Unaweza ukawa njia panda pale unapofika wakati wa kutoa habari zako mwenyewe, unaweza kuona labda ni vibaya kujisemea mwenyewe au unaweza ukawa unaona ukisemewa na watu ni vizuri zaidi.

Unapoacha watu wakusemee kuhusu wewe, sio kana kwamba kila kitu wanakijua, wanaweza wakakusemea tofauti kabisa na vile ulivyo. Na wanaweza kukusemea nusu ya wanayoyajua wakidhani wanajua kila kitu.

Wanasema ni vizuri watu wakakusemea kuliko wewe kujisemea, inaonekana unapojisemea mwenyewe ni kujiinua kabla hujainuliwa. Kwa hiyo watu wakisema fulani ni mtu mzuri, wakafika watu wawili watatu, haimaanishi huyo ni mzuri kweli. Unaweza ukawa ni mpango uliotengenezwa kwa ajili ya kumsafisha kwa watu.

Watu wanaposema fulani mbaya, wakafika watu wengi wenye kusema hivyo, haimaanishi moja kwa moja huyo mtu anayesemwa ni mbaya, akawa mbaya kweli. Maana inaweza ikawa ni njama iliyotengenezwa kumchafua mtu asiye na hatia yeyote.

Mtu anapokushuhudia wewe au mtu mwingine, unapaswa kuwa makini sana kusikiliza na kuchuja maneno yanayozungumzwa. Haijalishi huyo mtu anashuhudiwa kwa mabaya au kwa mema, unapaswa kuwa makini sana.

Rahisi kumwamini mtu kwa kushuhudiwa uongo, kumbe ni mtu salama kabisa isipokuwa kuna watu hawampendi, ndio maana wanatengeneza ushuhuda wa uongo ili watu wamwone hafai, wakati anafaa.

Pia unaweza kupewa ushuhuda wa ukweli kuhusu mtu fulani, alafu ukakutana na mtu mwingine ukamuuliza, bila kujua uliyemuuliza ni adui wa mtu uliyeambiwa ni mtu mzuri. Ushuhuda ule wa ukweli unaweza usiwe na nguvu tena kwako kutokana na Dunia leo ilivyokosa uaminifu kwa mambo mbalimbali.

Hadi hapo unaweza kuona kwamba kuacha watu wakushuhudie wenyewe bila wewe kusema chochote, wakati mwingine inaweza ikawa si salama sana kwako. Na wakati mwingine inaweza ikawa ni nzuri sana kwako kama watu wanakufahamu, na hao wanaokufahamu wakawa ni watu wazuri wasio na hila mioyoni mwao.

Hupaswi kukaa kwenye eneo moja, kwamba anayejishuhudia mwenyewe si mtu mzuri, kwa kujiuliza kwanini ajisemee mwenyewe na si watu wengine. Na ukawa unafikiri anayeshuhudiwa na watu ndio mtu sahihi, maana hajisemei mwenyewe.

Mtu anaweza kutengeneza watu wake wa kumsifia tu na akawa anawalipa pesa nyingi tu, kwa kuwa ufahamu wako umeufunga mwenyewe sehemu moja utaona huyo ni mtu sahihi kwako, kwa sababu amesifiwa na wengine.

Kujishuhudia mwenyewe ni nzuri sana, na wakati mwingine sio nzuri sana, lazima ujue maeneo yote mawili vizuri, ni nzuri, na ni mbaya. Unaweza ukajisifu kuwa wewe ni mtu fulani wa kiwango cha juu, alafu watu wakija kukufuatilia wanakuja kujua ulichokuwa unakisema ni cha uongo.

Na unapojishuhudia mwenyewe unaweza kujisemea vizuri sana kuliko mtu mwingine, maana unajijua mwenyewe vizuri sana kuliko idadi kubwa inayozani inakufahamu wewe vizuri. Inaweza kuwa katika watu kumi wanaofikiri wanakufahamu vizuri, yupo mtu mmoja tu kati ya hao anayekufahamu kwa undani kidogo. Hawa wengine tisa wakawa wanajidanganya tu.

Hili tunajifunza kwa Yesu Kristo aliye hai, kuna wakati alikuwa anajishuhudia mwenyewe kuwa ni nani. Kujishuhudia huko mwenyewe, Mafarisayo walimwona ni muongo, kwa sababu walijua anayejisemea mwenyewe atakuwa muongo, na anayesemewa/anayeshuhudiwa na watu wengine atakuwa ni mtu sahihi.

 

Pamoja na kumwona Yesu Kristo ushuhuda wake si wa kweli, hilo halikuweza kubadilisha ukweli wa mambo yote. Ushuhuda wa Yesu Kristo ulikuwa ni kweli tupu, bila kujalisha wangapi wanaupinga.

Rejea: Basi Mafarisayo wakamwambia, Wewe unajishuhudia mwenyewe; ushuhuda wako si kweli. Yesu akajibu, akawaambia, Mimi ningawa ninajishuhudia mwenyewe, ushuhuda wangu ndio kweli; kwa sababu najua nilikotoka na niendako; lakini ninyi hamjui nilikotoka wala niendako. YN. 8:13‭-‬14 SUV.

Kuwa makini sana, wala usikariri jambo lolote ambalo sio Neno la Mungu, hekima za Dunia zinaweza zikakuangamiza kabisa. Kwanini nakuambia hivyo, unaweza kukaa kwenye eneo moja ukifikiri ndio ipo hivyo, kumbe sivyo hivyo.

Hawa Mafarisayo walijua mtu anayejishuhudia mwenyewe, mtu huyo, ushuhuda wake utakuwa si kweli. Wakawa wamekaa katika sura hiyo, kumbe walikuwa wamejifungia kwenye maarifa ambayo yanawanyima fursa ya kujua mengi zaidi.

Yesu Kristo alikuwa anawashuhudia habari zake za kweli kabisa, kama ilivyo leo mtumishi wa Mungu anaweza kuishuhudia kweli ya Mungu iliyo sahihi. Pasipo kuingiza upotoshaji wa aina yeyote ile, alafu wakainuka watu wakasema huyu mtu ananena uongo.

Na vile vile anaweza akainuka mtu anayejiita mtumishi wa Mungu, akawa anashuhudia habari zisizo za kweli, watu wakasema huyu ndiye mtumishi wa Mungu wa kweli. Kumbe ni mpotoshaji tu wa injili ya Yesu Kristo.

Hadi hapo nina imani utakuwa umepata elimu ya kukusaidia katika maisha yako ya wokovu, hii ndio faida ya kujifunza Neno la Mungu. Nikusihi kama huna ratiba nzuri ya kusoma Neno la Mungu kila siku, anza leo kuwa na ratiba nzuri ya kusoma Neno la Mungu.

Mungu akubariki sana.

Ndugu yako katika Kristo,

Samson Ernest

www.chapeotz.com