Tunajifunza mambo mengi, tunasikiliza mafundisho mengi, yenye kujenga tabia njema na yenye kujenga tabia mbaya, yapo mafundisho mengine yanakuja kwetu kwa kusudi la kutuondoa kwenye kusudi la Mungu, na mengine kutupeleka kwenye mpango wa shetani.

Mafundisho/elimu hizi zinaweza zikawa zinalenga sana mambo ya kiroho, na yanaweza kuwa yanalenga sana mambo ya mwili, tunapokuwa tunapata mafundisho ya aina yeyote ile tunapaswa kuwa na tahadhari ndani yetu.

Mtu yeyote mwenye busara ndani yake, huwa ana tahadhari ndani yake kwa fundisho la aina yeyote ile. Haijalishi aliyetoa mafundisho hayo ni mtu wa namna gani, kama hajamfahamu vizuri ila huyo mtu anayempa mafundisho/elimu hiyo ni mgeni. Lakini anakuwa amejitambulisha kwa jina fulani kubwa ili kujenga umakini wa wasikilizaji wake, mwenye busara huwa ngumu kumteka.

Kama hutokuwa makini unaweza kupata mafundisho ya kuua biashara yako, kwa kuwa hukuwa na tahadhari ndani yako, unayabeba mafundisho hayo yasiyo sahihi unaenda kuyatumia kwenye biashara yako. Unashangaa baada ya kufanya mabadiliko kupitia maarifa uliyopata, ukaingia kwenye hasara kubwa.

Mtu anayekupa elimu hiyo au mafundisho hayo yasiyo sahihi, usifikiri hajui anachokifanya, wala usifikiri hajui anachokilenga, anajua kabisa haya mafundisho mtu akiyazingatia vizuri anaenda kuua biashara yake moja kwa moja.

Usishangae mtu alikuwa na huduma nzuri sana Mungu ameiweka ndani yake, mnashangaa anabadilika na kuwa mtu asiyeeleweka, alikuwa anafundisha vizuri mnaanza kuona ufundishaji wake umebadilika. Alikuwa anahubiri injili iliyonyooka vizuri, ghafla anaanza kupindishapindisha maneno, wakati mwingine anaunga mkono mafundisho potofu.

Kilichomkuta huyu ndugu ni kuamini kila mafundisho na kuyaweka moyoni, hakuwa na tahadhari ndani yake, akakutana na fundisho potofu akaliweka moyoni mwake na kuanza kuliishi.

Unaweza kupambana kumweka sawa huyu mtu, mwisho wa siku utajikuta mnapishana naye, kwa sababu mafundisho aliyoyashika moyoni mwake, hayakuwa mafundisho sahihi.

Hupaswi kuamini kila neno, wala hupaswi kuamini kila unachoambiwa, mtu akikuletea habari ambazo huna uhakika nazo au huna ufahamu nazo wa kutosha kuhusu hizo habari. Hakikisha unakaa chini unajua usahihi wa hizo habari ulizozisikia, nje na hapo utakuwa umepata kitu ambacho kinaenda kuangamiza kile ulichonakuwa nacho.

Anayeamini kila neno analoambiwa, huyo mtu hana busara, maana mwenye busara huangalia sana anachoambiwa ni kweli au nadanganywa. Lazima upime maneno unayoambiwa yana ukweli au ni ya uongo.

Rejea: Mjinga huamini kila neno; Bali mwenye busara huangalia sana aendavyo. MIT. 14:15 SUV.

Itakuwa sio busara kuamini kila maneno unayoletwa na watu, yapo maneno mengine yanaletwa kwako kwa ajili ya kuwagombanisha na mtu fulani. Usipokuwa mwangalifu unaweza kuyabeba hayo maneno kama yalivyo, bila kuyachuja vizuri.

Atakuja mtu anakwambia kuna kitu mkikifanya mtaingiza pesa nyingi sana, unakimbilia kufanya hicho kitu. Ukija kushtuka halikuwa jambo sahihi la kufanya, tayari umepoteza mambo yako mengi.

Kama ni jambo la kiroho, hakikisha unalipima kwa Neno la Mungu, hakikisha kinachosemwa kipo kimaandiko kabisa. Kama kitakuwa nje na hapo, unapaswa kuongeza umakini zaidi ya hapo.

Ujinga mwingi unaondolewa kwa kujifunza, unapokuwa na maarifa sahihi ndani yako unakuwa na faida kubwa sana ya kuweza kuchunja maneno mabaya na mazuri.

Ukiisoma Biblia ya habari njema, imelilainisha vizuri hili andiko takatifu kwa kiswahili cha sasa.

Rejea; Mjinga huamini kila kitu anachoambiwa, lakini mwenye busara huwa na tahadhari. Methali 14:15 BHN.

Haleluya, unaona hapo, kumbe mwenye busara huwa na tahadhari sana, lakini kingine tunakiona kwa mtu mjinga, yeye huamini kila neno. Liwe sahihi au liwe la uongo, yeye huamini kama lilivyo, au kama alivyoambiwa.

MUHIMU; Kama unahitaji kukua kiroho kwa kusoma Neno la Mungu kila siku, Chapeo Ya Wokovu ni jibu lako, karibu sana kwenye darasa letu linaloendeshwa kwa njia ya whatsApp. Tuma ujumbe wako kwenda namba +255759808081, tumia WhatsApp tu kutuma sms yako.

Mwisho, hapo chini usisahau kuweka email yako, ili uwe unapata masomo mazuri yanayowekwa kila siku kwenye tovuti yetu.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com