Ukilichukia Neno la Mungu utakuwa na agenda yako binafsi, lakini Neno la Mungu limenena kila kitu katika maisha ya mwanadamu. Kila kinachotokea sasa kwenye maisha ya mwanadamu tayari lilishatabiriwa siku nyingi.

Kanuni ya unabii ulionenwa utatokea, sharti utokee ili unabii ule utimie, ndivyo ilivyo hadi leo tunaona yale tunayojifunza ndani ya Neno la Mungu. Mengi yametokea, na yapo yanazidi kutokea kadri siku zinavyozidi kwenda mbele.

Huenda nyakati za mababu zetu waliona kila kitu kimetimia kwa nyakati zao walizoishi, ila wangepata bahati ya kurudi tena Duniani, naona wangeshangaa zaidi vile mambo mengi yamebadilika na mengi zaidi yametokea ya kumchukiza Mungu kuliko nyakati zao za uhai.

Kadri ninavyozidi kulisoma Neno la Mungu, kuna vitu nazidi kushangaa tu, unajua ni rahisi kusema kila kitu kipo ndani ya Biblia takatifu ila usiwe na ushahidi wa maandiko matakatifu. Unaweza kusema hivyo kutokana na kusikia watu mbalimbali kusema hivyo, ila unaposoma mwenyewe Neno la Mungu unajifunza zaidi.

Kuna wakati nilikuwa najiuliza watu wanaoua wakristo, wanajitoa mhanga kabisa kuangamiza wakristo, kuangamiza watumishi wa Mungu, kuchoma makanisa moto, kuhakikisha ukristo unafutika kabisa. Nikawa nafikiri ni hali tu ya chuki kwa watu wale, kumbe kitendo hichi wao wanafikiri wanamtolea Mungu ibada.

Mtu anapoua mkristo kwake sio huzuni, wala kwake sio jambo baya, bali ni jambo linaloleta amani ndani ya moyo wake, kwa sababu anafikiri anamtolea Mungu wake ibada njema. Nyie mnalia kwa kumpoteza ndugu yenu, mpendwa wenu, yeye anafurahia anamemfanyia Mungu wake ibada.

Jambo la kushangaza mno, na linaweza kukuchukua muda kuamini hili ila itakulazimu uniamini maana nitakupa andiko linalothibitisha hili ninalokuambia hapa. Shetani hafai, ameingiza upotofu kwa watu wengi wanaomkataa Yesu Kristo, wanaona kuua mkristo ni ibada kwao.

Hebu jaribu kuwaza, kama mtu anajua kuua mkristo mmoja atakuwa amemtolea Mungu ibada, unafikiri kila mtu aliyepandiwa elimu hii au roho hii. Ataweza kutulia bila kuua mkristo? La hasha, lazima atafute kila namna kuhakikisha ameondoa uhai wa mkristo. Maana kufanya hivyo ni ibada kwake, sio mimi nisemayo haya, ni maandiko matakatifu yanasema.

Rejea: Watawatenga na masinagogi; naam, saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada. Na hayo watawatenda kwa sababu hawakumjua Baba wala mimi. Lakini nimewaambia hayo, ili makusudi saa ile itakapokuja myakumbuke ya kuwa mimi naliwaambia. Sikuwaambia hayo tangu mwanzo, kwa sababu nalikuwapo pamoja nanyi.YN. 16:2‭-‬4 SUV.

Yesu Kristo alimaliza kazi kabisa, hapo alikuwa anawaambia wanafunzi wake kabla ya kupaa kwenda mbinguni, aliwaeleza ukweli. Ambapo leo wanafunzi wa Yesu Kristo ni wale waliaminilo jina lake kwa kuamua kuacha mambo mabaya ya Dunia hii.

Vita bado vipo pale pale, ukiwa kama mkristo ambaye umesimama vizuri, huna kona kona, wewe ni adui mkubwa sana kwa watu wa dini. Ambao hawataki kusikia habari za kuokoka ukiwa Duniani, na ambao hawataki kabisa kusikia habari za Yesu Kristo.

Utakaposimama kuhubiri kweli ya Mungu, usifikiri utapendwa na wale wanaoenda kinyume na maagizo ya Mungu. Utaingia kwenye kuchukiwa na ukikaa vibaya unaondolewa uhai wako, sio nakutisha, nakueleza ukweli wa Neno la Mungu.

Wanaweza wasikue mwili wako, ukashangaa wakadili na roho yako, ulikuwa vizuri kiroho, uhusiano wako na Mungu ulikuwa umesimama vizuri kabisa. Ghafla ukaporomoka chini, shida nini? Shida umedanganywa ukamtenda Mungu dhambi, kusimama tena inakuwa tabu kwako.

Vizuri kujua kwamba wapo watu kazi yao ni kuua watu, kuua kwao waliosimama na Yesu Kristo, kwao ni wanaona wanamtolea Mungu ibada. Kukutoa uhai wako kwao sio jambo baya, wala sio jambo la kushangaza bali ni sehemu ya kumtolea Mungu ibada.

Utasema ni Mungu gani huyo wa kupendezwa na ujinga wa namna hiyo, wao ndio wanajua hivyo, na wanaamini siku ya mwisho wataingia peponi. Kwako unayeijua kweli ya Kristo, unaweza kuwashangaa mno ila ukweli ndio huo.

Rejea: Watawatenga na masinagogi; naam, saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada.YN. 16:2 SUV.

Yamkini umetengwa na familia yako baada ya kuamua kuokoka, usirudi nyuma, endelea kusonga mbele, ilisha tabiriwa zamani. Kurudi nyuma kwa sababu ya kutengwa, au kwa sababu ya kutishiwa uhai wako, hicho sio kisingizio cha kukwepa hukumu ya Mungu siku ya mwisho.

Mungu akusaidie wewe uliyeamua kumfuata Yesu Kristo katika roho na kweli, usije ukaogopa wanaoua mwili, bali ogopa anayeua mwili na roho. Simama imara katika ukristo wako, simama imara katika huduma yako, chapa injili kisawasawa.

Unapenda kujifunza Neno la Mungu na umejaribu mara nyingi kujenga tabia hii nzuri, lakini umefeli mara nyingi? Karibu sana Chapeo Ya Wokovu whatsApp group, humo utakutana na watu wanaopenda na kujibidiisha kusoma Neno la Mungu. Wasiliana nasi kwa whatsApp +255759808081 uunganishwe.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com