Miongoni mwa vitu vinavyoogopwa sana na mwanadamu ni pamoja na kifo, hakuna ambaye yupo tayari kufa kirahisi, kila mmoja anapambana kuhakikisha anaendelea kuwa hai. Hata ukimkuta mzee ambaye hajakata tamaa ya maisha, utamwona bado anatamani kuendelea kuishi.
Ukitaka kujua kila mmoja hapendi kifo, wewe angalia barabarani watu wanavyovuka, utaona kila mmoja lazima aangalie kushoto na kulia ndipo avuke barabara. Hata kama yupo kwenye taa za kuongozea magari.
Miongoni mwa watu hao barabarani ni pamoja na yule aliyetoka nyumbani asubuhi akatishia ndugu zake bora afe tu, maana yake haoni tena haja ya kuendelea kuishi Duniani. Pamoja na haoni haja ya kuendelea kuishi Duniani, utamkuta yupo makini barabarani.
Hata kichaa mwenyewe yupo makini barabarani, ni wachache sana utamwona amekaa barabarani, anajua kifo sio kizuri. Hii ni asili ya mwanadamu, hakuna mwanadamu anayekubali uhai wake upotee kirahisi, ndio maana utawakuta watu wamejazana hospitalini kutafuta matibabu.
Kila siku tunaona na kusikia misiba mbalimbali, hakuna aliyetokea akasema amezoea kufiwa, hata ikitokea yeye anataka kufa hataogopa chochote. Kuogopa lazima aogope, uhai wako una thamani kubwa sana.
Hakuna mahali wanatoa uhai wa mwanadamu, haijalishi una pesa nyingi sana, huwezi kusema utaununua mahali. Kwa hiyo uhai wa mwanadamu utabaki kuwa kitu cha pekee kinachopatikana kwa Mungu peke yake, akiamua muda wowote kutoa uhai wangu au wako anautoa.
Anapotokea mtu akakuambia nipo tayari kufa kwa ajili yako, mwambie moja kwa moja wewe ni muongo, ndio haijalishi anakupenda sana. Na Dunia nzima inajua ninyi mnapendana, ni ngumu kutoa uhai wake badala yako au badala ya mtu mwingine.
Utasema mbona kuna watu huwa wanajitoa mhanga, hebu fikiri kwa ufahamu wako wa kawaida kabisa hiyo ni roho ya kawaida? Hiyo ni roho nyingine inakuwa imemvaa mtu yule, hata watu wanaojinyoga, hakuna anayejinyoga akiwa na ufahamu wake timamu, katika ulimwengu wa kiroho anakuwa amevaa au amevalishwa roho nyingine kabisa chafu.
Wewe angalia hata tunapozika mtu makaburini, umewahi kuona kuna mtu anang’ang’ania azikwe na mpendwa wake? Watu watalia sana, watesema alikuwa mtu muhimu sana kwao, lakini hakuna anayejitokeza kusema kutokana na upendo wangu kwa huyu ndugu yangu, naomba nizikwe naye.
Aliyeweza kutoa uhai wake kwa ajili ya watu wengine ni mwanaume mmoja tu, ambaye ni Yesu Kristo, tena yeye mwenyewe alifika mahali akaanza kuomba Mungu kikombe kile kimwepuke.
Rejea: Mwenyewe akajitenga nao kama kiasi cha kutupa jiwe, akapiga magoti akaomba, akisema, Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke. [ Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu.LK. 22:41-43 SUV.
Kama Yesu Kristo aliombe kikombe cha mateso ya kutoa uhai wake kimwepuke, ikabidi malaika kutoka mbinguni aje kumtia nguvu. Je wewe itakuwaje? Unaweza kuona ni jinsi gani ilivyo sio hali ya kawaida mtu kuondolewa uhai wake.
Kwahiyo asije akatokea mtu akakudanganya yupo tayari kufa kwa ajili yako, hakuna na hatatokea, atatokea mtu kutoa mali zake kuhakikisha unapata matibabu mazuri ila ukimwambia huyo mtu afe badala yako au akatokea malaika akamwambia afe badala yako. Huyo mtu anaweza kusitisha na huduma yake ya kutoa gharama ya matibabu yako.
Hii kauli ya nipo tayari kufa kwa ajili yako, huwa inatumiwa sana kwenye mahusiano, hasa ya uchumba au urafiki, pale mahusiano yanapokuwa moto. Watu huwa wanaongea mengi sana, hasa dada akishasikia mwanaume anamwambia yupo tayari kufa kwa ajili yake, anakuwa kama amefunikwa macho na ka ujinga fulani huwa kanaingia ndani yake.
Mwanaume anaweza kumfanya chochote wakati huo, kwa sababu tu alihakikishiwa hataachwa, sio hilo tu, yule mwanaume alisema yupo tayari kutoa uhai wake kwa ajili yake. Ajabu mwanaume yule akishampa mimba anamkimbia na kumwachia mtoto akiwa tumboni.
Hili lilijidhihirisha kwa Petro, miongoni mwa wanafunzi waliokuwa mstari wa mbele kwa Yesu Kristo ni pamoja na Petro. Petro alikuwa hana mchezo alipoona kuna hali fulani juu ya Yesu Kristo, ndio maana kuna mahali alimkata mtu sikio.
Rejea: Basi Simoni Petro alikuwa na upanga, akaufuta, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio la kuume. Na yule mtumwa jina lake ni Malko. Yohana 18:10.
Unaweza kuona ni kiasi gani Petro alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha Yesu yupo salama, lakini alipomwambia Yesu Kristo yupo tayari kutoa uhai wake kwa ajili ya Yesu. Hilo Yesu Kristo alimkatalia na kumwambia kuna wakati atamkana.
Rejea: Simoni Petro akamwambia, Bwana, unakwendapi? Yesu akamjibu, Niendako huwezi kunifuata sasa; lakini utanifuata baadaye. Petro akamwambia, Bwana, kwa nini mimi nisiweze kukufuata sasa? Mimi nitautoa uhai wangu kwa ajili yako. Yesu akamjibu, Je! Wewe utautoa uhai wako kwa ajili yangu? Amin, amin, nakuambia, Jimbi hatawika hata wewe utakapokuwa umenikana mara tatu.YN. 13:36-38 SUV.
Kama wewe ni msomaji mzuri wa Neno la Mungu, utakuwa umeona Petro alifika mahali alimkana Yesu Kristo mara tatu kama alivyomwambia Yesu. Huyu mtu aliyekuwa tayari kutoa uhai wake kwa ajili ya mwingine, huyo huyo ndio aliyemkana mwenzake.
Petro alikuja kukumbuka aliambiwa na Yesu Kristo kitu kama hicho, tayari alishatimiza kauli/andiko aliloambiwa na Yesu Kristo. Kutokana na misukosuko aliyoiona kwa Yesu Kristo hakutaka kabisa kuunganishwa kwenye mateso ya namna hiyo.
Jifunze kumtegemea Mungu, watu wanaonyesha kukupenda sana ila utapofika mahali uhai wako upo hatarini, hao hao uliowategemea wanaweza kukusaidia, watakukimbia au watakukana. Bora anayemtegemea Yesu Kristo, anaweza kumwinulia watu asiowategemea kumwokoa katika shida yake.
Bora kumtegemea Mungu, hata unapopita kwenye jaribu gumu ambalo hata ndugu zako wamekukimbia, kama ni mapenzi ya Mungu uyapitie hayo. Mungu mwenyewe atakutia nguvu, na utapata nguvu mpya, utashangaa unapita kwenye jaribu zito ila una ujasiri wa hali ya juu.
Acha kudanganywa na wanadamu wenzako wapo tayari kufa kwa ajili yako, huo ni uongo, hao hao wanaokuambia hivyo wanaweza kutumika kuondoa uhai wako au wanaweza kukukimbia wakati wa shida yako.
Vizuri kusoma Neno la Mungu unapata ufahamu wa mambo mengi sana, hakikisha unajiwekea ratiba yako kila siku kwa ajili ya kusoma Neno la Mungu. Kama hili ni changamoto kwako, karibu Chapeo Ya Wokovu whatsApp group, nitakusimamia kuhakikisha unafikia malengo yako, tuma sms yako whatsApp +255759808081.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com