
Zipo nyakati ambazo watu wa Mungu wanazipitia, nyakati ambazo wengi wamefika wakati wamechoka, wamelia sana sana mbele za Mungu. Lakini pamoja na kulia kwao sana, bado wanaona shida yao ipo pale pale.
Machozi yao yamekuwa yakilowanisha magoro yao, usiku kucha hawalali wanalia, mchana kutwa wanajaribu kujikaza ila wanajikuta machozi yanawatoka tu yenyewe. Ni kama macho yamekosa nguvu ya kuyazuia machozi yao yasitoke.
Ipo mizigo mizito wameibeba mioyoni mwao, mizigo ambayo hawana mtu wa kuwasaidia kuibeba, ni Mungu pekee ndiye anayeweza kuwasaidia. Kila wakijitahidi kutafuta furaha ya mioyo yao, bado wanaona tatizo lao limesimama palepale.
Nyakati kama hizi inakuwa ngumu hata kuomba kwa mtu huyu, wengi wanabaki wanalia tu, wakienda mbele za Mungu, badala ya kuomba Mungu, wao wanakuwa wanalia tu. Hawalii kwa sababu wanadeka sana, ipo mizigo mizito kwenye maisha yao.
Rejea: Nimechoka kwa kuugua kwangu; Kila usiku nakieleza kitanda changu; Nalilowesha godoro langu kwa machozi yangu. Zaburi 6:6.
Sio kana kwamba huyu mtu hajaokoka, kuokoka ameokoka ila amezidiwa na majaribu, kwake anaona ni moto mkali, kwenye maisha yake huenda hajawahi kukutana na jambo gumu kiasi hicho.

Mbaya zaidi ukute wakati bado yupo vizuri, yaani hapiti kwenye jaribu gumu kama hilo linalomfanya alowanishe mashuka na godoro lake kwa machozi. Alikuwa hasomi Neno la Mungu, kwa hiyo Neno la Mungu halimo moyoni mwake, kama halimo moyoni mwake lazima alemewe na jaribu lake.
Mtu aliye na Neno la Mungu la kutosha moyoni mwake, haijalishi anapitia gumu gani, hawezi kulingana na mtu asiye na Neno la Mungu, kwanza hawezi kulia kama mtu asiye na matumaini. Tena yapo majaribu mengine anaweza kuwa anapitia na usijue kabisa kama anapitia kwenye wakati mgumu.
Wapo watu wamelia sana kiasi kwamba wale watu wasiomjua Mungu, wameanza kuwapa maneno ya kejeli, kuwaambia Mungu wao yupo wapi. Maana kama wana Mungu kweli, kwanini Mungu wao amewaacha wamekuwa watu wa kulia tu.
Rejea: Machozi yangu yamekuwa chakula changu mchana na usiku, Pindi wanaponiambia mchana kutwa, Yuko wapi Mungu wako. Zaburi 42:3.
Wengine wamegeuka kero kwa wazazi wao, maana wazazi wao hawalali usiku wanahangaika kuwanyamazisha, wengine wamegeuka kero kwa majirani, wengine kwa waume zao, wengine kwa wake zao, wengine kwa ndugu zao, na wengine kwa wachungaji wao.
Ukisikia mtu analia ujue analia kweli, na mtu anayelia hawezi kula chakula akashiba, hata kama atakula, atakula kidogo sana. Maana ile hamu ya kula hana, na akiendelea kula chakula kidogo kwa muda mrefu, afya yake itaharibika sana.
Mtu wa namna hiyo anaweza kupauka mpaka ukamhurumia, unaweza kufikiri labda anaugua TB, unaweza kufikiri labda anaugua UKIMWI, kumbe ni jaribu gumu analopitia. Usiku na mchana ni mtu wa kulia tu, machozi yake yamegeuka chakula chake, machozi yake yamegeuka maji yake ya kunywa.
Hata ile kuyafuta hayo machozi hakumo tena, yamebaki yanatoka yenyewe, ndio wakati ambao wanaona Dunia nzima imewaangukia wao. Kama hujawahi kupita kwenye wakati kama huu huwezi kuelewa vizuri hili ninalokueleza hapa, ila wale waliopita wanajua.
Pamoja na hayo yote magumu, Mungu husikia kulia kwao, machozi yao Mungu hufika wakati akawafuta na kuwanyamazisha kabisa. Ni kama ilikuwa ngumu kunyamaza ila inapofika wakati wa Bwana, kila kitu huwa shwari.
Rejea: Enenda ukamwambie Hezekia, Bwana, Mungu wa Daudi, baba yako, asema hivi, Mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitaziongeza siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano. Isaya 38:5.
Ndugu yangu, kama unasoma ujumbe huu na upo kwenye wakati mgumu sana, wakati ambao unakufanya utoe machozi, wakati ambao unamwomba sana Mungu akatoe kwenye hali hiyo ya machozi. Amini Mungu anakusikia, usichoke kusubiri wakati wa Bwana.
Ukiwa na imani mbele za Mungu, hutojidharau, wala hutofika mahali ukatamani kujiua, watu wa Mungu huwa hawatamani kunywa sumu, watu wa Mungu huwa hawafikirii kujinyonga. Kama mawazo kama hayo yameanza kukujia kichwani mwako, tubu haraka mbele za Mungu, maana Mungu ameyaona machozi yako.
Mungu atageuza kulia kwako na kuwa kicheko, ni kama kitu kisichowezekana ila amini Mungu anaweza mambo yote, haijalishi unapita kwenye mlima mkali sana. Uwe na uhakika Mungu atakuvusha salama, hata wale waliosema Yesu wako yupo wapi, watageuza maneno wenyewe na kusema “hakika huyu mtu ana Mungu wa kweli”.
Usiache kusoma Neno la Mungu kila siku, unaweza kuungana na wenzako wanaosoma Neno la Mungu kila siku kwa njia ya wasa, ili uunganishwe kwenye kundi hili. Tuma ujumbe wako wasap namba +255759808081.
Soma Neno Ukue Kiroho.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com