Unapopatwa na shida yeyote ile kubwa yenye kuhatarisha uhai wako, watu wanapokuja kwako au wengine wanaposikia umepatwa na shida hiyo. Sio wote watakuwa wanakuhurumia na kukuombea upone, wapo wanasubiri kukuona/kusikia umekufa.

Wakati wewe unasema umesimama na Mungu, na wakati una imani kuwa unapita salama kwenye jaribu gumu ulilonalo, wapo watu wanajua huponi kwenye jaribu lililokupata.

Wapo watu wanaweza kusikia umepata ajali mbaya, kukimbilia kwao kuja kukuona kwenye ajali hiyo mbaya uliyopata, na wengine kutega kwao masikio kuhusu ajali uliyopata. Wanatamani kusikia au kukuona umekufa kabisa, na sio umepona.

Muda mwingine mambo tunayofanya huwa vigumu kueleweka kwa watu wengi, hasa tunapokuwa kwenye njia sahihi, hasa tunapokuwa tumesimama vizuri na Mungu, hasa tunapokuwa tunamhuhiri Yesu Kristo.

Mambo hayo hutufunya tuchukiwe na watu, sio kuchukiwa tu na kuishia hapo, tunapopatwa na shida yeyote ile, iwe kuumwa, iwe kupatwa na jambo fulani gumu. Watu hao husubiri kusikia hayo yaliyotupata yametuondoa kabisa uhai wetu.

Wapo wengine kwa sababu tunaenda kinyume na mapokeo yao ya imani, vile tunavyomhubiri Yesu Kristo na wale watu waliokuwa upande wao wanakuja kumwamini Yesu. Wanaona wanazidi kukimbilia upande ambao unafundisha habari za Yesu Kristo, usifikiri watu wale wanakufurahia na kukupenda, siku umepatwa na shida watatega masikio yao kusubiri ufe.

Pamoja na kutuwazia mabaya au kuwawazia watu mabaya wasio na hatia yeyote, watu wale wale hushangaa pale unapotoka mzima au wale waliotarajia utakufa kutokana na jambo lililokupata. Badala yake wanakuona unatoka salama kwenye shida/tatizo/jaribu lililokupata.

Unapotoka salama lazima watabadilisha maneno, mwanzo walisema lazima ufe kutokana na shida uliyopata, na wanajua kutokana na historia za nyuma hakuna mtu aliyewahi kupona alipopatwa na hilo tatizo. Pale wanapokuona umepona wataanza kukuona wewe sio mtu wa kawaida, watakupa jina lingine.

Hili tunajifunza kwa mtumishi wa Mungu Paulo, wakati Paulo anakabiliana na nyoka, watu waliokuwa karibu yake walikuwa na uhakika ile nyoka itamuua. Na wakawa wanamsema Paulo ni mtu mwuaji, wakaendelea kusema kuwa pamoja na mtume Paulo kuponea kumezwa na bahari, wakawa na uhakika kwa yule nyoka hataweza kupona.

Rejea: Paulo alipokuwa amekusanya mzigo wa kuni, na kuuweka motoni, nyoka akatoka kwa ajili ya ule moto akamzonga-zonga mkononi. Wenyeji walipomwona yule nyoka akilewa-lewa mkononi, wakaambiana, Hakosi mtu huyu ni mwuaji; ambaye ijapokuwa ameokoka katika bahari haki haimwachi kuishi. Wao wakadhani ya kuwa atavimba au kuanguka chini kwa kufa ghafula; na wakiisha kumwangalia sana, na kuona kwamba halimpati dhara lo lote, wakageuka, wakasema kwamba yeye ni mungu. MDO 28:3‭-‬4‭, ‬6 SUV.

Baada ya kuona lile walilolisubiri kwa Paulo limeshindwa kutimia, walibadilisha maneno na kusema kwamba Paulo ni mungu. Maana yake kile kitendo cha kupona kung’atwa na yule nyoka, kilikuwa ni kitendo ambacho hakikuwa cha kawaida.

Kwa mazingira ya kawaida kabisa, hebu fikiri umezongwa mwilini mwako na nyoka mwenye sumu kali, fikiria nyoka yeyote yule unayemfahamu mwenye sumu kali. Ambaye umesikia habari zake mbaya, alafu ukawa umepona kuawawa na huyo nyoka mwenye sumu kali.

Labda huo mfano wa nyoka unaweza ukawa mgumu kwako kutokana na mazingira uliyokulia, nikufikirishe kwenye kuumwa. Chukulia umepatwa na ugonjwa mbaya, ugonjwa ambao kila mtu ana uhakika hutopona kabisa, alafu ukawa umepona. Lazima watu wajiulize wewe ni mtu wa namna gani, kama walikuwa wanakuchukilia kawaida lazima mtazamo wao ubadilike.

Kama walikuwa hawataki kusadiki kuwa una Mungu wa kweli, ndio siku watakayosema hakika huyu mtu ameokoka, hakika huyu ana Yesu Kristo ndani yake. Kule kudhauriwa kwako, huondoka na kuja heshima kubwa kwako.

Hii inatufundisha mambo mengi sana, mojawapo ni pale tunapopatwa na jaribu gumu, tunapotulia kwa Bwana mwisho wake hutupa heshima badala ya aibu. Wakati watu wanasubiri ukate roho kupitia shida iliyokupata, kupitia shida hiyo ndio itakupa heshima ambayo ilikuwa haipo kwako kwa watu.

Usiogope matisho ya watu, watakuja na maneno magumu ya kukuambia hili ulilolipata hakuna aliyewahi kupona. Ukiwa na Yesu Kristo moyoni, na imani yako ikawa imara, utatoka salama na Yesu wako atatukuzwa kupitia lile lile tatizo lilokufanya watu wakae chini kusubiri ukate roho.

Maarifa ndio yanamfanya mtu awe na imani mbele za Mungu, na maarifa haya yanapatikana ndani ya Neno la Mungu. Hakikisha unasoma Neno la Mungu kila siku, una changamoto kwa hili la kusoma Neno kila siku, karibu kwenye kundi letu la wasap la kusoma Neno. Tuma sms yako kwa wasap namba +255759808081 utaunganishwa baada ya kupewa taratibu za kundi.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com