Kusumbuliwa kwako na watu, kukupa kesi ambazo sio za kweli, kukupeleka kwa mabaraza ya wazee, au kukupeleka mahakamani bila kosa lolote. Kwako inaweza kuonekana kama unaonewa, na kweli unaonewa kwa sababu hukufanya kosa lolote, lakini katika hayo mashtaka ipo faida kubwa.
Katikati ya maonevu hayo yapo mambo mazuri sana yatazaliwa humo, unaweza kujiuliza mambo gani mazuri yanaweza kuzaliwa kwenye maonevu. Mtu anasingiziwa kosa lisilo lake, inakuwaje jambo zuri lizaliwe?
Utakuwa unawaza hivyo, kwa kuwa tunajifunza, hebu twende pamoja utaelewa vizuri ni jambo gani hilo zuri linaweza kuzaliwa kwenye kushtakiwa pasipo kosa lolote.
Kuna watu ni maadui, wao kwa wao hawapatani, wamejaribu kusuluhishana imeshindikana kabisa, inawezekana hali hiyo imeenda kwa muda mrefu wakiwa kwenye ugomvi huo. Inatokea siku wanapatanishwa na mtu mmoja kwa namna ambayo hawakuwa wameipanga.
Siku wanamshtaki mtu ambaye alikuwa ni tishio kwao, mtu ambaye alikuwa kwenye masikio ya watu wengi, mtu aliyekuwa anatenda mambo makubwa sana ya kiMungu. Siku wamemshika na kuwafanya wawe pamoja wakati wanaendelea na kesi, ndio siku ambayo itavunja ugomvi wa miaka mingi.
Wakati watu wanalia kwa ajili yako unavyoonewa pasipo sababu yeyote, katika huo uonevu kuna watu wanapatanishwa, wapo watu walikuwa hawaongei miaka mingi, wapo watu walikuwa hawasalimiani miaka mingi. Lakini siku hiyo watasalimiana, wataombana msamaha na watasameheana bila tatizo lolote.
Chanzo haswa cha kuwafanya wapatane haraka ni kuunganishwa na adui yenu, mtu ambaye alikuwa anaharibu mipango yenu mibaya, mkipanga hichi na kile anaharibu kabisa mipango yenu.
Hili tunajifunza kwa Yesu Kristo, tunajifunzaje? Herode na Pilato walikuwa hawaelewani kabisa, yaani walikuwa maadui, siku Yesu anapelekwa kwa Herode. Ndio siku ambayo urafiki wao ulirejea kwa upya, kilichosababisha wao wapatane ni Yesu Kristo.
Rejea: Basi siku ile ile Herode na Pilato walipatana kwa urafiki kwa maana hapo kwanza walikuwa na uadui wao kwa wao. LK. 23:12 SUV.
Haleluya, kumbe kushtakiwa kwa Yesu Kristo pasipo kosa lolote, kulizaa upatanisho kwa Herode na Pilato, kwa maana nyingine Yesu Kristo ni mpatanishi wa ulimwengu. Yale yameshindikana kibinadamu kwake yanawezekana, yaani kama kuna watu ulikuwa na ugomvi nao, umejaribu kila namna mpatane. Lakini badala yake hakuna kilichosaidia chochote.
Dawa ni moja tu, ni kumbeba Yesu moyoni mwako bila kujalisha hali zozote unazopitia, unapokuwa na Yesu moyoni mwako, utaishi maisha matakatifu, utakuwa mtu wa ibada, utakuwa mtu wa maombi, utakuwa mtu ambaye hapendi kuona vitu vibaya.
Unapompokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wako, mambo mengi sana yanaweza kuzaliwa katika hilo, unaweza kuwapatanisha maadui wa miaka mingi kupitia wewe.
Rejea:Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu; ambaye alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote, utakaoshuhudiwa kwa majira yake. 1 TIM. 2:5-6 SUV.
Ndugu msomaji wangu, hebu jiweke vizuri na Mungu wako, najua ipo changamoto katika hili, utakutana na maneno mengi yasiyo mazuri. Ninachokuambia ni kwamba, ukiwa mtu uliyesimama vizuri na Mungu wako kuna mahali utakuwa na vita kubwa sana na watu. Maana kuna kazi za shetani utakuwa unaziharibu, unapoziharibu kazi zake, moja kwa moja unakuwa adui wa watu wanaomtumikia shetani.
Mungu akusaidie usimame vizuri na Mungu wako ili uendelee kufanyika mpatanishi wa maadui wengi, wale ambao walishindwa kusameheana, wakapatane kwa ajili yako. Maana umelibeba jina la Yesu Kristo, mpatanishi wa ulimwengu mzima.
MUHIMU; kulijua Neno la Mungu ni muhimu sana, na ili ulijue vizuri unahitaji kusoma Biblia yako katika mtiririko mzuri, na hili limekuwa changamoto kubwa kwa wakristo wengi. Lakini ashukuriwe Mungu atupaye akili, kwanini nasema hivyo, tumekuandalia darasa zuri sana la kujifunza Neno la Mungu kila siku kwa mtiririko mzuri kabisa. Darasa hili linaendeshwa kwa njia ya whatsApp group, kama unapenda kujenga nidhamu ya kusoma Biblia yako bila kuachilia njiani, tuma ujumbe wako kwenda namba +255759808081 utaunganishwa.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com