Mtu anayeandamwa sana na shetani, hawezi kuwa yule mlevi sana, hawezi kuwa yule mzinzi, hawezi kuwa yule muongo sana, hawezi kuwa yule mchonganishi sana, hawezi kuwa mwizi sana, hawezi kuwa yule muabudu miungu/sanamu.

Watu wa namna hiyo shetani hana muda nao kabisa, usishangae sana kuwaona wapo wapo tu, hawana misukosuko mingi katika maisha yao ya kila siku. Kinachowafanya wasiguswe na shetani, kwa sababu tayari ni watu wake, na wanamtumikia kwa matendo yao maovu, kwa hiyo shetani hana haja ya kuwaletea misukosuko wakati tayari amewabebesha mizigo ya kutosha.

Lakini ndani ya mioyo yao, wana huzuni nyingi, usiwaone kwa nje wapo vizuri ila ndani yao wanajua kabisa wamefungwa kwenye gereza baya. Gereza ambalo linawafanya watumikishwe kufanya vitendo vibaya, wengine wakitaka kutoka huko kwa akili zao huwa inashindikana.

Kwa yule mtu aliyekataa kuwa mtumwa wa shetani, huyo mtu ndio anakuwa adui wa shetani, mambo mengi mabaya yatakuwa yanamjia mara kwa mara ili kumfanya aache maisha yake ya wokovu na kuhamia maisha ya yasiyompendeza Mungu.

Mitengo ya shetani ipo mingi sana kwa watu waliokoka, watu hawa wanatafutwa wanase kwenye mitengo hii, ndio maana watu wa Mungu waliokoka sawasawa wanaandamwa sana na majaribu mengi.

Unaweza kufikiri kama ukristo wenyewe ndio huu si bora niachane nao kabisa, kufikiri hivyo inawezekana ila fahamu ufalme wa Mungu utatekwa na wenye nguvu.

Wale watakao vumilia mpaka mwisho, hao ndio watakaoshinda, hao ndio watakao okoa maisha yao, hao ndio wataziponya nafsi zao, haiji hivi hivi hadi mtu ajitoe haswa.

Rejea: Nanyi kwa subira yenu mtaziponya nafsi zenu. LK. 21:19 SUV.

Subira yako au uvumilivu wako kwa mambo mbalimbali unayokutana nayo, mambo yenye nia ya kukuangusha, wewe ukavumilia na kuendelea kuishi maisha ya kumpendeza Mungu wako. Uwe na uhakika nafsi yako itakuwa salama.

Kukosa subira au kukosa uvumilivu katika maisha yako, vitu vingi sana utashindwa kufanikiwa navyo, hata mambo tu ya kimwili, yanahitaji uvumilivu ndipo uweze kufanikiwa. Kama mambo ya kimwili yenyewe yanahitaji mtu mwenye uvumilivu, si zaidi kwa mambo ya kiroho?

Tuhitaji kuwa na moyo wa subira ndani yetu, kuna kitu unaona kinakawia kuja kwako, au kufika kwako, unahitaji kuwa na subira huku ukiendelea kumtumaini Mungu wako.

Ukikosa subira ndani yako, ukaanza kulazimisha mambo yaende kama unavyotaka mwenyewe, anguko lako litakuwa kubwa mno. Huko ndio tunasema kuangamiza nafsi yako, yaani kuharibu uhusiano wako na Mungu, au kwa maana nyingine ni kuua uhusiano wako mzuri na Mungu.

Subira ni muhimu sana kwa jambo lolote lile, unataka kuwa na mafanikio makubwa katika maisha yako, unahitaji kuwa na subira. Unahitaji mke/mume mzuri unahitaji kuwa na subira huku ukimgojea Bwana.

Unahitaji kuwa mwalimu mzuri, unahitaji kuwa mchungaji mzuri, unahitaji kuwa nabii mzuri, unahitaji kuwa mtume mzuri, na unahitaji kuwa mwinjilisti mzuri, unapaswa kuwa na subira wakati Mungu anakuandaa hatua kwa hatua.

Haijalishi unaona una wito ndani yako, unahitaji maandalizi, unahitaji kulelewa kwanza, unahitaji kufundishwa, unahitaji kujifunza, ili uweze kuitumikia nafasi yako vizuri aliyokuitia Mungu. Ukienda haraka, utashangaa mambo mengi yanavurugika, kumbe hukumsikiliza Roho Mtakatifu wakati anakupa maonyo.

Lakini ikiwa ndani yako kumejaa Neno la Mungu, na hilo Neno la Mungu umeliweka katika matendo, yaani unaliishi kila siku, huwezi kukosa subira/uvumilivu. Maana tayari unao mwongozo unaokusaidia kukuelekeza uenendeje.

MUHIMU; Kabla sijamaliza, nikushirikishe hili, tunalo darasa letu la kusoma Neno la Mungu kila siku kwa mtiririko mzuri. Hili darasa limekuwa baraka kwa watu wengi sana ndani ya Tanzania, na nje ya Tanzania. Na wewe kama una changamoto ya kusoma Biblia yako kwa mtiririko mzuri au unasoma Biblia yako katika mtiririko mzuri ila unataka uungane na wenzako. Na simu yako ina uwezo wa wasap, wasiliane nasi kwa wasap +255759808081, utaunganishwa.

Mungu akubariki sana.

Ndugu yako katika Kristo,

Samson Ernest.

www.chapeotz.com/somabiblia