa na mafundisho sahihi ya Neno la Mungu, usingeweka ustarabu wa watu wa Dunia hii unapofika eneo la kumsifu Mungu wako.

Mpaka uanze kumsifu Mungu wako kwa sauti kubwa, utakuwa eneo ambalo unaona ni sahihi, huwezi kusifu Mungu mahali popote. Mungu amekupa akili na ufahamu wa kuweza kujua mahali ulipo sio mahali sahihi kupiga kelele za namna yeyote, na mahali ulipo unapaona panastahili kumpazia Mungu wako sauti.

Tena tunaona Yesu Kristo anawajibu Mafarisayo katika ule mstari wa 40, anasema hivi; Akajibu, akasema, Nawaambia ninyi, wakinyamaza hawa, mawe yatapiga kelele. LK. 19:40 SUV.

Hata wakikunyamazisha, mawe yapiga kelele, sijui kama unanielewa vizuri hapa, maana yake ni kitu ambacho hawawezi kukinyamazisha kwa namna yeyote ile. Huwezi kuzuia Yesu Kristo kusifiwa, kujaribu kufanya hivyo atasifiwa hata na ndege wa angani.

Ni bora kuacha watu wamsifu Mungu wao, maana kuzuia watu kumsifu Mungu, Mungu anahitaji kusifiwa, kwa hiyo atainua vitu vingine kabisa vimsifu yeye tu. Utasema hilo linawezekana vipi, kwani uhai ulionao unalipia wapi Bili? Vyote ni vya kwake, aliumba kwa mikono yake mwenyewe, anaweza kuviamrisha vikafanye vile atakavyo yeye.

Acha kuhangaika kuzuia watu wasimsifu Mungu wao, Mungu atasifiwa tu kwa namna nyingi, ukizuia watu kumsifu Mungu wao kwa sababu unasema wanakupigia kelele. Wapo paka watakupigia kelele kwenye bati lako, wapo popo, wapo bundi, na wengine wengi.

Ukipata nafasi ya kumsifu Mungu wako, fanya kweli haswa, acha kumsifu Mungu kama vile umekatika mdomo na wakati Mungu amekujalia una mdomo mzuri, huenda na mikono unayo pia. Kwanini usimsifu Mungu wako? Msifu Mungu ndugu ungali una nafasi ya kufanya hivyo.

MUHIMU; Tuna darasa letu la kusoma Neno la Mungu kila siku kwa njia ya whatsApp group, una kiu ya kukua kiroho kwa kusoma Neno la Mungu kila siku na unakwama kila wakati? CHAPEO YA WOKOVU ni jibu lako, ukikubali kuongozwa na kusimamiwa, lazima ujengewe utaratibu mzuri wa kusoma Biblia yako bila kukwama njiani. Tuma ujumbe wako kwenda namba +255759808081, utaunganishwa kwenye group la whatsApp.

Mwisho, usiache kuweka email yako hapo chini kwa ajili ya kupokea masomo mbalimbali ya Neno la Mungu kila yanapowekwa hewani. Utapokea ujumbe moja kwa moja kwenye email yako unaokujulisha kuwa kuna somo jipya limewekwa.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest
www.chapeotz.com