Kwanza tupo siku ya tatu tangu tuanze mwaka mpya 2019, wapo tayari wameshapanga malengo yao, na wapo bado hawajapanga malengo yeyote ya mwaka huu.

Wapo wanaona ya nini kupanga malengo mapya au ya nini kuweka mipango mipya ya mwaka huu mpya, wakati yale ya mwaka jana karibia robo tatu hawajayatimiza.

Yupo mtu alipanga mwaka uliopita lazima aoe/aolewe na taratibu zote zilikuwa zinaenda vizuri kabisa, wengine walifika hatua ya kuvalishana pete za uchumba mwanzoni kabisa mwa mwaka 2018. Lakini hadi wanaingia mwaka 2019 hakuna kilichofanikiwa zaidi ya kuvalishana pete.

Wengine pamoja na kuvalishana pete za uchumba, walifika mahali wakaachana kwa ugomvi mkubwa sana, wengine waliachana kwa sababu mmoja alimgundua mwenzake anatembea na wanawake/wanaume wengine.

Yupo mtu anahitaji mtoto kwa muda mrefu, aliona kabisa mwaka uliopita lazima angepata mtoto, maana na ujazito ulikuwepo wa siku chache wakati anapanga mipango yake. Lakini baada ya miezi kadhaa kupita, ndoto zake zilififia baada ya ujauzito ule kutoka.

Mwingine mwaka uliopita ulikuwa ni mwaka wake wa kwenda chuo, wakati anaweka mipango hiyo kila kitu kilikuwa kipo vizuri kabisa. Ila baadaye mambo yalienda tofauti kabisa na alivyopanga na hadi mwaka unaisha hakuwa ameenda chuo chochote.

Yupo kijana alipanga mwaka jana lazima akatoe mahari/posa kwa binti aliyetarajia kumwoa, taratibu zote za kwenda kujitambulisha kwa binti na kutajiwa mahari zilishakamilika kabisa. Kazi yake kubwa ilikuwa kutoa mahari/posa aliyotajiwa, na alipewa muda hadi kufikia mwezi fulani awe amekamilisha mahari yake.

Pamoja na kuwa na matumaini makubwa sana ya kupata mahari aliyotajiwa, kutokana na mipango yake aliyokuwa ameweka. Baada ya muda fulani kupita, mipango yake yote ilivurugika na hadi anaingia mwaka mpya hakuna kilichokuwa kinaendelea.

Wazazi/walezi wa binti wamecharuka na kumwona ni mtu mbabaishaji tu, na binti ameanza kujazwa maneno ya kumwacha, kumbe kaka yule amekwama kabisa. Mipango yake yote ya fedha imevurugika kabisa, na kila anayemwomba msaada anamwambia hana.

Yupo alipanga kumalizia nyumba yake kabla ya mwaka 2018 kuisha, ila mipango yake haikwenda kama alivyopanga. Nyumba ipo pale pale hadi anaingia mwaka mpya, ni kama amevurugika hivi, ndio maana haoni maana yeyote ya kupanga malengo yeyote.

Mipango/malengo yapo mengi sana watu waliyopanga mwaka jana, siwezi kuyataja/kuitaja nikaimaliza yote kutokana na nafasi yangu finyu, ila wewe binafsi unajua ni mipango gani uliipanga na hadi mwaka unaisha hukutimiza mipango yako.

Kuna mahali ulikuwa unakosea bila wewe kujua, fahamu unapopanga mipango yako yote ya mwaka, ya mwezi, ya wiki, ya siku, unapaswa kumkabidhi Bwana mipango yako yote.

Usianze tu kienyeji bila kumkabidhi Bwana mipango yako yote, Mungu awe wa kwanza kwenye shughuli zako zote, kama kazi unapaswa kumwambia Yesu kile unatamani kitokee mwaka huu mpya. Hadi unafika mwishoni kabisa mwa mwaka huu uone hatua uliyopiga.

Bila Mungu huwezi kitu, anajua sawa ulichopanga ila Mungu anataka umweleze kwa kinywa chako mwenyewe. Yale yote umepanga mwaka huu, hakikisha mipango yako yote unamkabidhi Bwana, usione jambo dogo utaliweza mwenyewe.

Usione una uwezo mkubwa wa kuyafikia hayo malengo uliyojiwekea, bila Mungu, pamoja na uwezo wako mkubwa, hakuna utakachoweza kukifanya. Cha msingi ni kuhakikisha unamkabidhi Bwana mipango yote ya mwaka huu.

Sio mkabidhi mara moja na kukaa kimya, ni kuendelea kuombea mipango yako kila mara, kadri unavyopiga hatua kwenye malengo yako, usiache kumwambia Yesu. Usifurahie matokeo mazuri ukaacha kuomba, jua bado unamhitaji Mungu.

Rejea: Mkabidhi BWANA kazi zako, Na mawazo yako yatathibitika. MIT. 16:3 SUV.

Unaona huo mstari, sikuelezi habari za kwangu, nakueleza fundisho lililotokana na Neno la Mungu. Ili uweze kuona matunda ya kile umepanga mwaka huu, unapaswa kumkabidhi Bwana Yesu mwenyewe, ndipo utaona mafanikio kwa kile ulichopanga.

Hata kama mipango yako uliyopanga haitatimia kama ulivyopanga, hutokuwa kama mtu yule ambaye hakumkabidhi Bwana mipango yake. Wewe utakuwa unajua hatua uliyofikia na kukwama ni kwa sababu fulani za msingi, moyoni utakuwa na amani kabisa.

Mungu ametupa akili nyingi sana tuzitumie, ila epuka sana mtego wa kuzitegemea akili zako, mkabidhi Bwana mipango yako yote uliyojiwekea katika maisha yako. Kama lipo umepanga litimie mwaka huu, na likawa halijatimia mwaka huu, Roho Mtakatifu atasema nawe.

Hii ndio faida ya kuwa na Neno la Mungu kwa wingi moyoni mwako, bila Neno la Mungu huwezi kuelewa hili, utaishia kulalamika tu. Hakikisha unasoma Neno la Mungu kila siku, pia nakukaribisha kwenye kundi la wasap la kusoma Neno la Mungu. Tuma ujumbe wako wasap namba +255759808081.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com