Huenda hili swali limekuwa likuzunguka kwenye fahamu zako, hujui ufanyaje kwenye hili, rafiki uliyenaye ni mzushi au mtu wa mafarakano sana. Mnaweza mkawa mpo kwenye kundi ambalo linamtukuza Mungu, linaweza likawa la maombi, linaweza likawa kundi la kujisomea shuleni, linaweza likawa kundi la kujisomea Neno la Mungu. Akawa ni chanzo cha mafarakano yenu.
Makundi ni mengi sana sio rahisi kuyamaliza yote, cha msingi liwe kundi nzuri lenye nia njema, na lisilomkosea Mungu wenu, hata sio la mambo ya kiroho, likawa la mambo ya kimwili kabisa. Kama halimkosei Mungu, hilo ni kundi zuri ambalo nia yake inaweza ikawa kufikishana mahali mkiwa pamoja kama kikundi.
Katikati ya kundi lenu mkawa mna mtu mmoja mzushi/mchonganishi au mtu wa mafarakano, kila mkijaribu kumwonya hataki kuacha hiyo tabia, mmemwonya mara ya kwanza, mara ya pili, au mmemwonya mara nyingi sana hadi hamkumbuki ni maonyo mangapi.
Mtu wa namna hiyo mnapaswa kuachana naye kabisa, Ikiwezekana kukaa naye mbali kabisa, maana bila kufanya hivyo ataendelea kuwa chanzo cha mafarakano yenu. Kama mlikuwa na nia ya kufika mahali, mtashindwa kufikia malengo yenu.
Kama haupo kwenye kikundi chochote ila una rafiki mzushi au mtu wa mafarakano, unapaswa kumwonya kuhusu hiyo tabia yake mbaya, ukishafika mara mbili, mkatae kabisa huyo rafiki. Mwachie Mungu mwenyewe adili naye, wewe utakuwa umenawa mikono yako.
Sasa kuna watu huwa wanaona wao wameokoka sana, kumbe ni kukosa maarifa sahihi ndani yao, laiti wangekuwa na Neno la Mungu mioyoni mwao. Wasingekuwa wanawakumbatia marafiki wa namna hiyo, wangeshawaepuka siku nyingi sana.
Biblia takatifu ipo wazi kwa hili ninalokueleza hapa, huenda ulikuwa hujui unachofanya, huenda ulikuwa hujui kadri unavyozidi kuambatana na mtu mzushi anakuharibu na wewe. Unapaswa kujua hilo leo, maana bila kujua unaweza kuendelea kumshikilia mtu mzushi au mtu wa mafarakano ukifikiri upo sahihi.
Rejea: Mtu aliye mzushi, baada ya kumwonya mara ya kwanza na mara ya pili, mkatae; ukijua ya kuwa mtu kama huyo amepotoka, tena atenda dhambi, maana amejihukumu hatia yeye mwenyewe. TIT. 3:10-11 SUV.
Neno linasema mwisho mara mbili, na huenda hapo ulipo mmemwonya zaidi ya mara mbili, huyo mtu mkatae kabisa, ukiwa unajua mtu kama huyo amepotoka na anatenda dhambi.
Usibaki kusema nitafanyaje, Neno la Mungu linasema ‘mkatae’ sijui kama utakuwa unataka jibu lingine tena, hili linatosha kabisa la umkatae. Maana kama umeshamwonya mara nyingi na bado hataki kuacha hiyo tabia, na anaendelea na uzushi/uchonganishi wake, mkatae kabisa mtu wa namna hiyo.
Kumkataa sio kana kwamba una chuki naye, ni kwa ajili ya usalama wako/wenu, kuendelea kumkumbatia atakuletea madhara ambayo hukutegemea kabisa. Na madhara hayo yakakuletea sifa mbaya kwa watu, wakati watu wanajua umeokoka.
Unachopaswa kufahamu mzushi yeyote ni mtu wa mafarakano, anaweza kuzusha ka kitu kadogo sana, nia yake sio kujifunza, nia yake ni kuwafanya mfarakane. Kufanya hivyo, kwake huwa ni kama inamletea furaha ndani ya moyo wake, sasa usikubali kumletea huyo mtu furaha inayotokana na mafarakano.
MUHIMU; kama unapenda kukua kiroho kwa kusoma Neno la Mungu kila siku, unakaribishwa sana kwenye kundi la kujisomea Neno la Mungu kila siku. Ili uunganishwe kwenye program hii ya kujifunza Neno la Mungu kwa kusoma mwenyewe, tuma ujumbe wako kwenda namba +255759808081 (tumia WhatsApp tu)
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com