Tunaweza kugeuka washabaki wa injili ila tusiwe watu tunaotulia na kuyachunguza maandiko kila siku yanasemaje juu ya lile tunalolipinga au linasemaje juu ya lile tunalolikubali sisi.

Maana kulikubali kwetu jambo lolote lile linapaswa kuwa na uthibitisho wa Neno la Mungu, na kulikataa au kulipinga kwetu jambo lolote lile tunapaswa tuwe na maandiko matakatifu yanayotuthibitishia hilo tunaloliona halifai.

Tofauti iliyopo sasa tunaweza tukawa tunalikataa jambo fulani kwa hisia zetu tu, bila kuwa na maandiko yanayotufanya tulikatae hilo jambo. Na vile vile tunaweza tukawa tunalikubali sana jambo fulani bila kuwa na ushahidi wa Neno la Mungu.

Huwezi kusema tu nabii fulani, au mchungaji fulani, au mwalimu fulani, ni feki, kwa kigezo kipi hadi unasema ni feki? Lazima uwe na maandiko yanayokuthibitishia hilo. Wakati unasema mtu fulani hahubiri/hafundishi injili sahihi lazima uwe na uhakika na unachosema, na uhakika huo lazima utokane na Neno la Mungu.

Uhakika wako wa kusema nabii fulani au mchungaji fulani ni sahihi, hupaswi kutokana na miujiza anayofanya, maana hata shetani huwa ana miujiza yake. Uhakika wako unapaswa kuthibitishwa na Neno la Mungu, kwa kulisoma kila siku.

Mwongozo wetu ni neno, ni sawa na mchungaji wa kondoo au mbuzi au ng’ombe, kazi yake ni kutoa mifugo yake kuipeleka malishoni au kuiletea malisho. Inabaki kazi ya mifugo hiyo kula, ule mfugo ambao utabaki unaangalia tu majani, huo mfugo hutashiba.

Nasi kazi yetu ni kuchukua Neno la Mungu kulisoma ili liweze kushibisha mioyo yetu, tusipokuwa na utaratibu wa kukaa chini kujua maandiko matakatifu yanasemaje. Hatukaa tujue injili tunayohubiriwa ni sahihi au sio sahihi.

Ujue sio mpaka mtumishi anayekuhubiria awe wa shetani ndio akuhubirie injili feki, hata watumishi wa Mungu wanaweza kukulisha chakula kisicho sahihi. Ndio huenda yeye mwenyewe hana muda wa kusoma Neno la Mungu, akakutana na fundisho la Duniani huko akalichukua akizani linatokana na Neno la Mungu, kumbe halitokani na Neno la Mungu.

Kwa mfano huu msemo umeenea sana kwenye vinywa wa watu wengi, unasema hivi, HATA MUNGU ANASEMA TUJISAIDIE KWANZA NAYE ATATUSAIDIA. Hakuna andiko linasema hivyo ila wengi tunaona ni kweli Mungu anasema hivyo.

Ndio maana ni muhimu sana kujua maandiko yanasemaje, maana Neno la Mungu sio sayansi, wala sio historia, nikiwa na maana kwamba somo la historia linasema mwanadamu alitokana na NYANI. Lakini maandiko yanasema Mungu alimfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi.

Rejea: Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai. Mwanzo 2:7.

Unaweza kuona ni jinsi gani kuna utofauti mkubwa sana, lakini kama hutokuwa na muda wa kusoma Neno la Mungu utasema ni kweli binadamu wa kwanza alitokana na Nyani.

Uimara wetu na ujasiri wetu unatokana na Neno la Mungu, unapokuwa na ujasiri wa kusema huyu mtu sio sahihi, sio mawazo yako. Umeyachunguza maandiko matakatifu ukaona anachofundisha au anachohubiri hakitokani na Neno la Mungu.

Ndivyo walivyokuwa watu wa Beroya, hawa watu walikuwa ni wachunguzi wa maandiko, hawakuishia kusema fulani ni muongo, hawakujifungia kwenye kile wanachokiamini tu. Walikuwa wanasikiliza kisha kuyachunguza maandiko yanasemaje kuhusu kile walichokisikia au walichokifundishwa.

Rejea: Mara hao ndugu wakawapeleka Paulo na Sila usiku hata Beroya. Nao walipofika huko wakaingia katika sinagogi la Wayahudi. Watu hawa walikuwa waungwana kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa walilipokea lile neno kwa uelekevu wa moyo, wakayachunguza maandiko kila siku, waone kwamba mambo hayo ndivyo yalivyo. MDO 17:10‭-‬11 SUV.

Biblia inasema hawa watu walikuwa ni waungwana kuliko wale wa Thesalonike, Paulo na Sila hakuwapata shida kubwa sana kama waliyokutana nayo huko nyuma. Watu hawa Biblia inasema walikuwa waungwana, watu waliosikiliza kwanza kisha kuyachunguza maandiko yanasemaje kuhusu kile walichokisikia.

Sio wewe hujajua maandiko yanasemaje, unaishia kusema alichosema mtumishi huyu sio sahihi, una uhakika alichosema mtumishi sio sahihi au umekariri/umekaririshwa uongo na watu wenye chuki binafsi juu ya yule mtumishi wa Mungu.

Tunasoma watu hawa wa Beroya walivyoyachunguza maandiko wakaona ni kweli, hawakuishia kusema hawa watu wanahubiri kweli ya Mungu. Walichukua hatua ya kubadilika, kule kuamini kwao mwanzo kulibadilika na kuamua kufuata njia nyingine sahihi zaidi ya waliyoamini.

Rejea: Basi watu wengi miongoni mwao wakaamini, na wanawake wa Kiyunani wenye cheo, na wanaume si wachache. MDO 17:12 SUV.

Jiulize mwenyewe, ni mara ngapi umehubiriwa injili sahihi na baada ya kuhubiriwa ulienda kuyachunguza maandiko yanasemaje kuhusu kile umehubiriwa. Baada ya kujua kilichosemwa ni sahihi, na kile ulichokuwa unaamini mwanzo sio sahihi, umewahi kutoka mahali pasipo sahihi na kuingia mahali sahihi?

Au wewe umeshikilia imani yako uliyozaliwa ukakuta wazazi wako wanaiamini, au umeendelea na imani hiyo kwa sababu ulitoka dini nyingine ukahamia hiyo. Na hiyo dini uliyohamia imekulea sana hadi umefika hapo ulipo, unaogopa kutoka mahali hapo usije ukaonekana msaliti.

Kama upo mahali sio sahihi, lazima uchukue hatua nyingine ya kuifuata kweli, tunaona waberoya walivyoyachunguza maandiko na kuona ni kweli. Wakaamini ile injili iliyohubiriwa na Paulo na Sila, ambapo sio rahisi sana mtu kujua mahali alipokuwa hakuwa sahihi, akaamua kubadili mwelekeo.

Na wewe tamani kuwa miongoni mwa watu wanaopenda kuyajua maandiko matakatifu, soma Neno la Mungu kila siku. Na kama unaona ni jambo gumu kwako na unahitaji kuwa karibu na watu wanaopenda kusoma Neno kila siku, karibu kwenye kundi letu la wasap. Tuma ujumbe wako kwa wasap namba +255759808081.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com