Kila mmoja wetu ana malengo yake katika maisha yake, yupo mtu ana mipango ambayo anapambana kuhakikisha anaifanikisha katika maisha yake. Na tunajua sio kazi rahisi kufikia malengo uliyojipangia, inahitaji uwe na bidii haswa ikiambatana na nidhamu.
Wapo watu wana malengo ya kufanya huduma zao kutoka ngazi ya mkoa/taifa hadi kufikia ngazi ya kuhudumia watu kimataifa. Mpaka mtu kutoka hizo ngazi za chini hadi kuwa ngazi juu, mtu huyu anahitaji kuwa na bidii haswa.
Wapo wanafunzi wanasoma shule, wanatamani kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine ya juu zaidi, huyu mwanafunzi asipozishinda changamoto anazokutana nazo kwenye maisha yake ya shule. Itakuwa ngumu kwake kufikia malengo yake ya kusoma zaidi na kufikia ngazi anayoitaka.
Wapo watu wanaweka malengo kila mwaka kuhakikisha wanaacha tabia fulani mbaya, wanakuwa na bidii siku ya mwanzo kuishi tabia mpya ambayo wanaitaka iwe katika maisha yao. Wengi huwa hawafiki mbali wanakuwa wamerudia tabia zao mbaya za awali, hii ni kwa sababu walikata tamaa pale walipokutana na changamoto ngumu wakati wanajenga tabia mpya.
Wapo watu wanaweka malengo ya kusoma Biblia, kila mwaka unapoanza huwa na shauku kubwa sana ya kuanza kusoma Neno la Mungu kila siku hatua kwa hatua. Wanashangaa baada ya miezi mitatu tangu mwaka uanze, wanakuwa wamerudi nyuma wote, na wachache sana wanakuwa wamefanikiwa.
Hata unapoamua kuishi maisha ya wokovu, maisha ya kumpendeza Mungu wako, lazima uamue kutokubali kurudishwa nyuma na jambo lolote. Ndipo utaweza kufika mahali unapopatamani kufikia ukiwa kwenye maisha ya kumpendeza Mungu wako.
Kinachokuja kuturudisha nyuma ni kuruhusu vitu fulani viturudishe nyuma, unaporuhusu jambo lolote likuvute nyuma, umeruhusu anguko lako kutokea. Hata kama kwa wakati huo hutoliona, kadri unavyozidi kwenda mbele utaona huna hamu ya kufanya kile ulichokuwa unafanya.
Unachotakiwa kujua katika safari ya maisha yako, hutakiwi kuruhusu mtu yeyote akupunguzie mwendo, anaweza kutumia kinywa chake kukukatisha tamaa, usiruhusu hayo maneno yakuondoe kwenye mpango wako au malengo yako.
Hichi tunajifunza kupitia andiko hili takatifu, mwanamke mshunami alimwambia mtumishi wake asimpunguzie mwendo asipomwambia. Mwanamke huyu alijua safari aliyonayo ni ndefu na inahitaji mwendo wa haraka, bila huo mwendo alijua safari ingekuwa ngumu na ndefu zaidi.
Rejea: Akatandika punda, akamwambia mtumishi wake, Mwendeshe, twendelee mbele. Usinipunguzie mwendo, nisipokuambia. 2 FAL. 4:24 SUV.
Hebu jihoji mwenyewe, ni mambo mangapi uliyaruhusu kwenye safari ya maisha yako na leo unaona kabisa yalichangia kwa kiasi kikubwa kukurudisha nyuma. Katika kutafakari huko utaona ni mambo mengi au jambo moja uliliruhusu likuvute nyuma na leo umebakia hapo hapo.
Huyu mwanamke mshunami alimwambia mtumishi wake asimpunguzie mwendo, safari yake ilikuwa kumfikia mtumishi wa Mungu Elisha. Maana yule mtoto aliyempata baada ya kutabiriwa na Elisha, mtoto huyo alikufa, kabla ya kumzika alienda kutoa taarifa kwa Elisha.
Safari ya mwanamke huyu mshunami ilikuwa aonane na Mtumishi wa Mungu Elisha, tahadhari aliyompa mtumishi wake ni asimpunguzie mwendo bila kumwambia. Sijui kama unanielewa hapa, alisema asimpunguzie mwendo asipomwambia.
Wewe umeruhusu watu wangapi ambao hukuwaambia wakupe ushauri, ambao wamekuambia kuokoka ni ngumu, ambao wamekuambia hakuna mwanamke/mwanaume mwaminifu, ambao wamekuambia bora usioe/usiolewe, na ambao wamekupa mifano ya watu wengi walioshindwa kwenye eneo ambalo unakiu ya kufanikiwa kwa viwango vya juu.
Mwanamke huyu alikuwa anajua hili la kupunguziwa mwendo lipo, ndio maana alimpa tahadhari mapema mtumishi wake. Na mwisho tunaona mtoto wake alirejeshewa uhai wake tena na maisha yakaendelea.
Hata wewe unapaswa kulijua hili, usikubali changamoto yeyote ikupunguzie mwendo kwenye usomaji wako wa Neno la Mungu, usikubali changamoto yeyote ikupunguzie mwendo wa ibada, na usikubali changamoto yeyote ikupunguzie mwendo wa ndoto yako au maono yako.
MUHIMU; tumekuandalia darasa zuri sana la kujifunza Neno la Mungu kila siku kwa mtiririko mzuri wa kusoma sura moja ya kitabu na kupata muda wa kutafakari yale uliyosoma. Darasa hili lina nidhamu ya kutosha, kama unataka kuwa miongoni mwa wanafunzi hawa, na simu yako ina uwezo wa wasap, tuma ujumbe wako wasap kwenda +255759808081.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com/somabiblia