Sijui nani alitudanganya, nasema hivyo kwa sababu wengi tukikutana na mambo magumu katika maisha yetu, huwa tunasitisha na huduma, mtu alikuwa msomaji mzuri sana wa Neno anaacha, mtu alikuwa mhudhuriaji mzuri wa ibada anaacha, mtu alikuwa mwimbaji mzuri wa nyimbo za injili anaacha, mtu alikuwa mwombaji mzuri anafika mahali anaacha kuomba.

Kuacha huku sio kwa sababu inampa unafuu wa magumu yake anayopitia, anaona ni heri kupumzika kwanza hadi pale magumu yale anayopitia yatakapoisha kabisa au yatakapopungua kabisa. Badala yake anashangaa linaisha jambo hilo na linakuja lingine jipya kabisa.

Mwingine alivyosubiri magumu au tunaweza kusema changamoto au unaweza kusema majaribu yake yaishe, ule moto wake wa kumtumikia Mungu uliisha kabisa. Pamoja na kuisha kwa yale magumu aliyokuwa anapitia, magumu yale yameondoka na bidii yake kusoma Neno, yameondoka na bidii yake ya kuhudhuria ibada kanisani, yameondoka na bidii yake ya kuomba, yameondoka na bidii yake ya kumwimbia Bwana.

Shetani mjanja sana, anapoona akikupitisha kwenye eneo fulani zito alafu unaacha mambo mengi ya Mungu, anaona njia hiyo ni nzuri kwako kukuondoa kwenye kundi la wacha Mungu. Utashangaa tu hali ngumu uliyokuwa unapitia imeisha ila huna kiu tena na jambo lolote lile la kiMungu.

Kwa kifupi unakuwa umekaukiwa vibaya sana kiroho, kila ukijaribu kujisukuma urudi kwenye hali yako ya kawaida unaona kabisa inakuwa ni vigumu. Kutafuta tatizo ni nini unaweza usilione haraka ila ukweli upo wazi, wewe unapoguswa na ka changamoto kidogo unajipa likizo kwa mambo ya Mungu, shetani anajua njia nzuri ya kukuondoa kwenye njia sahihi ni kukuletea majaribu magumu mfululizo.

Lakini yule ambaye pamoja na anapitia magumu kwenye maisha yake, unamwona bado anaendelea kung’ang’ana na Mungu, huwezi kujua ni muda gani anapitia magumu. Maana kama ni kanisani utamkuta kwenye mafundisho ya Neno la Mungu, kama kwenye kipindi cha maombi utamkuta, kama ni kusoma Neno la Mungu kila siku huwezi kumwona ameacha.

Unaweza kujiuliza huyu ndugu mbona maisha yake mazuri sana, ina maana yeye hana changamoto yeyote anayopitiaga kwenye maisha yake? Unaweza kufika mahali ukaanza kujiuliza hivyo kutokana na mtu yule kusimama kwenye kitu anachokifanya bila kurudi nyuma.

Kama ulikuwa msomaji wa Neno la Mungu, ukaacha kwa muda fulani mrefu, ukija kurudi kumuuliza vipi ndugu bado unasoma tu Neno la Mungu? Atakujibu ndio bado naendelea kusoma, tangu ulivyoniacha kipindi kile tunasoma pamoja hadi sasa nimemaliza Biblia nzima na sasa nimeanza tena upya kuisoma.

Moyoni unaweza ukawa unajiuliza huyu mtu ina maana yeye hakutanagi na changamoto yeyote kwenye maisha yake? Jibu ni kwamba anakutana nazo sana ila hajawahi kuziruhusu zimzuie kusoma Neno la Mungu kila siku, anaweza akawa katikati ya magumu mazito ila huwezi kumwona amepitisha siku bila kusoma na kutafakari Neno la Mungu.

Hili tunajifunza kwa watumishi wa Mungu Paulo na Sila, pamoja na kukutana na magumu kwenye huduma yao ya kumhubiri Yesu Kristo. Pamoja na kupigwa fimbo nyingi sana, baada ya hapo wakatupwa gerezani, watumishi hawa hawakujipa likizo ya kumsifu Mungu wao, hata wale wafungwa wenzao walitambua kabisa awamu hii tumeletewa watu wa Mungu.

Rejea: Na walipokwisha kuwapiga mapigo mengi, wakawatupa gerezani, wakamwamuru mlinzi wa gereza awalinde sana. Naye akiisha kupata amri hii akawatupa katika chumba cha ndani, akawafunga miguu kwa mkatale. Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. MDO 16:23‭-‬25 SUV.

Ni rahisi sana kusoma hiyo mistari niliyokupa hapo juu, ukaona ilikuwa habari ya kawaida kabisa au ukaona ilikuwa ni zamani hizo ila sio sasa. Lakini nikuambie Neno la Mungu ni mwongozo sahihi kabisa wa maisha yetu wanadamu, hasa tulio na safari ya kwenda mbinguni.

Hapa inatuonesha pamoja na unaweza ukawa upo katikati ya majaribu mazito, hupaswi kuacha kumtukuza Mungu wako, badala yake unapaswa kuendelea na bidii yako ile ile. Katikati ya gereza Paulo na Sila wakapafanya sehemu ya ibada, wakamwinua Mungu wao kwa nyimbo na maombi.

Wakati wewe ukiguswa na kajaribu kidogo siku hiyo unalala bila hata kuomba,  acha lile la kusoma Neno la Mungu na kupata muda wa kutafakari yale uliyojifunza. Paulo na Sila wao hawakuangalia maumivu ya fimbo walizochapwa, wala hawakuangalia kwanini Mungu hawakuwatetea hadi wakipigwa fimbo nyingi kiasi hicho bila kosa lolote, lakini usiku wa manane walimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu.

Mwisho tunaona Mungu aliwatoa gerezani, ambapo leo unaweza usiwe gereza la segerea au gereza lolote unalolifahamu Tanzania, ukawa kwenye gereza la mahusiano yako ya uchumba, ukawa kwenye gereza la ndoa yako, ukawa kwenye gereza la uchumi, ukawa kwenye gereza la masomo yako, ukawa kwenye gereza la huduma yako.

Unapaswa kuendelea kumwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, utashangaa Mungu atakavyokutoa kwa kishindo kwenye hilo gereza ulilofungwa humo ndani. Hakuna atakayeamini umetokaje, hata wewe utaona kama ndoto, lakini itakuwa sio ndoto ni uhalisia kabisa Mungu amekutoa humo.

Uliacha kusoma Neno la Mungu kwa sababu ulikuwa unapita kwenye magumu fulani? Nakusihi urudi kusoma Neno, pia nikualike kwenye kundi letu la wasap la kusoma Neno kila siku, tuma ujumbe wako wasap namba +255759808081 utapata maelekezo mengine ya kujiunga.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com