Tunaweza kuwa na sababu nyingi za mtu kuzaliwa kilema, au kuwa kilema ghafla wakati alikuwa mzima kabisa, tunaweza tukawa na sababu za kiafya kuwa mtu huyo hakuwa makini na afya yake.

Tunaweza kuwa na sababu nyingine ya mtu huyo alimtenda dhambi Mungu ndio maana akapigwa upofu wa macho, ama akawa hawezi kutembea tena kwa miguu yake. Akawa mtu wa kukaa tu.

Tunaweza kusema amezaliwa kipofu wa macho au kilema wa miguu kwa sababu wazazi wake walimtenda Mungu dhambi, kutokana na tabia walizokuwa nazo wazazi wake.

Tunaweza kuona wazazi wamezaa watoto wenye ulemavu wa ngozi, tukaanza kusema ni laana au pigo la Mungu kwa wazazi hao. Kutokana na tabia chafu tulizokuwa tunaziona kwao, maana ni watu tunaoishi nao kwa karibu.

Tunaweza kusema mambo mengi sana, hasa pale tulipokuwa tunamfahamu mtu ni mzima kabisa wa afya yake. Ghafla akapoteza uwezo wa macho yake kuona(kipofu), mwingine alikuwa anatembea vizuri kabisa, tukaanza kumwona anatembea na baiskeli za vilema wa miguu.

Kwa vyovyote vile tunaweza kumtegenezea sababu nyingi sana, wapo tutasema alimtenda Mungu dhambi mbaya, kwa hiyo hilo ni pigo la Mungu. Na wengine tutasema wazazi wake walimkosea Mungu, hasa kama tunawafahamu walichukuana/walibebana kienyeji pasipo kufunga ndoa.

Pamoja na kuwaza mambo hayo yote, tunaweza tukawa kinyume kabisa na vile tunawawazia watu hao waliopata matatizo mpaka ikapelekea kuwa kilema. Tunaweza kuwa kinyume kuwaza wazazi wao walimtenda Mungu dhambi ndio maana wakazaa mtoto kilema.

Mtu kuzaliwa kilema wa macho, miguu, mikono, sio kana kwamba kuna dhambi ilitendeka au ni laana fulani, wakati mwingine ni mipango ya Mungu mtu huyo azaliwe hivyo. Lipo kusudi la Mungu kupitia huyo mtu, ili kazi ya Mungu idhihirishwe kupitia yeye.

Rejea: Hata alipokuwa akipita alimwona mtu, kipofu tangu kuzaliwa. Wanafunzi wake wakamwuliza wakisema, Rabi, ni yupi aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake, hata azaliwe kipofu? Yesu akajibu, Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake; bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake. YN. 9:1‭-‬3 SUV.

Uwezekano upo kabisa mtoto wako tangu mzae shingo yake haijawahi kutengamaa, anaweza kuwa ana mwaka mmoja, au wa pili, au wa tatu sasa. Lakini bado shingo yake haijakomaa kabisa, usiwaze tu ulimtenda Mungu dhambi, waza pia mapenzi ya Mungu juu ya mtoto wako.

Unaweza kuzitafuta dhambi hadi za mababu na mababu, kutokana na shida inayomkabili mtoto wako, ndugu yako, jirani yako, mume wako, mzazi wako. Ukawa unajisumbua tu mwenyewe, ikawa hakuna dhambi yeyote uliyofanya/aliyofanya huyo mtu.

Mungu anataka ajitwalie utukufu wake, na atajitwalia kweli pale tu huyo kilema atakapopokea uponyaji wake. Kwa hiyo kilema chako kinaweza kikawa kwa ajili ya kudhihirisha kazi za Yesu Kristo.

Usije ukaacha wokovu kwa sababu umeombewa sana ukashindikana kupona, usije ukaona mahali unaposali hakuna upako wowote ndio maana shida yako imeshindwa kukuachia. Shida yako hiyo imeshindwa kukuachia kwa kusudi maalum kama tunavyojifunza kwa kipofu huyu aliyeponywa na Yesu Kristo.

Kuna mtumishi wa Mungu mahali anadharauliwa sana, Mungu anataka kumdhihirisha kwa watu wake kuwa huyu ni mtumishi wangu. Atamdhihirishaje sasa? Kupitia shida yako ngumu iliyoshindikana kwa waganga wa kienyeji, na kwa maombi mengi ya watakatifu wa Bwana.

Kushindwa kuona kwako kunaweza kuwa ni kwa kazi maalum iliyoandaliwa na Mungu wako, kupitia wewe utamtambulisha mtumishi wa Mungu pale tu atapokuwekea mikono ukapokea uponyaji wako. Ili jina la Yesu Kristo litukuzwe kupitia uponyaji wako.

Fahamu na hili litakusaidia sana katika maisha yako ya wokovu, hata pale utakapoombea mtu akashindwa kupona, usije ukaanza kufikiri huna upako wa kutosha. Mungu amezuia kupona ili aje ajidhihirishe kwa mtu wake fulani, usiyemjua wewe kwa wakati huo.

Maarifa haya adimu, yanapatikana ndani ya Neno la Mungu pekee, nakusihi uwe na ratiba nzuri ya kusoma Neno la Mungu kila siku. Na kama una changamoto ya kusoma Biblia yako katika mtiririko mzuri, Chapeo Ya Wokovu whatsApp group ni jibu lako, tuma ujumbe wako kwenda namba +255759808081.

Mungu akubariki sana.

Ndugu yako katika Kristo,

Samson Ernest

www.chapeotz.com