Kimbilio lako ni lipi ndugu yangu, nakuuliza hivi kwa sababu kuna watu wengine wakiwa wanapita kwenye mambo magumu. Wanajitenga na mambo ya Mungu ambaye anaweza kuwasaidia kwenye shida zao, ndio wanajitenga naye mbali.

Nyakati za kupita kwenye majaribu/changamoto, ni wakati ambao unakuwa mgumu sana, mambo mengi unaweza kuona hayana hamu ya kufanya. Lakini pamoja na magumu unayopitia hupaswi kujitenga na kazi ya Mungu au mambo ya Mungu.

Kama ulikuwa una huduma ambayo watu walikuwa wanajifunza vitu vizuri vya kuwajenga kiroho kutoka kwako, hupaswi kujipa likizo kwa sababu upo kwenye wakati mgumu unapitia. Kimbilio lako ni Yesu Kristo, ukijitenga naye unafikiri utapona kwenye gumu lako unalopitia?

Unaweza kuona ni jinsi gani ni hupaswi kujipa likizo, wakati mgumu ndio wakati wa kukaa katika uwepo wa Mungu zaidi, mafundisho ya Neno la Mungu hayapaswi kupungua kwako, kusoma Neno la Mungu hakupaswi kupungua kwako.

Hakupaswi kupungua kwa sababu ndilo kimbilio lako la pekee la kuweza kukutoa salama kwenye jaribu ngumu linalokukabilii kwa wakati huo. Usipokuwa makini shetani atatumia nafasi ya magumu unayopitia kukuondoa kabisa kwenye njia sahihi ya Mungu.

Utashangaa jaribu ngumu ulilokuwa unapitia linaisha na hali yako ya kiroho inashuka chini kabisa, ulikuwa mwombaji mzuri ukawa huwezi kuomba tena, ulikuwa mtu unayependa mafundisho ya Neno la Mungu ukawa hupendi tena, ulikuwa msomaji mzuri wa Neno la Mungu ukawa hujisikii tena kutulia mbele za Mungu kusoma Neno.

Sijui wakati gani unapitia hapo ulipo, unajua mwenyewe ni gumu gani unapitia, linaweza lisijulikane sana na watu ila wewe unajua mzigo mzito ulionao ndani ya moyo wako. Kama hutokuwa makini ukaanza kuona unakuwa mzito kwa mambo ya Mungu, ujue anguko lako li karibu.

Hupaswi kuona mambo ya Mungu hayafai, maana ndio kimbilio lako pekee katika maisha yako, watu wanaweza kukukimbia wote kwenye shida yako, watu wote wanaweza kukuacha kwenye shida yako ila Mungu hawezi kukuacha kwenye shida yako.

Watu wanaweza kukuacha kwenye ugonjwa wako, lakini Mungu hawezi kukuacha, atakuwa na wewe wakati wote, sasa kwanini wewe unapokutana na changamoto kidogo unaamua kujiweka pembeni na mambo ya Mungu?

Rejea: Nimekukimbilia Wewe, BWANA, Nisiaibike milele. Kwa haki yako uniponye. ZAB. 31:1 SUV.

Kimbilio lako ni lipi? Kama kimbilio lako ni kwa BWANA, kwanini unatamani kuacha kusoma Neno la Mungu? Kwanini umeacha kusoma Neno la Mungu? Kwanini umeacha kwenda kanisani? Kwanini umeacha maombi? Kwanini ule upendo wako kwa Mungu umepungua?

Ulikuwa mwimbaji mzuri umeacha kumwimbia Mungu, ulikuwa msomaji mzuri wa Neno la Mungu umeacha kusoma Neno, ulikuwa mwalimu mzuri wa Neno la Mungu siku hizi umeacha kufundisha, ulikuwa mwinjilisti mzuri sana lakini sasa hivi umepoa kabisa.

Una mpango gani, kwanini ulemewe na mizigo wakati yupo wa kumtwisha mizigo yako, kwanini uchoke wakati wa kumkimbilia yupo? Anaweza kukuponya majeraha ya moyo wako, anaweza kukusaidia usiaibike.

Tena hutaibike milele, hata kama watu walisema sasa unaenda kupoteza kila kitu kwenye maisha yako, wakati wanafikiri hivyo, Yesu Kristo atawashangaza pale waliposubiri uaibike badala yake ukainuliwa juu zaidi.

Usiache kusoma Neno la Mungu kwa sababu ya magumu yamekupata, ukifika mahali hujisikii kabisa kusoma Neno la Mungu, jikumbushe kimbilio lako lipo kwa nani? Tumejifunza lipo kwa BWANA, kama lipo kwa Bwana sasa kwanini ukose kiu ya kuendelea kuutafuta uso wake kwa bidii bila kujalisha hali unayopitia.

Nikukaribishe uungane na wenzako wanaosoma Neno la Mungu kila siku kwa mtiririko mzuri, watu hawa wanapatikana kundi la wasap. Ili uweze kuungana nao, tuma ujumbe wako wasap wenye Neno CHAPEO YA WOKOVU kwa namba +255759808081.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com