Kila jambo la kiroho ambalo linaadhishwa, mengi sana watu hupata mafunuo ndani ya Neno la Mungu baada kusoma. Mambo mengi mazuri ya kumletea Mungu sifa na utukufu, sio kana kwamba watu huwa wanabuni tu, mengi huwa yanakuja baada ya kupata maarifa sahihi ya Neno la Mungu.

Neno la Mungu likikaa kwa wingi ndani ya mtu, mtu yule huwa na maono mazuri ya kuwafanya watu waendelee kumjua Mungu zaidi. Mbinu nyingi kiutendaji zinazotokea kwa watu, ni baada ya kupata mafundisho ya kutosha au baada ya kupata maarifa sahihi ya Neno la Mungu.

Ukiona mtu fulani aliyeokoka anakuwa na ubunifu fulani wa kipekee, ubunifu ambao unamzalia Bwana matunda mema, usifikiri huo ubunifu unakuja tu au usifikiri amezaliwa nao. Ubunifu huo anaupata kadri anavyojibidiisha kuliweka moyoni mwake Neno la Mungu.

Watu wengine wanaweza wasimwelewe sana mwanzoni ila kwa kuwa ni jambo linalomletea Mungu sifa na utukufu, baadaye watu wale wanakuja kumwelewa vizuri. Japo hapo mwanzoni alionekana kama mtu anayefanya vitu visivyoeleweka sana.

Vipo vitu vingi sana ambavyo tunaviiga kutoka mahali fulani na kuvifanya vya kwetu, hii ni kutokana na kuonekana hivyo vitu ni vizuri, na vimekuza huduma za watu wengi. Sio vibaya kuiga mambo mazuri na kuyafanya ya kwetu kama hayo mambo yana matokeo mazuri baada ya kuyafanya.

Lakini tukiwa kama wanafunzi wa Yesu Kristo, tunapaswa kujikita kwenye Neno la Mungu kujua maandiko matakatifu yanasemaje kuhusu kile tunafanya. Tunapojua jambo fulani tunalofanya maandiko yanasemaje, tunakuwa na ujasiri na nguvu kubwa ya kufanya hilo jambo.

Yapo mambo ya kiMungu hatufanyi kwa moyo wote, tunafanya imradi tuonekane na sisi tumefanya, hii ni kwa sababu hatujui tunayoyafanya/tunalofanya lipo kimaandiko ama la.

Changamoto nyingine ipo kwa baadhi ya watu, hawawezi kulikubali jambo haraka mpaka wajue Neno la Mungu linasemaje, sio vibaya, wapo sahihi kabisa. Watu kama hawa ukiwaambia wafanye jambo fulani bila wao kujua maandiko yanasemaje, hilo jambo hawatalifanya katika ufanisi mzuri.

Ushuhudiaji wa nyumba kwa nyumba, umeanza kufanyika siku nyingi kidogo, hasa tunapokuwa na mikutano ya injili, huwa tuna utaratibu wa kuingia nyumba kwa nyumba kuwaeleza watu habari za Yesu Kristo.

Pamoja na kufanya hilo, huenda hukuwahi kujua kama hili jambo lipo kibiblia, ulikuwa unachukulia kama jambo fulani la kimazoea. Na kwa kuwa ulikuwa hujui kama lipo kimaandiko, ulikuwa unafanya kama utaratibu wa dini/dhehebu lako.

Leo nataka nikuonyeshe kuwa hili jambo lipo kibiblia, ili wakati unaenda kushuhudia habari za Yesu Kristo nyumba kwa nyumba uwe unajua unafanya nini.

Rejea: Ya kuwa sikujiepusha katika kuwatangazia neno lo lote liwezalo kuwafaa bali naliwafundisha waziwazi, na nyumba kwa nyumba, nikiwashuhudia Wayahudi na Wayunani wamtubie Mungu, na kumwamini Bwana wetu Yesu Kristo. MDO 20:20‭-‬21 SUV.

Nataka utazame hayo maneno ya “nyumba kwa nyumba”, kuingia nyumbani mwa mtu na kuanza kumfundisha Neno la Mungu aweze kusadiki habari za Yesu Kristo. Sio jambo jambo ambalo limebuniwa na mchungaji wako, ni jambo ambalo lipo kibiblia/kimaandiko.

Kama ulikuwa unafanya hili jambo kama maagizo ya mchungaji wako, au Askofu wako, au mzee wako wa kanisa, kuanzia sasa ona hili jambo lipo kibiblia, kama lipo kibiblia unapaswa kulifanya kwa moyo wako wote, na nguvu zako zote, ukijua unamfanyia Bwana na si mwanadamu mwenzako.

Mtume Paulo alihubiri injili ya nje, na aliingia nyumba kwa nyumba kuwashuhudia Wayahudi na Wayunani habari za Yesu Kristo. Wapo walioamini, na wapo waliokataa kuamini.

Unapoona watu wanakazana kuingia nyumba kwa nyumba kutangaza habari za Yesu Kristo, usifikiri wamekosa kazi ya kufanya, wala usifikiri wanajisumbua tu bure. Kuanzia sasa ujue wapo kazini, wapo shambani mwa Bwana wanamtumikia.

Kuyajua haya yote ni mpaka uwe msomaji wa Neno la Mungu, soma Neno la Mungu kila siku hatua kwa hatua, sura kwa sura, utapata maarifa mazuri ya kukufanya uifanye kazi ya Mungu kwa ufanisi. Kama unapenda kuungana na wenzako wanaosoma Neno kila siku, tuwasiliane kwa wasap namba +255759808081.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com