Marafiki tulionao wana mchango mkubwa sana katika maisha yetu, yapo maeneo tumekwama kwa sababu ya marafiki tulionao. Na yapo maeneo tumefanikiwa sana kwa sababu ya kuambatana na marafiki wazuri.

Katika maisha yako sio kila mtu anaweza akawa rafiki yako, sio kila mtu wa kuambatana naye, wapo watu wanapaswa kubaki watu mnaoheshimiana na kushirikiana mambo ya kijamii tu ila sio kuwa marafiki zako.

Kuna watu husema kila mtu ni rafiki yangu, huo ni uongo, huwezi kuwa na urafiki na kila mtu, huwezi kuwa na undugu na kila mtu, labda urafiki jina tu ila sio ule urafiki wa ndani wa kuambatana kila wakati na kushirikishana baadhi ya mambo nyeti.

Unapaswa kuchagua watu wa kuambatana nao katika maisha yako, iwe kazini kwako unapaswa kuwa na watu wa kuambatana nao, iwe kwenye biashara yako unapaswa kuwa na marafiki wazuri wa kuambatana nao, iwe kwenye huduma yako unapaswa kuwa na marafiki wazuri.

Usiseme kila mtu ni wa Mungu, sawa watu wote ni wa Mungu ila maandiko matakatifu yanatuambia tukitembea na wenye hekima nasi tutakuwa na wenye hekima. Na yule mtu anayetembea/anayeenenda na marafiki wapumbavu atapata madhara.

Watu wote si wa Mungu? Kwanini Biblia inatuambia tuambatane na wenye hekima nasi tutapata hekima, na tukienenda na wapumbavu tutapata madhara. Alafu wewe unaona kila mtu wa kuambatana naye, unaambatana naye vizuri sawa lakini baada ya muda unashangaa unaanza kuwa na tabia fulani mbaya.

Rejea: Enenda pamoja na wenye hekima, nawe utakuwa na hekima; Bali rafiki wa wapumbavu ataumia. MIT. 13:20 SUV.

Hekima haipatikani kwa kila mtu, wapo watu ambao wanamcha Mungu katika roho na kweli na wenye Neno la Mungu ndani yao, ndio waliopata neema hii ya kuwa na hekima ndani yao. Watu ambao huwezi kuwakuta wakiongea ujinga, watu ambao kila unapoongea nao wakusihi kuenenda katika njia sahihi.

Tofauti kabisa na wapumbavu, hawa watakupoteza kabisa, wala hupaswi kuambatana nao hata kidogo, maana ukiambatana nao watakuambukiza tabia mbaya.

Unataka kuwa mtu fulani au una maono ya kuwa mtu fulani, ambatana na wenye hekima, ukiambatana na wapumbavu utaishia kupata hasara. Watakujaza maneno yasiyofaa, au vile wanavyoenenda wao nawe utaanza kuendana vivyo hivyo.

Unataka kufanikiwa kwenye usomaji wako wa Neno la Mungu, ambatana na wenye hekima, ukitaka kufanikiwa kwenye uandishi wako wa makala bora, ambatana na wenye hekima. Watu wanaopenda kile wanafanya, wenye kujiheshimu, wanaomcha Mungu katika roho na kweli, wenye bidii, wanaojitoa kwa mambo ya Mungu, hao ndio wakuambatana nao.

Rafiki anao uwezo wa kukuambukiza tabia mbaya au nzuri, inategemeana na huyo rafiki yako ni wa namna gani, ndio maana unapaswa kuwa na uchaguzi mzuri wa marafiki.

Kijana chunga sana marafiki unaoambatana nao, marafiki hao wana mchango mkubwa sana kuharibu maisha yako, au wana mchango mkubwa sana wa kukufanya ukawa mtu mzuri unayeheshimika na watu.

Watu wanaojua hili jambo huwezi kuwakuta wanaambatana na kila mtu, awe kiongozi wa watu wengi, ana watu wake anaoambatana nao, sio kwa sababu ni kiongozi utamkuta anaambatana na kila mtu. Hapana, unapaswa kujua hili ili uweze kufanikiwa katika maisha yako ya kiroho na kimwili.

Huwezi kuwa unamwomba sana Mungu akupe hekima ndani yako, wakati marafiki ulionao ni wapumbavu, moja kwa moja wale marafiki unaokuwa nao ndio wanakufanya uonekane vile wao walivyo. Mpaka uwe rafiki na wapumbavu ujue kuna vitu unavipenda kutoka kwao, huwezi kuambatana na rafiki ambaye mnapishana.

Kuanzia sasa angalia marafiki ulionao ni wa namna gani, unaweza ukawa unalalamika unashindwa kufikia Lengo la kusoma Neno la Mungu kumbe marafiki ulionao ni wavivu wa kutupwa. Tena muda wote wanapokuona unasoma Neno la Mungu wanakutupia maneno ya kukuvunja moyo, na mengine ya kukukashifu kabisa.

Wakati mwingine unaona ili usiendelee kuwakasirisha unaona bora uwasikilize, kuwasikiliza huko ndio unajikuta unarudi nyuma kwa kile ulichoanza kukifanya.

Kuna tabia mpya na nzuri ulianza kuijenga kwako, na unatumia nguvu kubwa unajikuta unakwama, Roho Mtakatifu amekusemesha mara nyingi uachane na hao marafiki wewe umekuwa umewang’ang’ania tu. Hujui wanaokuangusha na kukurudisha nyuma ni hao marafiki zako, kila ukijaribu kupiga hatua wao wanakuvuta nyuma.

Siku ya leo nakusihi sana uambatane na wenye hekima ili na wewe uwe na hekima, sitaki kurudia sana kuhusu madhara ya kuambatana na marafiki wapumbavu. Maandiko yamesema kuna madhara sio faida, shika hilo litakusaidia.

Enenda na wenzako wanaosoma Neno la Mungu kila siku, ili nawe uwe msomaji mzuri wa Neno la Mungu, watu hawa wanapatikana kundi la wasap la Chapeo Ya Wokovu. Unataka kuungana nao, tuma ujumbe wasap wenye maneno CHAPEO YA WOKOVU kwa namba +255759808081, utapata maelekezo mengine ya kujiunga.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com