Chukua hatua sasa.

Kama kuna vitu huwa tunajidanganya ni pale tunapoacha kuchukua hatua, kwa kujiambia nitaanza kesho au nitafanya kesho au mwaka mpya ukifika. Badala yake hiyo kesho inafika hatufanyi kama tulivyosema, na mwaka mpya ukifika huwa tunaanza kwa muda mfupi tunakuwa tumerudi kwenye maisha yetu ya nyuma.

Mtu ana uwezekano wa kuacha pombe leo, lakini anajiambia ataacha kesho au mwaka mpya ukifika ataanza ukurasa mpya wa maisha. Mwaka unafika anajikuta bado anaendelea na unywaji wake wa pombe au anaacha siku mbili tatu, anarudia unywaji wake wa pombe.

Mtu ana tabia fulani asiyoipenda, badala ya kuiacha wakati huo alionao, anaanza kujiambia ataacha kesho, kesho inafika anasogeza kesho nyingine tena. Zinakuwa kesho za kutosha hadi anaamua kukaa kimya mwenyewe.

Yupo mwingine anasubiri mwaka huu uishe, utapofika mwaka mpya ndio aanze kusoma Neno la Mungu, anaamini mwaka mpya ndio utamsaidia kuwa na nidhamu ya kusoma Neno la Mungu. Kweli mwaka mpya utafika, lakini huyu ndugu mwezi wa tatu mbali utamwona amerudi kwenye maisha yake ya kutokusoma Neno la Mungu.

Yupo mwingine ana huduma ndani yake na anaweza kuanza kumtumikia Mungu kwa hatua ndogo aliyonayo sasa, hataki kuanza na hiyo hatua ndogo. Anasubiri awe na hatua kubwa zaidi ya hapo alipo, wakati hata ile ndogo ameshindwa kuitumia.

Mwingine anasikia msukumo wa kuokoka, lakini kila akitaka kuokoka anasikia sauti nyingine inamwambia okoka kesho, utaokoka mwaka mpya. Ile sauti ya okoka sasa hivi inakuwa inashindwa nguvu na ile ya kesho na mwaka mpya, anajikuta anaendelea na maisha yake.

Ndugu yangu, huenda una malengo mengi sana katika maisha yako, na katika malengo hayo, mengi unaweza kuanza sasa hivi, wala huhitaji mwaka mpya, wala huhitaji uanze kesho. Hapo ulipo unaweza kuchukua hatua hadi unafika mwaka mpya utakutwa umeshafika mbali.

Wakati kelele za mwaka mpya zinafika, watu wakiwa wanajiwekea mipango mingi, wewe utakuwa umewaacha hatua nyingi mbele. Na huko mbele mtakuwa wachache mnaomaanisha kwa kile mnafanya.

Neno la Mungu ndilo linalotusihi na kutuambia wakati uliokubalika ni sasa, na sio kesho, wala mwaka mpya, usifikiri ni maneno ya watu waliokaa wakaona yanafaa kutumiwa na watu.

Rejea: (Kwa maana asema, Wakati uliokubalika nalikusikia, Siku ya wokovu nalikusaidia; tazama, wakati uliokubalika ndio sasa; tazama, siku ya wokovu ndiyo sasa.)2 KOR. 6:2 SUV.

Sio kila kitu unapaswa kusubiri kesho au mwaka mpya, yapo mambo unapaswa kufanya sasa, au unapaswa kuanza kuchukua hatua sasa.

Unaweza kusema utaokoka kesho au mwaka mpya, na usifike hiyo kesho au usifike huo mwaka mpya, fahamu wakati uliokubalika ni sasa, kama hujaokoka, siku ya wokovu wako ndiyo sasa.

Anza sasa malengo/mipango yako, na kujiwekea ukomo wa mwezi fulani, utapofika mwezi fulani uwe umemaliza. Ukijiwekea hivyo utakuwa unajisukuma kwa nguvu zako zote kufikia malengo yako.

Kuliko hii ya kujiambia utaanza jambo fulani au utachukua hatua fulani mwaka mpya, wakati huo umekaa tu, hujishughulishi na jambo lolote, kisa unasubiri kesho au mwaka mpya. Utashangaa utakuwa unaimba kila siku wimbo ule ule bila kuchukua hatua yeyote, huku wenzako wakisonga mbele.

Anza sasa kusoma Neno la Mungu kwa kuungana na wenzako ambao hawasubiri mwaka mpya uanze, wao wameshaanza safari ya kusoma Neno la Mungu kila siku. Unaweza kuungana nao kwa kujiunga na kundi la whatsApp la Chapeo Ya Wokovu, tuma ujumbe wako whatsApp +255759808081 utaunganishwa.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com