Tupokuwa tunafundisha watu habari njema za Yesu Kristo, lengo letu huwa tunagemea tupate matokeo mazuri kwa yale tuliyokuwa tunafundisha. Lakini wakati mwingine huwa sivyo tulivyodhani iwe.

Tunaweza kutumia nguvu kubwa sana aliyotupa Mungu ndani yetu, hiyo nguvu ikaweka wazi kweli yote ya Mungu kupitia Neno lake tunalolifundisha kwa watu. Ukategemea kupata matunda mazuri kwa yale uliyokuwa unafundisha.

Badala ya kupata matokeo mazuri kwa wale uliokuwa unawafundisha habari njema za Yesu Kristo, katika kundi hilohilo likagawanyika katika sehemu mbili. Wapo wanafunzi watakukimbia kutokana na mafundisho yako, na wapo wanafunzi wataendelea kung’ang’ana na wewe kutokana na ukweli waliouona ukiufundisha.

Usipolijua hili unaweza kuacha kufundisha kweli ya Mungu, na kuanza kufundisha mafundisho ambayo hayagusi dhambi za watu, hayamfanyi mtu akamjua Yesu Kristo, hayamfanyi mtu akaukulia wokovu, hayamfanyi mtu akatamani kuzaliwa mara ya pili.

Unaweza kubaki na mafundisho fulani yenye kuleta furaha ya muda mfupi kwa watu, wakati mwingine unaweza kutafuta mafundisho yanayopendwa sana na watu wasiotaka kubadili njia zao mbaya. Ukayatumia hayo ili kuendelea kuwa na kundi kubwa la watu wasiomjua Kristo.

Pamoja na mafundisho hayo yanayopendwa na watu wengi, kuna watu wachache na wazuri utawapoteza kwa kufundisha mafundisho fulani yasiyo lenga kumbadilisha mtu. Unaweza kuonekana una kundi kubwa, lakini ambao wameokoka sawasawa hawafiki hata robo ya hilo kundi.

Wote wapo hapo kwa sababu ya mafundisho yako yasiyogusa dhambi zao, yaani huonyi kuhusu dhambi, hukemei kuhusu dhambi, hufundishi njia iliyo sahihi. Unachofanya wewe ni kupita juu juu ili usije ukakimbiwa na washirika wako.

Hili lilimkuta Yesu Kristo katika huduma yake hapa Duniani, watu wengi sana walikuwa wanaambatana naye kwa sababu ya miujiza yake mikubwa aliyotenda kwa watu mbalimbali.

Pamoja na kutenda miujiza hiyo, Yesu Kristo hakuacha kufundisha kweli ya Mungu, hiyo kweli aliyofundisha yapo mambo ambayo hayakuwapendeza wengine. Waliamua kuondoka kabisa na kumwacha Yesu Kristo na wanafunzi wake kumi na mbili.

Wale wanafunzi wengine ambao walikuwa kundi kubwa, walitawanyika wenyewe kutokana na mafundisho sahihi ya Neno la Mungu. Yesu akawauliza wanafunzi wake, wale kumi na mbili, Je! Ninyi nanyi mwataka kuondoka?

Rejea:Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena. Basi Yesu akawaambia wale Thenashara, Je! Ninyi nanyi mwataka kuondoka? Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu. YN. 6:66‭-‬69 SUV.

Ndugu, huenda ulikuwa na bidii sana katika kuifundisha kweli ya Mungu isigushiwa na chochote, lakini ulifika mahali ukaacha kufundisha kweli ya Mungu kupitia Neno lake. Huenda kutokana na mashambulizi makali uliyokutana nayo, huenda kutokana na kuona unakosa washirika, huenda kutokana na kuona unakosa marafiki wa kukusaidia katika huduma yako.

Aliyekutuma anajua unahitaji nini, huna haja ya kuacha kufundisha kweli ya Mungu, usitishwe na mazingira unayokutana nayo. Endelea kumtumikia Mungu wako kwa uaminifu, iseme kweli ya Mungu, watu waamue kuokoka au kupuuza kuokoka ila wewe utakuwa umetimiza agizo la Mungu.

Yesu Kristo hawezi kukuondolea watu wote, wale waliokusudiwa na Mungu wataendelea kubaki na wewe, cha msingi ni wewe kuendelea kuwapa chakula kilichoiva sawasawa. Wanayo kiu ya maneno ya Mungu ndio maana wamekubali kuambatana na wewe, bila kujalisha wapo walioondoka.

Kupitia hilo kundi dogo, Yesu Kristo atawaleta wengine wengi wanaopenda mafundisho sahihi, maana wapo wanatafuta mafundisho sahihi lakini wanapata wakati mgumu kuyapata. Siku wakifahamu kuna mahali sahihi panafundishwa kweli ya Mungu, uwe na uhakika wataambatana na wewe.

Ndio maana tunasema kusoma Neno la Mungu ni muhimu sana, haya yote unayapata kupitia Neno la Mungu. Kama unahitaji kusoma Neno la Mungu kila siku kwa mtiririko mzuri, na hilo unaona ni changamoto kwako, unakaribishwa kwenye group la whatsApp la Chapeo Ya Wokovu, kupitia hili group utasimamiwa vizuri kuhakikisha unasoma Biblia yako kila siku. Ili uweze kuunganishwa, tuma ujumbe wako whatsApp +255759808081.

Mungu akubariki sana.

Ndugu yako katika Kristo,

Samson Ernest.

www.chapeotz.com