Kuajiri watu kwenye ofisi yako kuna changamoto zake nyingi, wengi wao unaowaajiri hutazama mshahara wao tu. Hawana muda wa kuangalia usalama wa mali zako ukoje, wakishamaliza majukumu yao, wanahitaji uwalipe mshahara wao.

Likitokea janga la kuteketeza mali zako, badala ya kuwaza kuokoa mali zako, wao watakuwa wanawaza itakuwaje pesa zetu. Wakati wewe mwenye mali unahaingaika kuokoa mali zako, wao wanawaza pesa zao.

Mfano leo bank fulani ipate shida, idadi kubwa ya wafanyakazi wa humo hawatakuwa na maumivu ya hasara iliyopatikana kutokana na shida iliyotokea. Wengi wao watakuwa wanaugua kwa kukosa uhakika wa kulipwa mishahara yao.

Watu wa mshahara wana tabu zake nyingi sana, tofauti kabisa na mtu ambaye ameajiriwa alafu anaangalia mali zako kama za kwake, na tofauti na wewe unayejituma kwenye mali zako mwenyewe.

Anayefanya kazi ilimradi mshahara wake uingie, ikitokea siku mharibifu akavamia mali zako, uwe na uhakika mtu huyo atakimbia mali zako. Hatakuwa na msaada wa kuweza kuiokoa mali zako, hata kama hutoamini hichi ninachokuambia hapa, fahamu hilo.

Hujawahi kukutana na mwalimu shuleni anasema maneno haya? Uelewe usielewe, uje shuleni usije, mshahara wangu upo pale pale au unaingia kama kawaida. Maana yake ufaulu au usifaulu kwake sio shida, mshahara wake utaingia kama kawaida. Sio kama anaongea uongo, ni kweli anachosema.

Huyu mwalimu hana kujali moyoni mwake, hana wito wowote juu ya kazi yake, yeye ni mwalimu wa mshahara tu, mwalimu huyu wa mshahara hawezi kuwa na uchungu na wanafunzi wake. Tofauti kabisa na mwalimu mwenye wito na kazi yake, anayepambana usiku na mchana kuhakikisha wanafunzi wake wanaelewa anachofundisha na kufaulu.

Ndivyo ilivyo na wachungaji wa mshahara, wao huwa hawajali sana washirika wao, hata kama wanafanya vitu vya kuwaangamiza maisha yao ya kiroho na kimwili. Huwa hawajali hilo, wanachojali wao ni sadaka ya mshirika wake, hapo ndio huwa mkali na makini sana.

Mchungaji wa mshahara hawezi kunyimwa usingizi na mshirika wake anayefanya vitendo viovu, tena hawezi kuwa na ujasiri wa kumwita na kumwonya, na hawezi kuumiza kichwa kumtafutia mshirika huyu chakula cha kumsaidia kukua kiroho. Mchungaji huyu atahaingaika kutafuta mafundisho ya utoaji tu.

Watu wa mshahara wanaliletea hasara sana taifa letu, na wanaliletea hasara kanisa, watu hawa hawawezi kuwa wabunifu kwenye kazi zao, wala hawezi kuwa na uchungu na majukumu waliyopewa. Uchungu wao huwa pale wanapoona wanaenda kupoteza nafasi zao la ulaji au wanapoona sadaka zimepungua.

Watu wa mshahara walikuwepo tangu zamani, Yesu Kristo aliwajua na akaamua kutuweka wazi kupitia Neno lake. Haya ninayokueleza yapo kimaandiko usifikiri ni maneno ya kutunga, hapana, watu wa mshahara wanajulikana sifa zao.

Rejea: Mtu wa mshahara, wala si mchungaji, ambaye kondoo si mali yake, humwona mbwa-mwitu anakuja, akawaacha kondoo na kukimbia; na mbwa-mwitu huwakamata na kuwatawanya. Yule hukimbia kwa kuwa ni mtu wa mshahara; wala mambo ya kondoo si kitu kwake. YN. 10:12‭-‬13 SUV.

Hebu jihoji mwenyewe, kama umeajiriwa mahali, Je! Unafanya kazi kama ya kwako au kama ya mwajiriwa? Kama unafanya kazi kama umeajiriwa, hiyo kazi utafanya kawaida sana na huwezi kuokoa mali za mwajiri wako pale itapotokea shida.

Jihoji pia kama wewe ni mtumishi wa Mungu, huo utumishi wako unatumika kama wito wako, au uliingia kwenye utumishi kwa sababu uliona maisha magumu. Ukaona sehemu pekee ya kupata fedha nyingi ni kuwa mchungaji, nabii, mtume, mwinjilisti, ama mwalimu wa Neno la Mungu.

Ama uliingia kwenye utumishi kwa kuona mtumishi fulani ana mafanikio makubwa ya kimwili, ukaona na wewe uingie kwenye utumishi ili uwe kama yule uliyemwona wewe. Lakini ndani yako kabisa hakuna wito wa kiMungu kutumika kwenye nafasi uliyonayo.

Majibu ya hayo maswali yote unaweza ukawa nayo kabisa ndani yako, maana wewe unajijua vizuri ndani yako, kama huduma unayofanya unasukumwa na wito au unasukumwa na malipo ya mwisho wa mwezi au kila jpili una uhakika wa kupata fedha baada ya ibada kuisha.

Hebu kuwa mchungaji mwema, unayehakikisha kondoo zako wanachunga vizuri na kushiba, na kuwalinda na mbwa mwitu. Na kuwa mwajiriwa mwadilifu anayeangalia mali za mwajiri wake kama kitu chake, utaona mafanikio makubwa sana kwenye utumishi wako unaoufanya.

Penda kujifunza Neno la Mungu kwa kulisoma na kulitafakari, Neno la Mungu ndio dira sahihi ya maisha yetu ya kiroho na kimwili. Hakikisha siku haipiti bila kusoma Neno la Mungu, na kama una changamoto ya kusoma Biblia yako, karibu Chapeo Ya Wokovu whatsApp group, utasimamiwa vizuri kuhakikisha unasoma Biblia yako. Tuma ujumbe wako whatsApp kwenda +255759808081 utaunganishwa.

Mungu akubariki sana.

Ndugu yako katika Kristo,

Samson Ernest

www.chapeotz.com