Kitu mpaka kihitaji kufunguliwa kitakuwa kilikuwa kimefungwa, huwezi kufungua kisicho fungwa, na huwezi kufunga kisicho funga.
Akili au fahamu zetu zinaweza kufungwa tusiweze kuelewa kile tulichopaswa kuelewa, na akili/fahamu zetu zinaweza zikafunguliwa tukaweza kuelewa kile tulipaswa kuelewa.
Anayeweza kufunga akili zetu na kuzifungua ni Mungu mwenyewe, pia anayeweza kutufunga akili/fahamu zetu tusiweze kuelewa chochote kuhusu Yesu Kristo ni shetani.
Unaweza kumwona mtu ni msomi mzuri kabisa na ana nafasi kubwa kabisa katika jamii, ila ukashangaa ufahamu wake kwa mambo ya Mungu ni mdogo sana. Hata unapofanya bidii za kibinadamu kumwelewesha njia iliyo sahihi, anakuwa hakuelewi chochote.
Mtu kama yule ni msomi wa Dunia hii ila kwenye mambo ya kiroho, kuna eneo amefungwa ufahamu wake asiweze kuelewa kile alipaswa kukielewa. Kuhangaika naye kwa akili za kibinadamu utafika mahali utakwama tu.
Wapo watu wamefungwa ufahamu wao na Mungu mwenyewe kwa makusudi yake mwenyewe, hawa hawawezi kufanana na waliofungwa ufahamu wao na shetani. Maana nia ya shetani huwa ni mbaya siku zote.
Naomba uelewe hapa, sio kila mtu anaweza kusoma Neno la Mungu na akaelewa, ndio sio kila mtu anaweza kusoma Biblia takatifu akaelewa yaliyomo ndani. Wapo watu wanasoma lakini fahamu zao zimefungwa, kwa kuwa zimefungwa wanasoma vizuri lakini hawaelewi wanachosoma.
Watu kama hao wamefungwa ufahamu wao, kama hawajamkubali kumpokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yao. Shetani hawezi kuruhusu/kukubali watu hawa wafahamu maandiko matakatifu, maana anajua siri iliyopo kwenye maandiko matakatifu.
Kama umewahi kuchunguza au kama umewahi kuona, pale mtu alipopunguza uhusiano wake na Mungu, hata alipojaribu kusoma Neno la Mungu alishindwa. Mwingine alianza kuona uzito mkubwa wa kusoma Neno la Mungu.
Yupo mwingine anaacha kuona ile ladha ya Neno la Mungu wakati anasoma, wakati uhusiano wake na Mungu ulikuwa vizuri, alikuwa anasoma Neno la Mungu hadi anasikia nguvu ya Roho Mtakatifu inatembea ndani yake.
Kitu cha kwanza kabisa Shetani anachowinda kwa mtu ni kushika akili zake au fahamu zake, ndio unaweza kushangaa hawa ndugu kwanini wanang’ang’ania kwa nabii feki. Sio wao tena hapo, fahamu zao zimetekwa, na ili uweze kuwarejesha mahali sahihi ni kuwaombea fahamu/akili zao zifunguliwe.
Nakueleza haya kwa ufahamu wa Neno la Mungu, Neno la Mungu linatuthibitishia haya ninayokuambia hapa;
Rejea:Ndipo akawafunulia akili zao wapate kuelewa na maandiko. Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya. LK. 24:45-48 SUV.
Ndugu yangu, kama akili za hawa wanafunzi wa Yesu Kristo zilifunuliwa wakapata kuelewa maandiko matakatifu. Hata kwako zinahitaji kufunuliwa juu ya Neno la Mungu, juu ya mafundisho ya Neno la Mungu.
Pasipo kufunuliwa akili zako, utakuwa unaona mafundisho ya Neno la Mungu kama makelele, utakuwa unaona Neno la Mungu ni historia tu za zamani. Ili uweze kuelewa kile unasoma, akili zako zinapaswa kutiwa nuru ya Kristo.
Kama bado hajaokoka, unapaswa kuokoka, yaani kumpokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yako, kisha kubatizwa kwa maji na kwa Roho Mtakatifu.
Rejea: Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu. Yohana 3:5.
Tena andiko hili takatifu linatuthibitishia kuwa, hatuwezi kuuingia ufalme wa Mungu pasipo kuzaliwa kwa maji na kwa Roho Mtakatifu. Kazi kwako kuhakikisha unatimiza haki yote ili uweze kuuona ufalme wa Mungu.
MUHIMU; umeokoka na Yesu Kristo ni Bwana na mwokozi wa maisha yako? Tumekuandalia darasa zuri sana la kujifunza Neno la Mungu kila siku kwa mtiririko mzuri kabisa. Tena unajifunza kwa kusoma Biblia yako mwenyewe, lakini unakuwa kwenye usimamizi mzuri kupitia darasa hili. Ili uweze kuunganishwa unahitaji kuwa na simu yenye uwezo wa whatsApp, unayo hiyo simu, tuma ujumbe wako kwenda whatsApp namba +255759808081 utaunganishwa.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com