Kuna watu ambao hatukutegemea kabisa kama wangetufanyia mambo mabaya kutokana na ukaribu tuliokuwa nao, badala yake wamegeuka adui zetu wakubwa kiasi kwamba hawakuwa ndugu zetu wa karibu. Hii imetufanya tuumie sana, na wengine wamefikia hatua wametengeneza msemo huu, bora kumfadhili mbuzi utamla nyama kuliko mwanadamu.
Wapo watu wengine tulikuwa nao karibu sana kama ndugu zetu wa kiroho, tukawabeba mahali fulani wakati wanapita kwenye changamoto ngumu. Tukavaa viatu vyao na kuhakikisha wanavuka kwenye shida zao, lakini walipofanikiwa kutoka kwenye shida waliyokuwa nayo, wamegeuka adui zetu badala ya kuwa baraka kwetu.
Je, kweli tuache kuwasaidia watu shida zao? Je, tuache kuwanyanyua wengine waliopo chini na wakati tupo nafasi ambazo tunaweza kumsaidia na mwingine akawa juu zaidi? Haya maswali yote yana majibu yake hapa, utajua leo nini huwa shida haswa.
Huenda umejiuliza maswali mengi sana kuhusu hili, kutokana na wale uliowafahamu ni watu wazuri, mlipofika mahali walikugeuka na kuanza kutumika kukuumiza moyo wako. Wakati ulitegemea wawe faraja kwako, wao waligeuka kuwa mwiba kwako.
Watu uliowategemea watakuwa upande wako, maana kuna mambo mengi umekuwa pamoja nao, katika huzuni zao uligeuka kuwa faraja kwao, katika ugonjwa wao ulichukua jukumu la kuhakikisha wanapata matibabu sahihi, katika huduma zao ulihakikisha unaelekeza mahali pa kupitia ili waweze kufikia malengo/maono yao.
Kweli hawa watu walifanikiwa kwa kujitoa kwako, vile Mungu alikupa moyo wa kuwasaidia wengine, vile Mungu alikupa moyo wa kusapoti wenye huduma wafikie viwango alivyotaka Mungu, hao hao uliowasapoti wakafanikiwa. Siku unahitaji msaada wao waligeuka na kuwa mwiba kwako.
Ni kama vile Dunia haina usawa kabisa, kama mtu ulimsaidia kwenye shida yake, leo hii anakuwa sehemu ya kuhakikisha anakuangamiza kabisa. Wakati anajua kile kilichomfikisha hapo alipo ni ile sapoti uliyompa, hata kama Mungu alipaga iwe hivyo, ulitii sauti yake ukampa msaada aliouhitaji, kwanini sasa arudishe mabaya kwako badala ya mazuri?
Kabla ya ndugu zetu hawa, au marafiki zetu hawa, hawajatusaliti, huwa kuna kitu kinafanyika kwanza, kinachofanyika ni kwamba shetani huwa anawaingia kwanza. Shetani anapowaingia, ndio huanza kazi ya kutusumbua na kuwa sehemu ya makwazo kwetu.
Hili tunajifunza kwa Yesu Kristo mwenyewe, Yuda Iskariote, alikuwa ni mwanafunzi wake, ndiye aliyekuja kumsaliti kwa kupewa pesa. Lakini kilichoanza kwa Yuda Iskariote ni shetani alimwingia kwanza, ndipo mambo mengine yakafuata.
Rejea: Shetani akamwingia Yuda, aitwaye Iskariote, naye ni mmoja wa wale Thenashara. Akaondoka, akaenda akasema na wakuu wa makuhani na majemadari, jinsi atakavyoweza kumtia mikononi mwao. Wakafurahi, wakapatana naye kumpa fedha. Akakubali, akatafuta nafasi ya kumsaliti kwao pasipokuwapo mkutano. LK. 22:3-6 SUV.
Ndugu yangu, unaweza kushangaa sana na kuanza kujiuliza maswali kama haya, huyu kweli wa kunifanyia haya, huyu kweli anakuwa sehemu ya mimi kuteseka, huyu kweli amesahau wema wangu kwake, huyu kweli anaona mimi ni mtu mbaya kwake, huyu kweli wa kusahau nilitumia mali zangu kuhakikisha anafika hapo alipo?
Ukishajiuliza maswali kama haya unaweza ukajikuta unalia sana na kuona Dunia hii haina huruma hata kidogo, unaweza kuona hii Dunia haina usawa kabisa. Pamoja na kuona hayo yote, upaswa kujua shida haswa ipo wapi, shida ni kwamba shetani amewaingia ndani yako.
Mtu yeyote anayekugeuka na kuwa mwiba kwako, jua kwamba mtu huyo shetani ameshajenga nyumba yake kwake, haijalishi unamwonaje kwa nje, haijalishi unamwona mtu wa ibada sana. Jua shetani ameshaweka makazi yake kwake, chanzo cha matatizo yote hayo ni shetani, siku ameingia kwake ndipo ilipoanza shida.
Kujua maandiko matakatifu yanasemaje inatusaidia sana kuepuka kushindana na mambo mengine kimwili, tunakuwa tunajua moja kwa moja, jeuri ya huyu mtu inatoka wapi, na imesababishwa na nani. Ukishajua hilo huwezi kupata mfadhaiko mkubwa sana, kama ni kupambana unakuwa unajua unapambanaje.
MUHIMU; kama tulivyoona kuna umhimu wa kuwa na Neno la Mungu moyoni mwako, tumekuandalia darasa zuri sana la kujifunza Neno la Mungu kila siku. Darasa hili litakufanya uwe na nidhamu ya kusoma Biblia yako kwa mtiririko mzuri bila kuachilia njiani, hasa ukiwa na nia ya kweli. Ili uweze kuunganishwa kwenye darasa hili, tuma ujumbe wako wasap, kwa namba +255759808081 utaunganishwa.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest
www.chapeotz.com/somabiblia