Mwaka unaokuja 2019, maeneo mengi au sehemu nyingi watakuwa na uchaguzi wa viongozi mbalimbali wa idara, idara ya watoto na vijana watakuwa na uchaguzi wa viongozi wapya. Idara ya wanawake itakuwa na uchaguzi, idara ya sifa na mziki itakuwa na uchaguzi wa viongozi wake.

Yanafuata maeneo mengine kwa wachungaji na maaskofu, kuna uchaguzi wa viongozi wa parishi, misheni, jimbo na taifa, ngazi zote hizi zitakuwa na uchaguzi wa viongozi wapya kabisa mwaka ujao 2019. Kutokana na katiba inavyosema, watamchagua mtu anayefaa kuongoza nafasi atakayochaguliwa.

Kabla ya uchaguzi huo, nimeona nikuletee ujumbe huu, ambao unakusaidia kujua ni mtu yupi unapaswa kumchagua awe kiongozi wako katika nafasi husika. Hata kama ni mtumishi wa kanisa la mahali, unapotaka kuchagua mtu wa kukusaidia katika eneo fulani, uwe unajua vizuri ni mtu mwenye sifa gani unapaswa kumchagua.

Itakusaidia pia kujua ni mtu gani ulimchagua, lakini amekosa sifa ya kuitwa kiongozi, na hupaswi kumchagua tena aweze kuongoza nafasi aliyochaguliwa. Sio kana kwamba kutomchagua utakuwa umemwonea, au utakuwa na chuki naye, hapana, atakuwa amekosa sifa ya kuwa kiongozi.

Kila kanisa lina utaratibu wake wa kupata viongozi, na wana namna yao, pamoja na hayo tunapaswa kujua mwongozo wetu ni neno la Mungu. Neno la Mungu linatuweka katika mstari mmoja, kupitia Neno la Mungu tunakuwa na ufahamu wa kuelewa nini tunapaswa kufanya.

Kwahiyo mimi sitafungwa na dhehebu lolote katika kufanunua hili, nitafundisha vile Neno la Mungu linasema. Kama litakugusa eneo ambalo hukutaka liguswe, uvumilie tu maana ukweli huwa una maumivu yake makali sana.

Kwanza unapaswa kujua kwamba kuchagua viongozi hakujaanza leo, kumeanza siku nyingi sana, wala sio utaratibu wa kibinadamu, bali ni utaratibu wa kiMungu. Kwa hiyo unaposikia uchaguzi usifikiri ni jambo ambalo watu wamejiundia wenyewe, hapana, wanafuata kanuni ya kiMungu.

Kiongozi yeyote, awe shuleni kwenye vipindi vya dini, awe chuoni kwenye vipindi vya dini, awe ngazi ya mkoa, au awe ngazi ya jimbo, au awe ngazi ya taifa. Lazima ujue mtu unayeenda kumchagua ana sifa na tabia njema, haijalishi ni mzuri sana kimwonekano, kama hana sifa hizi tatu usimchague.

Kwanza, awe mtu mwema, huwezi kuchagua tu mtu ilimradi anasema ameokoka, mtu huyo lazima awe mtu mwema. Hana sifa ya wizi, sio mlevi, sio mzinzi, ni mwaminifu kwa mambo mbalimbali ya Mungu na kanisa, ikiwezekana awe mwaminifu pia kwenye utoaji.

Pili, awe mtu aliyejazwa na Roho Mtakatifu, hili ni lazima kwa mtu anayetaka kuwa kiongozi, usije ukachagua kiongozi ambaye hajajazwa na Roho Mtakatifu. Huyo mtu atawasumbua sana kwenye uongozi wake, tena mtawapa mzigo viongozi wenzake maana atakuwa hawajibiki ipasavyo, kila kitu atataka asukumwe kwa nguvu.

Anaweza kufanya mambo ya hovyo kwa sababu amekosa uongozi wa Roho Mtakatifu, mtu yeyote anayefaa kuwa kiongozi wenu au wako. Unapotaka kumpa kura yako, unapaswa kujua hili, na mtu aliyejazwa Roho Mtakatifu anajulikana. Hasa ukiwa na wewe umejazwa na Roho Mtakatifu itakuwa rahisi zaidi kumtambua.

Ukiona inakupa shida, tazama sifa namba moja niliyokutajia hapo juu, matendo yake yatakusaidia kujua mtu unayetaka kumpa kura yako anafaa au hafai. Roho Mtakatifu ni wa muhimu sana kwa mtu anayetaka kuwa kiongozi wenu/wako, shika sana hili jambo siku zote.

Tatu, awe mtu mwenye hekima, hekima ya kiMungu haiji hivi hivi, lazima maisha yako ya wokovu yawe safi, ndipo Roho Mtakatifu ataweza kukaa ndani yako. Anapokaa ndani yako anakusaidia kuelewa Neno la Mungu, na Neno la Mungu ndilo linampa mtu hekima ndani yake.

Mtu asiye na hekima ya kiMungu ndani yake hataweza kuongoza watu, badala ya kulijenga kundi atalibomoa/atalisambaratisha kwa sababu tu ya kukosa hekima ndani yake. Ipo misimamo ambayo mtu anakuwa nayo, bila kuwa na hekima ya kiMungu anaweza kutumia misimamo yake ya kibinadamu kulipoteza kundi nzima.

Rejea: Basi ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili; na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno. Neno hili likapendeza machoni pa mkutano wote; wakamchagua Stefano, mtu aliyejaa imani na Roho Mtakatifu, na Filipo, na Prokoro, na Nikanori, na Timoni, na Parmena, na Nikolao mwongofu wa Antiokia. MDO 6:3‭-‬5 SUV.

Haleluya, unaona jinsi maandiko matakatifu yanavyotuelekeza namna ya kumpata mtu tunayemtaka awe kiongozi? Vizuri kufuata maelekezo haya, tutaepuka kuwa na viongozi wanaotusumbua, viongozi wanaoua makundi mbalimbali kwa sababu ya tabia zao.

Kwahiyo unapoona mtu hana hizo sifa tatu nilizokutajia hapo juu, huyo mtu hafai kuwa kiongozi wenu/wako. Kiongozi anapaswa awe na hizo sifa, zingine ni za kawaida sana, maana akikosa hizo sifa hata kama awe msomi sana, atawasumbua tu.

Hayo ni mambo machache ya kuzingatia kabla hamjamchagua mtu awe kiongozi, inajulikana mpaka mtu atachaguliwa atakuwa ameonekana ana uwezo fulani wa tofauti na wa pekee. Pamoja na kuwa na uwezo huo wa tofauti, anapaswa awe mwema au tunaweza kusema mwandilifu, awe amejazwa Roho Mtakatifu, na awe mwenye hekima ya kiMungu.

Mkimchagua mtu wa namna hiyo, uongozi wake utamzalia Bwana matunda mema, tena jina la Yesu Kristo halitatukanwa kwa ajili yake. Maana atakuwa ni mtu asiyependa kumkosea Mungu, atajua nafasi aliyopewa kuongoza, anapaswa kuongoza vizuri na kuhakikisha mambo yanaenda vizuri.

Hii ndio faida ya kusoma Neno la Mungu, tukiwa kama wakristo wenye safari ya kwenda mbinguni, tunapaswa kuwa na maarifa ya kutosha ya Neno la Mungu. Bila Neno la Mungu mambo mengi tutakuwa tunafanya kama desturi fulani tuliyoikuta bila kuelewa imetoka wapi, wakati mwingine tunaweza kupuuza baadhi ya mambo kwa kufikiri tofauti.

Hakikisha unasoma Neno la Mungu kila siku, kama hili zoezi linakupa shida, nikualike kwenye darasa letu la kusoma Neno la Mungu kila siku kwa njia ya whatsApp group. Kama una kiu kweli ya kusoma Neno, tuma ujumbe wako whatsApp kwenda namba +255759808081.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com