
Tabia ya kushirikiana pamoja kwa watu wanapookoka na kuwa kitu kimoja, ni tabia ambayo haijaanza leo, ilianzia kwa kanisa la kwanza, yaani kwa wale watu waliompokea Yesu Kristo. Waliuza mali zao na kuwasaidia wale wahitaji wakiwa kama kitu kimoja.
Unapoona kanisa/dhehebu/kikundi fulani wanajitoa kwa moyo wote kwa ajili ya kumsaidia mwenzao kwa jambo fulani, hasa la kifedha, ujue watu wale wanafanya jambo la kiMungu.
Tena kundi la namna hii linalosaidiana kama washirika, huvuta watu wengi sana kuja kwa Yesu Kristo, wanapoona mwenzao akifiwa wanaenda kumtembelea, na akipatwa na shida wanaenda kumtia moyo.
Kundi hili huwafurahisha wale ambao bado hawajapata neema ya kuokoka, ule upendo wa shirika kwa kundi lililomwamini Yesu Kristo. Huwavuta wale wenye mioyo migumu ya kuokoka.
Usione ajabu kanisa/dhehebu fulani linazidi kuwa na watu wengi, usifikiri ni kwa sababu ya kuhubiri sana kwa masipika makubwa. Wakati mwingine sio hivyo, washirika kuongezeka wanavutwa na vitu vingi, ambapo ni pamoja na ule ushirika wa watu waliokoka.
Tena makanisa mengine kabla ya kutawanyika kwenda nyumbani, hupata chakula cha mchana pamoja, hichi ni kitendo cha maana sana kwa waamini. Sio tu kitendo cha mwili, ni kitendo ambacho kinawafanya muendelee kuwa kitu kimoja.
Kitendo cha kuchangishana michango kwenda kumwona mshirika mwenzenu, sio kupoteza muda wako, wala sio kupoteza pesa zako, ni kitendo ambacho kinamfanya yule aliyepata shida aendelee kuona ana ndugu wanaolia naye na wanaocheka naye.
Kudumu katika mafundisho ya Neno la Mungu ni jambo ambalo linapaswa kupewa uzito mkubwa sana kwa kila mwamini yeyote yule, katika Kudumu huko katika mafundisho. Mnapaswa kushirikiana kwa pamoja kwa mambo muhimu wanayopata washirika/waamini wengine.
Jumuiya ya watu waliokoka inayoshirikiana pamoja kwa kila jambo la mwamini, jumuiya hiyo lazima idumu, na jumuiya hiyo lazima iwe na matunda mazuri ya kuwavuta watu wengine kwa Yesu Kristo. Maana haishii kufundishana maneno ya Mungu, pale mwenzao anapopatwa na shida, wanakuwa pamoja naye katika shida yake.
Jambo la kuzingatia katika jumuiya hii ya waamini, kila mmoja hapaswi kuwa mnyimi/mtegevu, kila mmoja anapaswa kuwa mtoaji kwa kile anacho kumsaidia mwenye uhitaji. Asiwepo mtu anayetaka kufanyiwa mambo mazuri, alafu yeye kwa wenzake hataki kujitoa, wala hataki kutoa muda wake.
Tukiwa kama waamini wenye safari ya kwenda mbinguni, wenye kufundishana maneno ya Mungu katika vipindi vyetu makanisani na makusanyiko mbalimbali. Lazima tujue hili la kusaidiana kama jumuiya kutokana na taratibu mlizowekeana, hili tendo linaimarisha umoja wenu na linawavuta watu wengi kwa Yesu Kristo.
Hili tunajifunza kupitia Neno la Mungu, usifikiri ni ushauri tu wa kawaida, hili jambo lipo kiMungu na ukilizingatia utaona matunda yake makubwa sana. Ukiacha kufikiri unapoteza pesa zako bure, ukawa mstari wa mbele kushirikiana na washirika wenzako, hutaona ukipungukiwa katika maisha yako.
Rejea: Na wote walioamini walikuwa mahali pamoja, na kuwa na vitu vyote shirika, wakiuza mali zao, na vitu vyao walivyokuwa navyo, na kuwagawia watu wote kama kila mtu alivyokuwa na haja. MDO 2:44-45 SUV.
Haleluya, pamoja na matendo makuu ya Mungu yaliyokuwa yanaendelea kwa waamini hawa wapya na wa zamani, waliuza mali zao, na vitu walivyokuwa navyo, kuwagawia wale wahitaji.
Hebu fikiri mwenyewe hili jambo ulikuwa unalionaje kabla hujakutana na hili andiko au somo? Baada ya kujipa zoezi la kutulia na kutafakari hili, utajipa majibu sahihi mwenyewe, usijipendelee wala usijionee huruma, jipe jibu sahihi hata kama linauma.
Unaweza usiwe na fedha nyingi sana, kile kidogo ulichonacho kinaweza kikawa baraka kwa mwenzako mwenye uhitaji, na unaweza siku nyingine usiwe kabisa na fedha. Lakini ukawa na kitu chako ulichokuwa unatumia ukachukua sehemu ndogo ukampa mwenzako, na unaweza usiwe kabisa na hivyo vyote, tumia muda wako kuwa faraja kwa mwenzako.
Usiache kushirikiana na wenzako wanaompenda Yesu Kristo, shiriki ibada za pamoja, shiriki matukio mbalimbali ya pamoja, ambayo unaweza kushiriki kwa fedha zako, au unaweza kushiriki kwa vitu vyako, au unaweza kushiriki kwa muda wako. Au vyote kwa pamoja, yaani fedha, vitu, na muda, kutokana na nafasi yako.
Ushirika kama huu unapatikana pia Chapeo Ya Wokovu whatsApp group, licha ya kusoma Neno la Mungu kila siku, tunashirikiana kwa pamoja pale mwenzetu anapokuwa mhitaji wa jambo, liwe la furaha au la huzuni, tunakuwa naye pamoja. Karibu sana kwenye ushirika huu wa kujifunza Neno la Mungu na kushirikiana mambo mengine, wasiliana nasi kwa wasap namba +255759808081 utaunganishwa kwenye group letu.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com