Marafiki walioshibana vizuri, wanaopendana kweli pasipo unafiki, marafiki hawa wanaweza kushirikishana mambo mengi sana pasipo kuwa na shaka na mwenzake.

Hata inapotokea mmoja wao amekosea, huwa wanaambiana ukweli na uwazi, wakati mwingine inaweza isionekana kwao kwa uwazi sana pale wanaporekebishana. Maana wapo kitu kimoja, hakuna anayemwona mwenzake ni adui, wala hakuna anayejisikia vibaya pale mwenzake anapomrekebisha.

Yapo mambo mazuri wanaweza kushirikishana na kusaidiana kimawazo na kifedha pia, hakuna kati yao atakubali mwenzake alemewe na jambo pasipo kumsaidia mwenzake.

Wakati watu wengine wameungana kwa urafiki wa mambo mazuri, wapo wengine wameungana kwenye urafiki kwa mambo mabaya. Urafiki wao umeunganishwa na vitu visivyofaa, wanashauriana kumtenda Mungu dhambi, wanaunganishana vitu ambavyo havifai kabisa mbele za Mungu.

Kama ni mama/dada anakuwa anatumika kuwaunganisha marafiki zake na wanaume wenye tabia chafu, mama/dada huyu anakuwa kiunganishi wa kuwasihi marafiki zake watembee na wanaume wale kimapenzi(uzinzi/uasherati)

Mwanaume akiwa na shida na dada fulani na anajua rafiki yake ni dada/mama fulani, anamtumia nafasi ya mama/dada yule kumwomba amfikishie ujumbe wake. Anaweza kuahidiwa malipo atapofanikisha mpango huo, na huyu mama/dada akatumia nguvu ya urafiki wao kumshawishi rafiki yake atembee na mwanaume huyo.

Unaweza kuona ni jinsi gani urafiki unavyoweza kutumika vibaya, na matokeo yake yakawa mabaya sana kwa yule aliyeunganisha na mtu mbaya. Ukiangalia watu wengi wameingia kwenye mahusiano mabovu, kwa sababu ya ushawishi wa marafiki zao, walikuwa na urafiki na mtu asiye na Yesu Kristo sawasawa, huyo mtu akamwingiza kwenye matatizo.

Wapo marafiki wazuri ambao unaweza kuwatumia kufikisha ujumbe wako, unaweza kukuta kuna mtu huwezi kumweleza jambo lako moja kwa moja. Na mtu huyo akawa na rafiki yake walioshibana na kuheshimiana, unaweza kumtumia rafiki yake kumweleza lile ambalo unataka limfikie rafiki yake.

Nikitoa mfano huu ninaweza kueleweka vizuri zaidi, kama kuna kaka anataka kumwoa dada fulani, na kaka huyo akawa hana ujasiri wa kwenda kumweleza huyo dada anayempenda. Kwa kuhofia kupewa majibu hasi na binti, kaka huyu anaweza kumwomba mama walioshibana na dada yule kumfikishia ujumbe wake.

Hapa kuna changamoto kama kaka huyu atakutana na mama asiye sahihi, mama asiye na Roho wa Mungu ndani yake, mama asiyejiheshimu, au mama ambaye anaona kwanini asimwoe binti yake. Anaweza kumchafua kwa dada aliyempenda au anaweza asifikishe ujumbe husika.

Kama ni dada ndio ametumwa na kaka kwa rafiki yake na huyu dada sio mwaminifu, anaweza kuona wivu na kujiuliza kwanini rafiki yake amepata mwanaume mzuri, na kwanini huyo mwanaume asiwe wa kwake. Anaweza kugeuza kutumwa kwake kumchafua rafiki yake ili yeye aolewe, sasa hawa sio wale marafiki wa ukweli.

Wakati mwingine ni vizuri kwenda wewe kama wewe, ila kama kuna mahali unaona unakwama na unafikiri unahitaji msaada wa mtu mwingine. Usiwe na hofu ndio lengo kubwa la kukuletea somo hili, ili uweze kupata ufahamu mzuri, huenda ulikuwa unaona ni vibaya kutokana na mafundisho uliyokuwa nayo.

Nimekutolea mfano wa mahusiano ila mifano ipo mingi nje na mahusiano, ambapo tunaweza kuwatumia watu wengine kutufikishia ujumbe wetu kwa marafiki zao. Wale tunaohitaji jambo fulani kwao, huenda hatuna kabisa uhusiano wowote nao, au huenda hawatufahamu kabisa, au wanatufahamu ila tunaona ni ngumu kueleweka kwao. Sasa ni vyema tukatumia urafiki wao na wale tunaowalenga kutufikishia ujumbe wetu.

Hili tunajifunza kwa wanafunzi wa Yesu Kristo, Yesu Kristo alikuwa na mwanafunzi mmoja aliyempenda sana, Simoni Petro alimtumia mwanafunzi huyo aliyempenda Yesu. Kumwambia amuulize ni nani aliyekuwa anamzungumzia, yaani yule atakayemsaliti.

Rejea: Wanafunzi wakatazamana, huku wakiona shaka ni nani amtajaye. Na palikuwapo mmoja wa wanafunzi wake, ameegama kifuani pa Yesu, ambaye Yesu alimpenda. Basi Simoni Petro akampungia mkono, akamwambia, Uliza, ni nani amtajaye? Basi yeye, hali akimwelekea Yesu kifua chake, akamwambia, Bwana, ni nani? Basi Yesu akajibu, Ndiye mtu yule nitakayemtowelea tonge na kumpa. Akatowelea tonge, akalitwaa akampa Yuda, mwana wa Simoni Iskariote. YN. 13:22‭-‬26 SUV.

Kupitia andiko hili, tumeweza kufahamu kati ya washirika wengi kanisani, mshirika mmoja anaweza kuwa anapendwa zaidi ya wengine na mchungaji wake au mwalimu wake. Hii ipo kibiblia, hata kama mchungaji atasema anawapenda wote, yupo mtu ambaye watakuwa naye karibu zaidi ya wote, huyo ndiye ninayemzungumzia hapa siku ya leo.

Kupitia andiko hili, inatufundisha kuwa, mnaweza kuwa wanafunzi wengi darasani, ikatokea mwanafunzi mmoja anapendwa zaidi na mwalimu wake. Kuliko wanafunzi wengine darasani, lakini wote ni wanafunzi ambao wapo pamoja na mwalimu wao na anatamani wote wafikie kiwango kikubwa cha elimu.

Kupitia andiko hili, tunafahamu kuwa kuna mama/baba anaweza kuwa na watoto wengi aliowazaa mwenyewe, lakini akawa ana mtoto mmoja anayempenda zaidi, na mtoto huyo akawa karibu zaidi na baba/mama yake.

Kupitia andiko hili, tupata ufahamu kuwa mnaweza mkawa wafanyakazi wengi kwenye ofisi moja, akatokea mfanyakazi mmoja akawa anapendwa zaidi na boss. Huyu mmoja anayependwa akatumika kama daraja zuri la kufikisha changamoto za wafanyakazi wenzake, kama atakuwa na moyo mzuri.

Hivi ndivyo tunavyoweza kutumia nafasi za marafiki kufikisha ujumbe wetu kwa watu walio karibu nao, haya tunajifunza kupitia Neno la Mungu. Simoni Petro alitumia nafasi ya mwanafunzi mwenzake aliyekuwa anapendwa na Yesu Kristo, kumuuliza kile kilichokuwa kinamtatiza. Tunaona Simoni Petro alipata jibu la swali lake.

Maarifa kama haya yanapatikana kwenye Neno la Mungu, Neno la Mungu linakupa elimu hii nyeti usiyoweza kuipata sehemu nyingine kirahisi. Vyema kuwa na muda wa kusoma na kutafakari Neno la Mungu, na kama unapenda kuungana na wenzako wanaosoma Neno la Mungu. Karibu sana Chapeo Ya Wokovu whatsApp group, tuma ujumbe wako whatsApp +255759808081.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com