Ili uonekane mbaya kwa watu sio lazima ufanye kitu ambacho kinamchukiza Mungu wako, kusimama tu katika kweli, inaweza kukuletea shida kubwa ambayo hujawahi kuifikiri kama inaweza kukuletea tabu zote hizo utakazokutana nazo.
Mtu akishakuona mbaya wake, hakuna jambo zuri utafanya likampendeza, siku zote utaonekana wewe ni mbaya. Na wakati mwingine unaweza kuingia kwenye vita mbaya sana, hata wale wasiojua nini kinaendelea kati yenu wanaweza kuona kitu kisicho cha kawaida kwenu.
Unapoonekana mbaya, hata ukiongea neno zuri kwa nia njema, utaonekana kwao umeongea neno baya la kuwatukana. Kila neno utakaloongea kwao, utaonekana una dharau au utaonekana umewatukana au utaonekana upo kinyume nao.
Unaweza kushangaa maneno yanayosambazwa kwa watu kuwa wewe unatukana watu, au wewe una dharau sana kwa watu au wewe kila kitu unapinga. Alafu watu wengine wasio na ubaya wowote na wewe, wanaweza kujiuliza kwanini unazushiwa maneno kama hayo. Maana wanaona hakuna jambo baya unalofanya/ulilofanya.
Pia wapo watu wengine wanaweza kukuchukia kutokana na habari zako walizokutana nazo kwa watu mbalimbali wakisema wewe ni mbaya sana. Watu wale pasipo kuchunguza ubaya wako upo wapi, wanajenga tu chuki kwako, na kuwa kitu kimoja na wale wabaya wako.
Wanakuwa kitu kimoja kwa sababu watu wale ambao wanakuona ni mbaya kwao, wana uhusiano wa karibu na wale watu au ni watu wanaoaminika na jamii kutokana na nafasi zao.
Unapaswa kuelewa hili, pale maadui zako wanapokuandama, uwe unajua hakuna jambo zuri litasemwa juu yako. Tena ukiingia kwenye mtego wao, utakutana na mauzi mengi sana, sio mauzi tu ya maneno, unaweza kupigwa kabisa.
Haijalishi upo kwenye haki, haijalishi hufanyi mambo mabaya mbele za Mungu, kama upo kinyume na wakuu wa nchi, kama upo kinyume na wakuu wa dini, uwe na uhakika utakuwa kwenye vita ngumu sana, alafu ukute wale ambao wanaokuona wewe ni mbaya wawe na nafasi fulani au mamlaka fulani.
Nakuambia utapata tabu sana, utawekewa vikwazo vya kila namna, utazushiwa maneno magumu yenye kukujengea picha mbaya kwa wale wanaokuamini. Haitaishia hapo, unaweza kuendelea kukutana na misukosuko ya aina mbalimbali.
Haya tunajifunza kwa Yesu Kristo, Yesu Kristo katika huduma yake hakuna jambo baya alilolifanya, walikuwa wanamchukia tu kwa sababu ya kazi zake alizokuwa anazifanya. Kitu kingine kilichokuwa kinawasumbua ni pale alipoitwa mfalme wa ulimwengu huu, na pale watu walipomwamini yeye.
Wakati wamemshika Yesu wamsulubishe, swali walilomuuliza alipotoa majibu yake, hawakufurahishwa na majibu yake hadi mtumishi mmoja alimpiga Yesu kofi.
Rejea: Ya nini kuniuliza mimi? Waulize wale waliosikia ni nini niliyowaambia; wao wanajua niliyoyanena. Basi aliposema hayo, mtumishi mmojawapo aliyesimama karibu alimpiga Yesu kofi akisema, Wamjibu hivi Kuhani Mkuu? Yesu akamjibu, Kama nimesema vibaya, ushuhudie ule ubaya; bali kama nimesema vema, wanipigia nini?YN. 18:21-23 SUV.
Kama Yesu Kristo alifanyiwa hivi, unafikiri watapokukamata wale wabaya wako, au watapokujia na maneno, alafu ukainua mdomo wako kuwajibu. Unafikiri watakuacha hivi hivi? Hapana, lazima ukutane na maumivu ya kipigo au adhabu yeyote ile ya kukukomoa.
Unachotakiwa kufahamu ni kwamba, hakuna jibu zuri utatoa kwa mbaya wako, alafu jibu hilo likaonekana ni zuri kwake, maana hutojibu kinafiki, utajibu vile wamekuuliza. Ukiwapa ukweli wabaya wako, usifikiri watakubali uwe mshindi alafu wao washindwe, ilimradi upo mikononi mwao, lazima ukutane na tabu.
Simama imara hata utakapokutana na hali kama hizi ngumu katika maisha yako ya kihuduma au maisha yako ya wokovu, unaweza kufikiri labda umekosea kutoa majibu mazuri au umeongea maneno mabaya katika mafundisho yako. Na unaweza kuuliza ubaya wako upo wapi, usishangae utakapokosa majibu ya maswali yako.
Ukuaji wako wa kiroho ni muhimu sana katika maisha yako ya wokovu, na ukuaji huo unaletwa na kusoma Neno la Mungu kila siku. Kama unahitaji kujenga tabia mpya ya kusoma Neno kila siku, na unaona jambo hili ni changamoto kwako. Karibu Chapeo Ya Wokovu whatsApp group, utasimamiwa kuhakikisha unajenga tabia ya kusoma Neno, wasiliana nasi +255759808081.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest
www.chapeotz.com