Majuto ya watu wengi waliokoka yamekuja baada ya kukaidi sauti ya Roho Mtakatifu, waliambiwa usifanye hivi wao wakafanya, waliambiwa usiende huko wao wakaenda, waliambiwa usioe huyo mwanamke wao wakaoa, waliambiwa usiolewe na huyo mwanaume wao wakaolewa.

Mungu anaweza kusema nawe usimwelewe, kwa kuwa Mungu wetu anatupenda na kile anazungumza nasi anataka tuelewe, ametumia watumishi wake kusema nasi ili tuweze kuelewa sauti yake.

Wakati mwingine anaweza kutuonyesha kabisa kwa macho ya nyama kile ambacho anaona ni hatari kwetu, kama ulikuwa na mchumba wako ambaye sio sahihi. Anaweza kukuonyesha mchumba wako huyo akiwa anafanya vitendo visivyofaa, vitendo ambavyo kwa mtu aliyeokoka hawezi kufanya.

Labda nikupe mfano huu rahisi unaweza ukanielewa zaidi, hajawahi kuwa kwenye safari ya kutembea kwa miguu, ukafika mahali ukasikia kusita kuendelea mbele. Ukajaribu kulazimisha kuendelea kufuata hiyo njia ila kadri unavyozidi kwenda mbele, unasikia kelele ikipiga ndani yako ubadili njia.

Kama hutotii hiyo sauti iliyokuwa inakuzuia usiendelee kufuata hiyo njia, linakutokea jambo baya sana, baadaye unakumbuka ulikosa amani kufuata hiyo njia. Wengine husema machale alinicheza kabisa kuwa hii njia sio nzuri, lakini mimi nililazimisha kuifuata.

Labda mfano huo wa kutembea kwa miguu unaweza ukawa mgumu kwako hasa kama usafiri wako mkuu ni kutembea kwa gari, lakini najua umekutana na hili hata kama usafiri wako mkuu ni magari. Unaweza ukaamka unajisikia mzito kusafiri, sio kwamba ni uvivu ila ghafla unakosa amani ya safari yako na kujisikia kukosa amani moyoni mwako.

Ukashindwa kuelewa sauti ile iliyokuwa inasema na wewe, unaanza safari yako, katikati ya safari unaenda kukutana na ajali mbaya sana. Unaweza ukapona wewe ila gari lako likaharibika vibaya sana, unasikia tena ndani yako ile sauti inakumbusha kuwa ilikuambia usiende.

Wapo pia wamekuwa wakitii sauti zile ambazo zinasema nao, baada ya kutii sauti zile ambazo zilisema nao, wameona matokeo mabaya kama wasingetii sauti zile. Wengine wameshuhudia ajali mbaya baada ya kutii kutopanda gari fulani au kutopita njia ile.

Wapo wameshuhudia mtu akiuawa vibaya sana kwenye njia ile ile ambayo walikatazwa na Roho Mtakatifu wasipite, huenda hawakuelewa sana kama Roho Mtakatifu alisema nao. Ndio maana nikasema wengine husema “NILICHEZWA NA MACHALE” ni msemo ambao unapaswa kutumiwa na watu wasiomjua Kristo, ila wakristo ndio tumeufanya wa kwetu.

Wengine Roho Mtakatifu amewazuia kuolewa na mwanaume fulani, sio kana kwamba hajaokoka, kuokoka ameokoka vizuri kabisa, isipokuwa Mungu anajua sababu ya kuzuia hilo.

Ukipata nafasi ya kuongea na wale ambao waume/wake zao wamekufa siku chache baada ya kuingia kwenye ndoa, mmoja wapo aliyesimama vizuri na Mungu alisema naye ila hakutii ile sauti na kuipuuza.

Ukipata nafasi ya kuongea na mtu ambaye anasumbuliwa na ndoa yake, atakwambia kabisa aliona viashiria vingi sana kwa huyo mume/mke wake kuwa sio mtu sahihi kwake. Kuna wakati Mungu alitumia watu wake wa karibu kumwambia huyo mtu sio mtu mzuri, wakampa na vithibitisho kabisa.

Na yeye moyoni aliona kabisa anakosa amani juu ya yule anayetaka kuishi naye kama mume na mke, lakini alipuuza hivyo vyote na kuona ni shetani tu hataki yeye kuoa/kuolewa na huyo anayemtaka yeye.

Sio mahusiano tu, yapo mambo mengi sana Roho Mtakatifu alitukataza kufanya ila tulipuuza na tukajikuta tumeingia kwenye hatari kubwa sana. Mwingine Roho Mtakatifu alisema naye juu ya biashara yake, alikuwa anasikia usichukue mzigo mkubwa sana, chukua kidogo, yeye akaona ni usumbufu kurudi mara kwa mara.

Alishangaa aliuza nusu ya mzigo baadaye akasikia bei imeshuka, kwa hiyo ile nusu nyingine ya mzigo akawa ameuza kwa hasara kubwa. Hata ile bei aliyonunulia mzigo ikawa haijafika, utasikia anaanza kusema nilikuwa nasukumwa kuchukua mzigo kidogo ila nikawa nakataa.

Wote tunapaswa kujua hili, tunapaswa kutii sauti ya Roho Mtakatifu anapotukataza jambo fulani tusifanye, tunapaswa kutii hayo maagizo. Kutii kwetu kutatuepusha na majanga mengi sana katika maisha yetu.

Wengine leo nyumba zao zimekutwa na bomoabomoa kwa sababu ya kutotii sauti ya Roho Mtakatifu alivyosema nao siku ya kwanza kabisa wakati wananunua kiwanja. Wengine wametapeliwa pesa zao kwa kuuziwa viwanja feki, lakini kabla ya kutoa pesa zao, Roho Mtakatifu aliingilia kati, wakaona ni mawazo potovu.

Hili tunajifunza kupitia Neno la Mungu, tangu zamani Roho Mtakatifu alisema na watumishi wa Mungu. Walipofika mahali waliambiwa wasihubiri Neno la Mungu mahali fulani na wasiende mahali fulani;

Rejea: Wakapita katika nchi ya Frigia na Galatia, wakikatazwa na Roho Mtakatifu, wasilihubiri lile neno katika Asia. Walipofika kukabili Misia wakajaribu kuenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu hakuwapa ruhusa. MDO 16:6‭-‬7 SUV.

Hebu jiulize katika huduma yako, Roho Mtakatifu amekuzuia mara ngapi kwenda mahali fulani kutoa huduma ila wewe ulilazimisha kwenda? Na baada ya kulazimisha kwenda bila shaka uliona madhara makubwa.

Na wakati mwingine tumeona kama Mungu alikaa kimya, kumbe alisema nasi kabla ya kufanya kile ambacho tulipanga kufanya. Baada ya kuona hatutaki kumsikiliza, alituacha tufanye tunavyojua wenyewe.

Jifunze kumsikiliza Roho Mtakatifu, maana mambo mengi sana tumeingia kwa kushindwa kumsikiliza Roho Mtakatifu. Badala yake tumekuwa na majuto makubwa kwenye maisha yetu, kwa sababu tulikatazwa mapema sana sisi tukapuuza.

Kupitia somo hili ukapone kwa jina la Yesu Kristo, pia nakusihi sana uwe na bidii ya kusoma Neno la Mungu kila siku. Usisikilize sauti inayokuambia usisome Neno la Mungu. Unapenda kujiunga na kundi letu la kusoma Neno, tuma ujumbe wako wasap namba +255759808081.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com