
Sio kitu cha ajabu kabisa kumwona mtu ameokoka sawasawa, lakini bado kuna vitu vya nyuma vinamtesa, anajiona bado ana hatia kubwa mbele za Mungu. Bila kumlaumu sana huyu ndugu, nikueleze ukweli mtu huyu amekosa maarifa sahihi ya Neno la Mungu.
Wapo watu hawana amani kabisa kwenye maisha yao ya wokovu, unaweza kufikiri labda ni kwa sababu kuna mahali bado wanachanganya maisha yao. Ila ukweli wapo hawana michanganyo ya aina yeyote, ila sababu inayofanya wawe hivyo ni ile kushindwa kujisamehe wenyewe.
Mtu anaweza akawa alikuwa ameokoka vizuri, baadaye akarudi nyuma, alivyorudi nyuma kuna vitu vingi vibaya alivifanya katika maisha yake ya dhambi. Vitu hivyo huenda vimeleta hasara kubwa sana kwenye maisha yake, kila anapovikumbuka anaona Mungu bado hajamsamehe.
Huenda mtu alikuwa jambazi, akaua hadi na ndugu zake wa damu kabisa, sasa hayo aliyafanya akiwa mtumwa wa shetani. Sasa kama amekubali kuokoka na kuachana na hayo yote mabaya, mtu mwingine anakuja kujiona hawezi kusamehewa kabisa kwa matukio makubwa aliyofanya.
Katika jamii zetu, tunaona watu wengi wakiua ndugu zao kwa sababu ya kutafuta mali/utajiri, wapo wameua watoto wao wazuri, wapo wameua mama zao, wapo wameua baba zao. Siku wanaamua kumrudia Mungu, wengine wanakuwa wanalia kila siku kwa kufikiri Mungu bado hajawasamehe maovu yao.
Yupo mwingine alizalishwa watoto na wanaume tofauti tofauti kabla ya kuolewa, wanaume wote hao hakuna aliyemwoa zaidi ya kumzalisha na kumwacha hapo. Alivyoona anachokifanya sio sahihi mbele za Mungu, aliamua kumpa Yesu Kristo maisha yake, lakini pamoja na kumpa Yesu Kristo maisha yake. Bado anajiona ana hatia mbele za Mungu.
Mwingine amezalishwa mtoto na mwanaume aliyemdanganya atamwoa, baadaye mwanaume huyo alimkimbia na kwenda kuoa mwanamke mwingine tofauti kabisa. Alivyoona maisha ya hivyo sio mazuri bora kukimbilia kwa Yesu Kristo, bado hicho kitu hakijatoka moyoni mwake, anajiona ana hatia mbele za Mungu.
Hasa anapoona wenzake wanaolewa na wanaume wazuri ila yeye haoni mwanaume wa kumwoa, kama ni kuomba ameomba sana, tena zile siku za mwanzo wakati ameokoka alikuwa na bidii sana kwa mambo ya Mungu. Huwezi kumkosa kwenye vipindi vya mafundisho ya Neno la Mungu, na huwezi kumkosa kwenye vipindi vya maombi kanisani.
Baada ya miaka kadhaa kupita, anaona hakuna kinachoendelea kwake, alafu wakati huo ana hamu ya kuitwa mke wa mtu. Dada/mama huyo hujiona mwenye hatia mbele za Mungu, tena anajiona bado hajasamehewa makosa yake.
Mwanaume mwingine kwa sababu alikosea mwanzo, akazaa kienyeji na mwanamke ambaye hakufuata taratibu zozote, au alifuata taratibu zote kabisa. Ila wakati anaoa maisha yake ya kiroho hayakuwa vizuri, akabeba mke ambaye hakuwa chaguo la Mungu kwake, wakafika mahali ndoa yao ikasambaratika kabisa.
Mwanaume huyu pamoja na kuamua kumrudia Mungu, na kuomba toba ya nguvu, na kujiona kabisa Mungu amemsamehe dhambi zake. Yeye mwenyewe bado anajiona ana hatia, akifikiria alichezea ujana wake vibaya, akijiona alipoteza muda wake vibaya kwa mtu asiye sahihi, akijiona kwanini hakuwa na subira.
Mtu mwingine alipata magonjwa mabaya kwenye kuruka-ruka kwake, huenda alipata na ugonjwa wa ukimwi, wengi hatupendi kusikia kitu kama hichi ila ni ugonjwa ambao upo na unawatesa watu wengi sana. Japo siku hizi haonyeshi sana kama wanaugua huo ugonjwa, sasa mtu huyu anakuwa anajiona mwenye hatia kubwa.
Pamoja na kuokoka kwake, na Yesu Kristo kumsamehe makosa yake, yeye mwenyewe bado hajajisamehe makosa yake. Kama hajajisamehe makosa yake, haijalishi Yesu amemsamehe dhambi zake, bado ataendelea kuteseka kwenye gereza.
Huu ni mtego ambao watu wengi wameshindwa kuutambua kama ni mtego mbaya sana kwao, kwa kukosa kwao maarifa sahihi ya Neno la Mungu. Shetani amepata nafasi ya kuwatesa ndani ya mioyo yao, kwa kuwafikirisha kuwa bado hawajasahemewa dhambi zao.
Ndugu yangu, najua umeteseka sana kwenye eneo hilo, ukijiona bado una hatia mbele za Mungu, hasa unapoona mambo hayawi kama ulivyotarajia yawe baada ya kuokoka kwako. Hujui kuwa hayawezi kuwa vile unataka yawe, lazima usubiri wakati wa Bwana ufike, ndipo utaona mafanikio.

Kama ulikuwa unafikiri bado hujasamehewa na Mungu, kuanzia sasa ondoa hayo mawazo kabisa, Yesu Kristo ameshakusamehe dhambi zako zote ulizozitenda siku umeokoka. Tena sio kukusamehe tu, ameshazisahau kabisa, hazikumbuki tena.
Rejea: Kwa sababu nitawasamehe maovu yao, Na dhambi zao sitazikumbuka tena. EBR. 8:12 SUV.
Hupaswi kuteseka kwenye hatua ambayo umetoka huko, wewe ulikuwa mwenye dhambi zamani, ukaamua kuachana na hayo, na ukaamua kuokoka kwa hiari ya moyo wako. Hupaswi kabisa kuendelea kujiona mwenye hatia mbele za Mungu.
Wapo watu wanashindwa kufanya mambo makubwa mbele za Mungu, mambo ambayo yanamletea Mungu sifa na utukufu. Kwa kufikiri labda watu wataibua makosa yao ya zamani, bila kujua hata kama wakiyaibua Mungu alishawasamehe na hayakumbuki tena.
Rejea: Dhambi zao na uasi wao sitaukumbuka tena kabisa. EBR. 10:17 SUV.
Hata kama mtu atakuja kukuambia mbona wewe ulikuwa mtu wa namna hii, yaani akakutajia matukio yako mabaya uliyotatenda huko nyuma, au huenda sio siku nyingi sana. Huenda ulifanya wiki iliyopita, au huenda ulifanya jana, lakini leo umeamka umeamua kuokoka na kutubia mambo yote mabaya uliyofanya.
Jibu utakalompa, mwambie hayo unayonieleza yalikuwa mambo ya zamani, ila sasa wewe ni kiumbe kipya. Usiwe na hofu yeyote kwa watu ambao watataka kukushambulia kwa maneno, kama una uhakika wanayosema ni ya ukweli, usione shaka kuwajibu kama Roho Mtakatifu atakupa kibali cha kufanya hivyo.
Wewe Mungu ameshakusamehe dhambi zako zote, hata kama watu bado wanakataa kukusamehe pamoja na kuwaomba msamaha, hilo lisikufanye ujione mwenye hatia mbele za Mungu. Kama hawataki na wewe umeshawaomba msamaha, waache watamalizana na Mungu, wewe huna hatia yeyote.
Rejea: Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe, wala sitazikumbuka dhambi zako. ISA. 43:25 SUV.
Acha kujikondosha bure kwa mawazo mengi, acha kujisababisha presha bure, acha kujiona hufai tena, maadamu bado unaishi, bado unaitwa fulani. Na bado hujaanza kuitwa marehemu, una nafasi ya kufanya vizuri zaidi kuliko mwanzo, heri mwisho wa jambo kuliko mwanzo.
Hakuna mtu atakayeingia mbinguni kwa mwanzo mzuri, tutaingia mbinguni kwa mwisho mwema, anza vizuri na Mungu. Lakini hakikisha unamaliza vizuri na Mungu, ndivyo maandiko yanavyosema, usije ukajisifia sana kwa mwanzo mzuri alafu mwisho wako ukawa mbaya. Uwe na uhakika mbingu hutaingia.
Acha kabisa kujiona hufai, Mungu anakuona unafaa sana, anakutaka uzae matunda mema, maana haukumbuki tena uovu wako, baada ya kukusamehe. Nimekupitisha kwenye mistari kadhaa uweze kuona hili ninalokueleza hapa.
Acha kutabishwa na mafundisho potovu, mara uambiwe una laana za wazazi wako, mara uambiwe una laana za kuzaa bila kufunga ndoa, waambie ilikuwa zamani kabla hujaokoka. Kwa sasa umeokoka huna tena hizo laana, wewe ni kiumbe kipya kabisa.
Mwisho, nikualike kwenye kundi la kusoma Neno la Mungu kila siku, Neno ambalo linaponya majeraha ya moyo wako, Neno ambalo linakupa uhakika wa safari yako ya wokovu. Kundi hili ni la wasap, tuma ujumbe wako wasap namba +255759808081.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com