Miongoni mwa jambo linalowapa tabu watu wengi ni pamoja na pale wanapookoka tu, watu huanza kuwachukia sana, chuki ya watu wale ni kwa sababu huyu ndugu haendi tena kama wao wanavyoenda.
Unapoamua kumpa Yesu Kristo maisha yako, sikufichi rafiki, nitakuambia ukweli, ili utakapoanza kuona unakosa marafiki na utakapoona unakuwa na maadui wengi. Usije ukafikiri ulikosea njia, kumpokea kwako Yesu Kristo, ni sawa na mtu aliyesimama jukwani au kwenye vyombo vya habari kutangaza watu wote wamchukie.
Kuokoka kuna raha yake kubwa sana ila ulimwengu huu utakupa karaha nyingi sana, wakati mwingine usipokuwa makini unaweza kutamani kurudi tena kwenye maisha ya dhambi. Kosa kubwa sana ulilotenda kwao ni kuamua kuacha dhambi na kumfuata Yesu Kristo.
Unapoamua kumpa Yesu Kristo maisha yako, na ukaamua kusimama katika kweli ya Neno lake, wewe tayari unakuwa sio mtu wa ulimwengu, yaani sio mtu wa kukimbilia mambo mabaya. Kabla hujaokoka ulikuwa mlevi, mzinzi, mwizi, mchawi, na mambo mengine machafu, lakini ulivyoamua kuachana na mambo hayo. Lazima uwe adui wa shetani, maana umeshatoka kwake.
Shetani hupanda chuki kwa watu wake, wale waliomwacha waanze kuona wokovu hufai, waanze kuona wokovu mgumu, maana walikuwa na marafiki wengi. Marafiki hao wanawatenga na yeye anajitenga nao kwa mabaya, lazima waanze kumtupia maneno magumu.
Watu kukuchukia wewe ni jambo ambalo lipo kibiblia, chuki yao ni kwa sababu wewe si wa ulimwengu huu, mwenendo wako na matendo yako ni tofauti kabisa na mtu ambaye hajampokea Yesu Kristo kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yake.
Usishangae unakuwa adui wa wazazi wako, sio kwamba umebadilika sura, ujue katika ulimwengu wa kiroho, wewe sio ndugu yao, wewe ni mwana wa nuru na wao ni wana wa giza. Kuna tofauti kubwa sana kati yenu, kuna uhusiano fulani mkubwa haupo kati yenu.
Wanapojaribu kuleta chuki kwako ni kukutaka urudi kwenye maisha ya kale, urudi kwenye maisha ya kuabudu sanamu, urudi kwenye maisha ya kuabudu miungu ya mababu, urudi kwenye maisha ya kumtumikia Shetani. Hiyo vita lazima iwe kubwa na unapaswa kujua hiyo vita si vyako ni vya Bwana.
Neno la Mungu lipo wazi kabisa kwenye hili ninalokueleza hapa, huenda umeshindwa kuelewa Kwanini chuki kubwa imeinuka baada ya kuamua kuokoka. Huenda unashindwa kung’amua hadi leo, wakati unafanya mambo yasiyofaa ulitakiwa uchukiwe kwa hilo, ila leo umeamua kuyaacha, badala ya watu kukufurahia wanakuchukia.
Chuki yao kubwa ni kwa sababu wewe si mwana wa ulimwengu huu tena, wewe ni mtoto wa Mungu, Shetani hana nafasi tena ya kukutumikisha kwa jambo lolote. Ndio maana anapanda chuki kubwa kwa watu wake, yaani wale ambao bado wanafanya dhambi za kumchukiza Mungu.
Rejea: Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia. YN. 15:19 SUV.
Haleluya, wewe sio wa kawaida, Yesu Kristo alikuchagua kati ya wengi, ukaisikia sauti yake ukaitika, ukamua kuvua viatu vya uzinzi, ulevi, uasherati, ukahaba, uchawi, kuabudu sanamu, na mengine mengi machafu. Ukaamua kumtumikia Mungu wako kwa kile alichoweka ndani yako, uwe na uhakika ulimwengu huu hautakupenda kamwe.
Tena unapaswa kujua anayekuchukia wewe, anamchukia aliyekuchagua ambaye ni Yesu Kristo, na mtu anayemchukia Yesu Kristo, anamchukia Mungu mwenyewe. Ndio, usikatae na usione nimekosea, narudia tena, mtu yeyote anayemchukia Yesu Kristo, huyo anamchukia Mungu mwenyewe.
Rejea: Yeye anichukiaye mimi humchukia na Baba yangu.YN. 15:23 SUV.
Unaona hilo andiko, sio mimi nasema, ni Yesu mwenyewe anasema wazi, kama unaona mtu anakuchukia kwa sababu ya kuokoka kwako, kwa sababu ya huduma yako ya kumhubiri Yesu Kristo katika kweli, kwa sababu ya kufundisha kwako Neno la Mungu lisiloghushiwa. Ujue huyo si wa Mungu, aliye wa Mungu hawezi kuwa hivyo.
Usiogope mtu, wala usifike mahali ukaona ulikosea njia, ulikosea kuokoka, njia uliopo ni sahihi kabisa isipokuwa ina vita vikali sana. Usihangaike na vita visivyo vyako, yeye anayekuchukia wewe mwana wa Mungu, anamchukia Yesu mwenyewe.
Rejea: Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi. YN. 15:18 SUV.
Ndugu mpendwa katika Kristo, simama kishujaa, usitetereke kwa jambo lolote, acha watu wakuchukie wanavyojua wao, acha wakutengenezee mambo mabaya ya kutunga wao. Siku zote jua wewe si wa ulimwengu huu, wewe ni ulimwengu mwingine kabisa.
Tena wewe umewazidi hatua nyingi sana mbele, na wakitaka kushindana na wewe, hawatashindana na wewe kama wewe, watashindana na yule aliye ndani yako. Ambaye ni Yesu Kristo, watashangaa wakipata madhara wao na si wewe.
La muhimu zaidi, utapata marafiki zako ndani ya wokovu, hata kama ni wachache sana, hao ni muhimu sana, maana ni marafiki mlio njia moja, ni marafiki wanaoweza kukubeba kwa maombi, ni marafiki wanaoweza kukusaidia mambo mengi yasiyoweza kuonekana kwa macho ya nyama.
Muhimu kuliko yote ni kuhakikisha hupungukiwi na Neno la Mungu, siku yako isipite bila kusoma Neno la Mungu, moyo wako ufurike Neno la Kristo ndani yako. Hiyo ndio silaha yako muhimu sana ya kumshinda shetani, mitengo yote ya Shetani utaweza kuibaini na kuweza kuikwepa ukiwa na Neno la Mungu.
Kama kusoma Neno la Mungu ni changamoto kwako, na utamani sana kujenga tabia mpya ambayo haitaondoka kwako. Kwanza amua kweli kutoka moyoni mwako, pili chukua hatua ya kuanza sasa kusoma Neno la Mungu, na tatu ambatana na watu wanaopenda kusoma Neno la Mungu. Kama unaona ni ngumu kuwapata, karibu Chapeo Ya Wokovu whatsApp group utakutana na watu wanaojibidiisha kusoma Neno, wasiliana nasi whatsApp +255759808081.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com