Kuna watu wanainuka na kujiita manabii, wengine mitume, wengine wadiriki kusema wametumwa na Mungu katika utumishi wao. Lakini pamoja na kusema wametumwa na Mungu, wengine sio kweli wametumwa na Mungu.

Wengine wanakuwa wamejiita wenyewe nabii na mtume, ila ndani yao Mungu hajaweka huduma hiyo ya unabii, wala ndani yao hakuna wito wa kiMungu. Mbaya zaidi bado hawajazaliwa mara ya pili, ila wanasema wametumwa na Mungu.

Hilo sio shida, kama wametumwa na Mungu kweli, itajulikana, na kama huduma zao zimetokana na tamaa zao za kibinadamu itajulikana. Kitu cha kibinadamu kitajulikana tu, na kitu cha kiMungu kitajulikana tu.

Mtu yeyote anayeinuka kwenye utumishi, kudumu kwake kwenye utumishi kutategemeana na huduma yake imetoka kwa nani, ikiwa imetoka kwa binadamu itavunjwa. Na ikiwa imetoka kwa Mungu haitaweza kuvunjwa, zaidi itaendelea kudumu na kuendelea mbele, na itaendelea kukua zaidi.

Haijalishi mtu fulani ameibuka na kujiita nabii aliyetumwa na Mungu, kama sio nabii wa Mungu, mpe muda, hiyo huduma yake itasambaratika kwa sababu ndogo tu. Hata kama atawakusanya maelfu ya watu wengi, na kuwalaghai kuwa yeye anaitenda kazi ya Mungu, hiyo sio sababu.

Kazi zote zinatoka kwa Mungu hakuna mtu yeyote ataweza kuivunja hiyo kazi, haijalishi serikali itasimama kinyume kusambaratisha hiyo kazi, haijalishi wazee gani watakaa vikao vyao kutaka kuhakikisha mtu fulani haendelei kufanya kazi ya Mungu. Mipango hiyo yote haitafanikiwa kamwe kuivunja hiyo kazi, hata kama itapita kwenye misukosuko mingi sana itaendelea kusimama.

Kama kazi inatokana na mwanadamu, hiyo kazi ikipita kwenye msukosuko mmoja tu itasambaratika yenyewe, haitasimama tena. Maana ilikuwa imetoka kwa binadamu, yaani yule aliyekuwa anajiita mtume au nabii, alikuwa amejiita mwenyewe sio kana kwamba ni huduma aliyopewa na Mungu.

Kazi ya Mungu huwezi kuivunja, ila kazi ikiwa imetoka kwa binadamu utaivunja, hili tunapaswa kulifahamu watu wa Mungu. Kama una huduma ndani yako, unasikia moto wa Roho Mtakatifu unawaka ndani yako, alafu unaona kuna vita vikali sana mbele yako. Usiwe na mashaka, hakuna ataweza kuuzima huo moto, labda wewe uamue uzimike kwa kuruhusu vitu vichafu.

Huduma yako itaendelea kusimama imara, hata kama itapita kwenye misukosuko mingi, maana inatoka kwa Mungu. Ila kama haitoki kwa Mungu, hesabu huna chako, hiyo kazi unayoifanya utafika mahali itavunjwa na sababu moja tu.

Sikuelezi habari za hewani, nakueleza jambo ambalo lipo kimaandiko kabisa, kazi yeyote inayotoka kwa Mungu hakuna mtu yeyote ataweza kuivunja. Ila ile kazi inayotoka kwa binadamu itavunjwa, tena na wanadamu wale wale.

Rejea: Basi sasa nawaambia, Jiepusheni na watu hawa, waacheni; kwa kuwa shauri hili au kazi hii ikiwa imetoka kwa binadamu, itavunjwa, lakini ikiwa imetoka kwa Mungu hamwezi kuivunja; msije mkaonekana kuwa mnapigana na Mungu. MDO 5:38‭-‬39 SUV.

Umeona hapo, nataka utazame kazi inayotoka kwa Mungu na kazi inayotoka kwa binadamu, umeona hapo inasema kazi inayotoka kwa Mungu huwezi kuivunja, ila kazi inayotoka kwa binadamu itavunjwa. Kwahiyo ukiona kuna huduma ilikuja kwa kasi kubwa alafu ghafla ikapotea, chunguza vizuri, utakuta haikuwa kazi ya Mungu.

Kazi ya Mungu hata kama mtu aliyekuwa amesimama kwa ajili ya hiyo kazi, mtu huyo atamwasi Mungu, hiyo kazi haiwezi kupotea, Mungu atamwinua mtu mwingine kwa kazi ile ile. Utashangaa badala ya kufa, inaendelea kusonga mbele zaidi.

Pando lolote asilolipanda Mungu, haijalishi linaonekana ni zuri sana na linatastawi sana, uwe na uhakika pando hilo litang’olewa kwa namna yeyote ile.

Rejea: Akajibu, akasema, Kila pando asilolipanda Baba yangu wa mbinguni litang’olewa. MT. 15:13 SUV.

Usijidanganye unaweza kuua huduma ya mtumishi wa Mungu fulani, wala usidanganywe ukristo utakufa, wala usidanganywe watumishi wa kweli wataisha, hata kama ije dhoruba gani. Kazi ya Mungu itaendelea kusimama, na injili itaendelea kuhubiriwa kila kona, kwa hiyo usiogope kuitenda kazi ya Mungu.

Mwisho, nikualike kwenye group letu la kusoma Neno la Mungu kila siku, karibu kwenye kundi hili ili uweze kujenga tabia mpya ya kusoma Neno la Mungu. Ili uunganishwe kwenye program hii, tuma ujumbe wako kwa whatsApp namba +255759808081.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com