Kama umekuwa makini katika maisha yako, kuna mambo mazuri uliwahi kuwa na msukumo nayo ndani ya moyo wako ila ulishindwa kutimiza nia ya moyo wako, kutokana na kuanza kupewa hadithi mbaya juu ya kile ulichokuwa unataka kukifanya.

Yapo mambo yana hatari sana kwenye maisha yetu ila pamoja na yana hatari, Mungu anakuwa ameweka wito ndani yetu kuyafanya, haijalishi kuna mitego mingi imewekwa ili kutuangamiza pale tutapothubutu kufanya kile ambacho watu hawataki tukifanye.

Mungu akiweka mzigo ndani mwa mtu wake kwa jambo ambalo anajua lina vita kubwa, huwa anajua kabisa, na kama hajamwambia mtu wake acha anapaswa kuendelea kutumika bila kujalisha kuna mitego gani imeandaliwa kwa ajili yake.

Hili linaweza likawa jambo gumu sana kwa watu wengi, pamoja na ugumu linaweza likawa jambo gumu zaidi kama wale wanaotupa tahadhari na wao ni watu ambao wamejaa nguvu za Roho Mtakatifu. Ambao Roho Mtakatifu anasema nao mambo ambayo yatawapata wale wanaomtumikia Yesu Kristo kwenye kusudi lile aliloweka ndani yao.

Ukiwa kama mtumishi wa Mungu, unaweza kuletewa taarifa mbaya za kuhusu usalama wa maisha yako, na taarifa ulizoletewa sio kana kwamba ni za kukutisha tu ili uache ile huduma uliyokuwa unaifanya, hapana, ni taarifa sahihi kabisa kuwa watu wameandaa mpango wa kukumaliza au kukufunga.

Watu wanaokupenda na wanaojua umhimu wako hawawezi kukuacha uangamie kizembe hivyo, watakupigia makelele mengi usiende huko ambapo watu wamejiandaa kukushika, na watafanya mengi kukuonyesha kuwa hicho ulichodhamiria kwenda kukifanya hupaswi kwenda.

Kama na wewe husikilizi Roho Mtakatifu anasemaje ndani yako, utajawa na hofu nyingi, na utashindwa kufanya kile ambacho Mungu alikutuma ukifanye. Mungu anaweza kusema nawe kuhusu mambo utakayoenda kukutana nayo kwenye huduma yako ila asikuambie usiende, utaenda ukiwa tayari unajua mambo magumu utakayopata.

Muda mwingine Mungu anaweza asiseme na wewe kabisa kuhusu mambo yatakayoenda kukuta wakati ukifanya kazi ya injili. Ukaenda kimya kimya, baada ya kufika kwenye eneo la tukio unakutana na changamoto kiasi kwamba unajiuliza kwanini iwe hivyo kwako.

Kufungwa kwako rohoni usijiue yatakayokukuta au Mungu kutokusema na wewe, sio kiashiria kwamba usiende huko ambapo ulitakiwa kwenda, unapaswa kwenda hivyo hivyo.

Rejea: Basi sasa, angalieni, nashika njia kwenda Yerusalemu hali nimefungwa rohoni, nisiyajue mambo yatakayonikuta huko; isipokuwa Roho Mtakatifu mji kwa mji hunishuhudia akisema, ya kwamba vifungo na dhiki vyaningoja. MDO 20:22‭-‬23 SUV.

Unaona hapo ndugu yangu, mtume Paulo anasema anaenda Yerusalemu hali amefungwa rohoni asiyajue mambo yatakayomkuta huko. Anasema hivyo kwa sababu alizoea kuwa Roho Mtakatifu alikuwa anasema naye kuhusu mahali ambapo angeenda kutangaza habari njema za Yesu Kristo.

Mambo ya kiMungu unapaswa uwe makini sana, unaweza kuletewa taarifa mbaya zenye lengo za kukuondoa kwenye msimamo wako wa kuisimamia kweli ya Mungu. Usipomsikiliza/usipomtii Roho Mtakatifu unaweza kujikuta unatoka kwenye msimamo wako.

Tuna wazazi wetu, wake zetu, waume zetu, watoto wetu, walezi wetu, marafiki zetu, ndugu zetu, washirika wetu, hawa wakiona kitu ambacho sicho kizuri usifikiri watakuacha hivi hivi. Lazima watahakikisha wanakuzuia kabisa usifanye hicho ulichokusudia kukifanya, wapo wengine watasimama mbele yako kukuzuia usiende kwenye huduma.

Wakati wewe ukijitazama ndani yako unajiona upo tayari kwa lolote kwa ajili ya jina la Yesu Kristo, ujasiri upo mkubwa ndani yako, na unasikia msukumo wa Roho Mtakatifu kwenda kuhubiri mahali ambapo watu wengine wanapaogopa.

Rejea: Basi tuliposikia haya, sisi na watu wa mahali pale, tukamsihi asipande kwenda Yerusalemu. Ndipo Paulo alipojibu, Mnafanya nini, kulia na kunivunja moyo? Kwa maana mimi, licha ya kufungwa, ni tayari hata kuuawa katika Yerusalemu kwa ajili ya jina lake Bwana Yesu. MDO 21:12‭-‬13 SUV.

Ndugu yangu, watu wakishajua huko uendako yanaenda kukuta mabaya, ulipo panaweza kugeuka msiba ghafla kutokana na kelele za vilio vingi wa watu. Vilio ambavyo vinakusihi usifanye hicho unachotaka kufanya, ama usiende huko unapotaka kwenda.

Utachagua mwenyewe, maana ni wakati ambao unaweza kujawa na huruma vile unaona ndugu na jamaa wanalia kwa ajili yako, ukaona bora kuachana na huduma aliyokupa Mungu ndani yako. Lazima ujue kumsikiliza Roho Mtakatifu, maana nyakati kama hizi zinaweza kutukuta mahali ambapo hatukupanga.

Paulo hakukubali kuwasikiliza watu wale, badala yake aliwajibu yupo tayari kuuawa kwa ajili ya jina la Yesu Kristo. Ni ujasiri mkubwa sana ambao tunapaswa kujifunza kwa mtumishi wa Mungu huyu, maana katika huduma tunaweza kukutana na mazingira kama haya.

Rejea: Alipokataa shauri letu, tukanyamaza tukisema, Mapenzi ya Bwana na yatendeke. MDO 21:14 SUV.

Hawa watu walikuwa wana Roho wa Mungu ndani yao, unaona hekima waliyokuwa nayo, walivyoona ushauri wao hakukubaliwa, walinyamaza kimya na kusema mapenzi ya Mungu yatendeke.

Sasa unaweza kukutana na watu ambao hawana hekima kama hawa aliokutana nao Paulo, wenyewe wakawa wanajua mazingira yale kwa kuyafahamu kwa macho au kwa kusikia habari zake. Uwe na uhakika ukikataa ushauri wao, watakupia maneno magumu.

Neno la Mungu linapaswa kuwa ndani yako kwa wingi, unaweza kukutana na mazingira kama haya ya Paulo, ukazuiwa na Roho Mtakatifu kufanya huduma. Kwa kuwa huna neno la Mungu la kutosha, ukashindana na Roho Mtakatifu ukafanya lile alilokuzuia kwa kusema hata mtume Paulo alikutana na hili, lakini hakuogopa.

Soma sana Neno la Mungu upate maarifa mazuri kama haya, kama hili limekuwa changamoto ngumu kwako, karibu sana kwenye kundi letu la wasap la kusoma Neno la Mungu kila siku. Tuma ujumbe wako kwa wasap namba +255759808081.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com