Wakati watu wengine wanazidi kupokea majibu ya maswali yao kupitia huduma yako, na wakati watu wengine wanazidi kufunguliwa katika vifungo mbalimbali vya shetani kupitia kazi yako ya utumishi. Kuna watu wataifurahia huduma yako inayomwinua Kristo mbele za watu wengine waliovunjika mioyo yao.

Kadri unavyozidi kutumiwa na Mungu wako katika huduma, miujiza mbalimbali inatendeka, watu wanaokoka, vilema/viwete wanatembea, vipofu wanaona, viziwi wanasikia, wenye kisukari wanapona, wenye mapepo wanafunguliwa, na mengine mengi ya kufanana na hayo.

Usije ukafikiri kila mmoja atafurahia hayo, hasa wakuu wa dini, wanaweza kuona kwa uwazi kabisa siku za mbeleni hawatakuwa na washirika/waumini. Washirika wote watakuwa wamekimbilia mahali ambapo wanamwona Yesu Kristo anahubiriwa habari zake, mahali ambapo wameona wanatoka hatua moja kiroho kwenda hatua nyingine kubwa.

Wasiokoka wanahubiriwa habari njema za Yesu Kristo, wengi wao wanakimbilia kumpokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wao. Na wakishampokea hawataweza kurudi tena mahali ambapo walikuwa wanafichwa habari za Yesu Kristo.

Huduma ya namna hiyo haitakubalika kwa wakuu wa dini, lazima utakaliwa vikao wajue ni namna gani wataweza kukabiliana na wewe haraka. Ili usiendelee kuleta madhara makubwa zaidi kwa washirika/waumini wao.

Kadri unavyozidi kumfurahia Yesu Kristo anavyokutumia kuwarejesha watu wengi kwake, usifikiri hicho kitendo kitafurahiwa na watumishi wengine. Utumishi wako mzuri mbele za Mungu unaweza kusababisha wakuu kuanza kupanga mipango mibaya dhidi yako.

Unaweza kushangaa hata kanisani kwako vita kubwa ikanuka dhidi yako, kama una mchungaji wa mshahara, ataanza kuona unataka kuchukua nafasi yake. Kumbe ulikuwa hufikiri kabisa hilo jambo, ila huduma yako itakuletea vita vyote hivyo.

Usipokuwa makini, shetani anaweza kutumia nafasi hiyo kukuvunja moyo, unashangaa ulikuwa vizuri kumhubiri Yesu Kristo. Ghafla unaacha kufanya hivyo, ulikuwa umesimama vizuri, unavunjika moyo na kuwa mtu wa kawaida kabisa.

Hupaswi kuogopa unapokutana na changamoto kama hii, maana Yesu Kristo anajua ipo vita ya namna hiyo na yeye aliishinda wakati yupo Duniani. Kama aliishinda na sisi tutashinda, maana tunaye ndani yetu, nasi tupo ndani yake, hakuna jambo lolote litaweza kutushinda, amini hivyo.

Rejea: Basi wakuu wa makuhani na Mafarisayo wakakusanya baraza, wakasema, Tunafanya nini? Maana mtu huyu afanya ishara nyingi. Tukimwacha hivi, watu wote watamwamini; na Warumi watakuja, watatuondolea mahali petu na taifa letu. YN. 11:47‭-‬48 SUV.

Songa mbele, mhubiri Kristo pasipo kumwogopa mtu yeyote, wewe chapa injili ya Yesu Kristo watu wampokee kama Bwana na mwokozi wa maisha yao. Wale waliofungwa wapate kufunguliwa katika vifungo vyao, na wale waliovunjika mioyo yao wapate kuinuliwa tena.

Hakuna kurudi nyuma, acha wakuu wa dini wakuletee vipingamizi vingi, hawakupingi wewe kama wewe, wala hawashindani na wewe, wanashindana na aliyekutuma. Hivyo vita lazima ushinde, na wao lazima washindwe.

Yupo anayekutetea katika huduma yako, muhimu ni wewe kusimama katika kusudi lake, usiyumbishwe na jambo lolote linalokuja au linalojitokeza mbele yako. Endelea kumtumikia Mungu wako, ipo taji yako ya ushindi siku ya mwisho usipozimia moyo njiani.

Ukiwa kama mtumishi wa Mungu, una wito ndani yako, na kile Mungu amekupa ndani yako unakitumia kwa moyo wako wote, kwa nguvu zako zote, kwa roho yako yote, kwa akili zako zote. Hakikisha siku haipiti bila kusoma Neno la Mungu, Neno la Mungu ni hazina njema ya moyo wako, hazina ya moyo wako haipaswi kupungua hata kidogo.

Ukipungukiwa na hazina ya Neno la Mungu, anguko lako linaweza kuwa rahisi sana, utashangaa mtego mdogo unakunasa na kukuangusha dhambini. Usikubali kunaswa na mtego wa aina yeyote ile, lipo Neno la Mungu likupalo maarifa mazuri ya kukusaidia kuishinda mitengo ya mwovu shetani.

Kama una changamoto ya kusoma Biblia yako katika mtiririko mzuri, karibu sana Chapeo Ya Wokovu whatsApp group tutakusimamia kuhakikisha unasoma Biblia yako sura kwa sura, mstari kwa mstari. Ili uunganishwe kwenye program hii, tuma ujumbe wako whatsApp kwenda +255759808081.

Mungu akubariki sana.

Ndugu yako katika Kristo,

Samson Ernest

www.chapeotz.com