
Yapo mambo madogo sana tunayoyapata katika maisha yetu, wakati mwingine yanatunyima usingizi sio kwa sababu hayana majibu yake. Kukosa kwetu maarifa au kutokuelewa kwetu maandiko matakatifu yanasemaje, tumebaki tunahangaika na mambo ambayo tayari yana majibu yake.
Tuchukulie unaumwa sana, kama hutochukua hatua ya kwenda hospital, ugonjwa ule unaweza kuendelea kukutesa kwa kufikiri ni tatizo kubwa sana. Kumbe ungeenda kupima, ungepatiwa vipimo na kuelezwa dawa unayotakiwa kutumia, sasa kwa kutoelewa kwako hilo, unaendelea kuumwa huku ukijaribu dawa za kienyeji bila kujua tatizo unaloumwa.
Yapo mambo mengi sana yamekuwa mzigo kwetu kutokana na kukosa maarifa sahihi, kweli kabisa unakuta mtu anateswa na msongo wa mawazo kwa jambo fulani. Akifikiri hilo jambo halina majibu yake na kuona hilo jambo limemkalia vibaya kwa kukosa majibu, kumbe hilo jambo lina majibu yake.
Sawa na mtu ambaye hajui kabisa matumizi ya simu, nikiwa na maana hajui mahali pa kuwashiwa simu, wala hajui mahali pa kupiga, wala hajui mahali pa kutuma sms. Anachojua yeye ni kifaa kile kinaitwa simu, wala hujui kama kuna kuishiwa moto, siku ikizima kwa kuishiwa moto anaweza kufikiri simu mbovu.
Nenda kwa mafundi simu watakwambia kabisa kuna simu zingine huwa wanaletewa ni nzima kabisa, sema mwenye simu anakuja pale anadai simu yake ni mbovu. Kumbe simu sio mbovu ni nzima kabisa, shida yake ni kutokujua vizuri matumizi ya simu yake.
Hata wewe utakuwa shahidi wa hili, kuna wakati ulifikiri jambo lako fulani haliwezekani, kumbe jambo linawezekana kabisa. Ukikuta mtu mwaminifu na anayeelewa hilo jambo, atakwambia hili jambo lako lipo hivi na vile, utaona kumbe ilikuwa ni rahisi tu shida ni kutokuelewa kwako.
Kwahiyo kutokuelewa kwako kunaweza kukupa shida kubwa sana, unaweza kufikiri shida iliyokupata ni kubwa sana haiwezekani kuisha haraka. Kumbe sivyo ilivyo, shida iliyokupata ina majibu yake, inawezekana kabisa una kitabu cha maelekezo ndani kwako ila kwa sababu husomi unaona haiwezekani.
Ni sawa na simu, unapoenda dukani kununua unapewa na kitabu cha maelekezo namna ya kuitumia hiyo simu, lakini wengi huwa hatuna muda wa kukikosoma hicho kitabu cha maelekezo. Inapotokea jambo dogo tu, huwa tunakosa mbinu kutokana na ufinyu wa maarifa sahihi.
Ndivyo ilivyo kwa wakristo wengi, mambo mengi sana tunapata nayo shida kutokana na kutofahamu/kutokuelewa maandiko matakatifu yanasemaje. Tunaweza kuteswa na tatizo dogo sana ambalo tungejua maandiko matakatifu yanasemaje kuhusu hilo jambo, tungejua cha kufanya.
Kutokujua kwetu maandiko matakatifu kumetufanya tuteseke na mambo mengi yanayotupata kwenye maisha yetu, na hili limekabili watu wengi sana. Haijilishi umeokoka miaka kumi iliyopita, kama huna maandiko matakatifu ya kutosha moyoni mwako, miaka yako mingi haiwezi kukusaidia kitu.
Hili tunaliona kwa Mariam Magdalene alivyoenda kaburini kumwona Yesu siku ya tatu, hakukuta mtu, alikutana na sanda, kitendo kile kilimshtua na kukimbilia kuwapa taarifa wanafunzi wa Yesu. Ambao walikuwa ni Simon Petro na yule mwanafunzi aliyempenda Yesu ambaye alikuwa ni Yohana.
Na wao walivyopewa taarifa walikimbia mbio kwenda kaburini, kile kile walichoambiwa na Mariam Magdalene ndicho walichokutana nacho kaburini. Hawakujua kabisa siku ya tatu ilikuwa ni ya kufufuka kwa Yesu Kristo.
Maandiko matakatifu yanatuambia kabisa hawa watu hawakulifahamu andiko, ya kwamba Yesu Kristo alipaswa kufufuka siku ya tatu katika wafu.
Rejea: Kwa maana hawajalifahamu bado andiko, ya kwamba imempasa kufufuka.YN. 20:9 SUV.
Hebu fikiri mwenyewe, ni mambo mangapi umekosa haki zako za msingi kabisa kwa kutokufahamu kwako maandiko matakatifu. Hebu jiambie ukweli bila kujipendelea au bila kujionea aibu au kwa kutojihurumia, baada ya kujipa hayo majibu utaona ni jinsi gani mambo mengi umehangaika nayo sana na kukosa haki zako.
Huenda yapo mengine mengi unaendelea kuhangaikia nayo kwa sababu hujui ufanyaje, kumbe kitabu cha maelekezo unacho, huna muda wa kukikosoma. Na huenda hujui kilichoandikwa ndani ila unaona kitabu tu, na wengine tulivyosikia kitabu fulani ni kizuri tulienda kukinunua, ila tangu tukinunue hatujawi kukikosoma.
Hebu acha kuweka Biblia yako ndani kama urembo wa nyumba yako, acha kuifanya Biblia yako kama nguo maalum ya kuendea kanisani au kwenye shughuli maalum. Tenga muda wako kila siku wa kusoma Neno la Mungu, utajua mengi sana.
Kuna dhambi imekung’ang’ania kwa sababu ya kukosa Neno la Mungu, umeomba sana lakini bado unaona hali ipo vile vile, unahitaji Neno la Mungu. Unahitaji maarifa sahihi ya Neno la Mungu, mambo mengine hayahitaji maombi, yanahitaji maarifa sahihi ya kukutoa hapo ulipo.
Hakikisha unaanza sasa kujiwekea ratiba yako ya kusoma Neno la Mungu, unaona hilo ni shida kwako, tupo tayari kukusaidia hatua kwa hatua. Tutahakikisha tunakusimamia kama utakubali kusimamiwa, cha msingi ni kujiunga na program yetu ya kusoma Neno kwa njia ya whatsApp group. Wasiliana nasi kwa whatsApp +255759808081 utaunganishwa.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com