Kuna watu ni mwiba mkubwa sana kwa watumishi wa Mungu wa kweli, hawapendi kuwaona wakihubiri kweli ya Mungu. Kwao wanaona hawatakiwi kufanya hivyo, maana wanawaharibia kazi zao.

Shetani anawatumia pasipo wao kujua, ama kujua kuwa wao ni mawakala wa shetani, ambao hawapendi kuwaona watumishi wa Mungu wakisimama katika kweli ya Kristo. Kwao jina la Yesu Kristo kutajwatajwa ni kama wametamkiwa Neno baya sana lisilofaa kwenye maisha yao.

Wakishaona jina la Yesu Kristo linazidi kuenea, watu wanaokoka, watu wanakimbilia imani sahihi, wao wanapata tabu sana kwa sababu wanaona wanazidi kukosa watu.

Tukiachana hilo la kuwadhuru watumishi wa Mungu, tuangalie eneo lingine tena ambalo watu wengi wanatumiwa na shetani kuwahaingaisha watumishi wa Mungu.

Wapo watu kazi yao ni kuhakikisha mtumishi wa Mungu hana amani, wataibua kila jambo kuhakikisha huyo mtumishi haendelei na huduma yake. Watakuja na hili leo, kesho watakuja na lingine, kesi hazitaisha kwa mtumishi huyo wa Mungu.

Ukiwa kama mtu wa kusikia tu maneno, unaweza kufika mahali ukasema labda maneno yanayosemwa yatakuwa ya kweli, kumbe hayana ukweli wowote ni chuki tu za kutaka kumwangusha mtumishi wa Mungu.

Unaweza kusikia mchungaji fulani amezini na mshirika wake, kumbe ni kitu ambacho kimetengezewa ili mchungaji yule aonekane hafai kuchunga kanisa. Sababu haswa, ni kwa sababu kuna watu wanashindwa kufanya mambo yao kwa uhuru wanaotaka.

Ni kama mchungaji au mtumishi yule amekuwa kizuizi wa maovu yao, wakitaka kupitisha jambo fulani la kuua kanisa, yeye anasimama wima kuhakikisha hilo jambo halipiti.

Mtu yeyote anayesimamia kweli ya Mungu, haijalishi ni mshirika wa kawaida kabisa, huyo mtu ni adui mkubwa sana wa shetani. Huyo mtu haishi kuwekewa mitengo ya kumpoteza uhai wake, labda mtu huyo awe hana nguvu kubwa, ila kama ana nguvu kubwa atatafutwa usiku na mchana.

Pamoja na hiyo vita kubwa kwa watoto wa Mungu, inafika saa Yesu anasema imetosha kuwasumbua watoto wangu, maana mtu yeyote anayemsumbua mtumishi wa kweli wa Mungu. Anakuwa amegusa mboni ya jicho la Mungu, saa ya Mungu ikifika, huyo mtu atashughulikiwa kisawasawa na Mungu.

Mtu anayeua watu wa Mungu, watu wanaoisimamia kweli ya Mungu, watu hao wanaweza kujiona watadumu milele, ila hawajui itafika mahali watakwama kabisa. Pamoja na ubabe wao wote, ipo siku na saa watapambana na Yesu mwenyewe.

Hili tunajifunza kwa Sauli, Sauli alikuwa ni mwiba mkubwa kwa Mitume wa Yesu, alikuwa kinyume kabisa na mtu yeyote aliyekuwa anatangaza habari za Yesu Kristo. Hiyo chuki ilimfanya afanye mambo mabaya sana kwa watu wa Mungu.

Wakati anaenda kutekeleza mpango wake wa kuua, Yesu Kristo alimshukia mwenyewe, alisema na Sauli kwa sauti na kumpiga upofu. Kuanzia siku hiyo hakuwa na nguvu tena ya kufanya mauji yake, badala yake na yeye alianza kutafuta msaada.

Rejea: Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, Sauli, Sauli, mbona waniudhi? Akasema, U nani wewe, Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi Yesu unayeniudhi wewe. Sauli akainuka katika nchi, na macho yake yalipofumbuka, hakuona kitu; wakamshika mkono wakamleta mpaka Dameski. Akawa siku tatu haoni; hali, wala hanywi. MDO 9:4‭-‬5‭, ‬8‭-‬9 SUV.

Ndugu, kiburi cha mtu cha kufanya mambo mabaya kwa watumishi wa Mungu ni kwa sababu tu huyo mtu saa yake haijafika. Mungu anaona na anasikia kilio cha watu wake, kuugua kwao anajua sana, saa yao ya kushughulikiwa na Yesu ikifika watajua kumbe tunamtumikia aliye hai.

Nani angejua Sauli angekuja kuwa mtumishi mzuri, zile zile habari alizokuwa anazipinga mwenyewe, ndizo alikuja kuwa anazisema kwa kinywa chake. Watu walishangaa na kufikiri anafanya utani, ila walioona kilichompata hakuwa wanaona anafanya utani.

Rejea: Mara akamhubiri Yesu katika masinagogi, kwamba yeye ni Mwana wa Mungu. Na wote waliosikia wakashangaa, wakasema, Siye huyu aliyewaharibu walioliitia Jina hili huko Yerusalemu? Na hapa alikuwa amekuja kwa kusudi hilo, awafunge na kuwapeleka kwa wakuu wa makuhani? Sauli akazidi kuwa hodari, akawatia fadhaa Wayahudi waliokaa Dameski, akithibitisha ya kuwa huyu ndiye Kristo. MDO 9:20‭-‬22 SUV.

Jeuri ya mtu ni kwa sababu Yesu ameamua kumpa nafasi tu, ila siku akimwamlia huyo mtu, jeuri yake yote itakwisha. Usije ukafikiri Yesu anafurahia vile unakosa usingizi mzuri kwa sababu ya mtu fulani amegeuka mwiba kwako.

Yesu hafurahii hata kidogo, siku ikifika ya kumshughulikia huyo mtu, atageuka rafiki mzuri sana kwako, unaweza kushangaa anakuwa upande wako wa kusimamia kweli ya Mungu. Inaweza kushangaza watu na wengine wasiamini sana ila ndio utakuwa ukweli wenyewe.

Mtu yeyote ukiona anaua watu kwa sababu ya Yesu Kristo, jua bado Yesu hajaamua kumshughulikia, siku ikifika ataona moto wake. Na kupitia yeye watu wengi wataamini jina la Yesu Kristo, cha msingi ni kuendelea kusimama na Mungu.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com