SOMA

Maisha magumu yamefanya watu waonekane sio kitu sana mbele za watu, watu wamewachukulia kama watu wasio na uwezo wa kuweza kuwasaidia wao. Wamewaona kama wao wenyewe wameshindwa kujitoa kwenye hali walizonazo, watawezaje kuwasaidia wengine? Kweli ni ngumu.

Wengine sio uduni wa maisha, wengine ni ile kujulikana ni mtoto wa fulani, wengine ni ile kujulikana walisoma shule fulani, wengine ni ile kujulikana kuwa walikuwa na maisha fulani mabaya yasiyofaa mbele za Mungu.

Wengine ni watu waliwafahamu walipotoka, kuanzia anazaliwa hadi anakua walikuwa wanamwona, wengine wakacheza naye, na
wengine walisoma naye, na wengine wamekuwa naye katika kazi fulani fulani katika maeneo tofauti tofauti katika kutafuta maisha.

Huenda wengine katika maeneo hayo, hawakuwa watu wanaoonekana wana maono makubwa sana ya kuwa watu fulani. Walionekana ni watu wa kawaida kabisa, na huenda wakati mwingine walionekana ni watu wasiojitambua sana, na wasiojua mwelekeo wa maisha yao ukoje.

Mtu mwingine vile alivyo, alitoa maoni yake fulani kwenu au kwa watu wengine, akaonekane anasema hivyo kama nani. Akaonekane kama ni mtu asiyefaa kuzungumza maneno kama yale, kwa kumhoji anazungumza hivyo kwa nafasi ipi aliyonayo.

Wakati watu wanamfikiria kwa tofauti mtu yule na kumwona sio kitu sana, yeye moyoni mwake anakuwa anafanya hivyo kwa msukumo fulani ulio ndani yake. Anakuwa anafanya kwa sababu ya nguvu ya upendo anayosukumwa nayo ndani yake.

Nyie wengine mnaweza mkamchukulia kama mtu fulani hivi anayejipendekeza kwa kujitoa sana kwa ajili ya vitu fulani, kumbe huyo mtu ndiye Mungu aliyemchagua awe mkombozi/msaada kwenu. Kwa sababu ninyi mnatazama kama wanadamu hamwezi kujua kitu alichobeba huyo mtu ndani yake, wala hamwezi kujua Mungu anavyoanza kumtambulisha kwenu.

Hili tunajifunza kwa Musa, yule Musa aliyewavusha wana wa Israel kwenye bahari ya shamu, huyo ndio Musa ninayezungumza habari zake hapa. Mtu aliyedharauliwa na wale wale aliotakiwa awatoe Misri kwenye nchi ya utumwa.

Musa alikuwa anajaribu kuwaonyesha wana wa Israel waliokuwa Misri kwenye utumwa, kuwaonyesha kuwa yeye ni ndugu yao. Hawakumwelewa hata pale alipowatetea na kuwapatanisha pale walipokuwa wameshindwa kuelewana.

Rejea: Siku ya pili yake akawatokea walipokuwa wakishindana, akataka kuwapatanisha, akisema, Enyi bwana zangu, ninyi ni ndugu. Mbona mnadhulumiana? Lakini yeye aliyemdhulumu mwenziwe akamsukumia mbali, akisema, Ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu na mwamuzi juu yetu? MDO 7:26‭-‬27 SUV.

Hapo Musa aliishia kusukumwa na yule mtu aliyemdhulumu mwenzake, na kumhoji hivi; Ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu na mwamuzi juu yetu? Hicho kitendo kilikuwa kinaonyesha dharau kwa Musa, kwa kumwona anayafanya hivyo kama nani, nani aliyemchagua kuwa mkuu na mwamuzi wao?

Hata siku za leo tunayashuhudia haya, watu wengi wanatuchukulia kawaida sana kutokana na vile wanatufahamu mazingira tuliyokulia. Wengine ni ndugu zetu kabisa wametulea hadi tumefika hapo tulipo, kwahiyo baadhi ya maeneo wanatufahamu udhaifu wetu.

Vile wanatufahamu udhaifu wetu, saa ya Mungu kutubadilisha tabia zetu na mwenendo wetu, wao hawawezi kujua ila wanachojua wao ni mtoto wa fulani, yule tulisoma naye, yule tulicheza naye, ndicho wanakijua wao ila mengine hawajui.

Pamoja na kukudharau kote, pamoja na kukuwekea vikwazo vingi kwenye huduma yako, pamoja na kukuona hujui chochote, pamoja na kukuona huwezi kufika viwango fulani vya juu zaidi katika huduma yako. Saa ya kuinuliwa itakapofika watashangaa wenyewe, watajiuliza mara mia mia huyu ndiye yule fulani au tunamfananisha?

Yule mliyemkataa, au wale waliokukataa ndiye Mungu aliyekuchagua na kukutuma uwe msaada kwa wale wale waliokuwa wanakukataa na kukuona si kitu, wala si chochote. Hawataamini watapokuona unakuwa msaada kwao, hawataamini siku wanakuja wenyewe kukuomba uwasaidie jambo fulani.

Rejea: Musa huyo waliyemkataa, wakisema, Ni nani aliyekuweka kuwa mkuu na mwamuzi? Ndiye aliyetumwa na Mungu kuwa mkuu na mkombozi, kwa mkono wa yule malaika aliyemtokea katika kile kijiti. MDO 7:35 SUV.

Leo tunajifunza sana kwa Musa ila wapo wengi sana wa kujifunza kwao, mfano akina Yusuf aliyeonekana hawezi kuwa mkuu, wakamuuza utumwani Misri, yupo mwingine Daudi aliyekuwa anachunga kondoo za baba yake. Hakuna aliyejua kuwa huyo ndiye dawa ya Goliath, wao walimwona mchunga kondoo tu.

Kwa leo tupo kwa Musa, Musa hakueleweka kabisa ila pamoja na kutokueleweka huko, Mungu hakubadilisha maamzi yake kwa Musa. Pamoja na Musa aliyeonekana hana sifa, Mungu alimwona ana sifa zote.

Kaka unaweza kujiona wewe ni mtu wa kawaida sana, huwezi kuoa yule mke mzuri unayemtaka kutokana na hali yako, ukiwa na Yesu Kristo usiogope hilo. Jikubali na amini Mungu atakupa mke wako mzuri, wala usitishwe na hali ya nje, endelea kuweka bidii zaidi kwa Mungu na Mungu atashughulika na mambo yako.

Wale wale waliokuona huna cha kuwasaidia, utageuka msaada mkubwa kwao, wale waliokuona utaishia kupanga kwenye nyumba za watu, hao hao watakuja kuwa wapangaji wako. Hata kama sio wao moja kwa moja, watoto wao na ndugu zao watakuja kuwa wapangaji wako.

Acha wakukatae sasa na wakuone huna kitu, hilo lisikuogopesha na kujiona hufai, Mungu anakuona namna ya tofauti sana kuliko mwanadamu mwenzako akutazamavyo. Watashangaa siku wanaenda kutafuta msaada ofisi fulani, wanakukuta wewe ndiye boss wa ofisi ile.

Hebu nikusihi usome Neno la Mungu kila siku, kama hujaanza hili jambo, anza sasa, na kama unaona unaanza alafu unakuja kuishia njiani. Tafuta watu wa kuenda nao kwenye hili, kama unaona ni ngumu kuwapata, karibu kwenye group letu la kusoma Neno la Mungu kila siku. Tuma ujumbe wako whatsApp namba +255759808081, hapa utakutana na timu kubwa inayosoma Neno.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com