
Vipo vitu ukiambiwa ndio chanzo cha kitu fulani kuwa vile kilivyo, unaweza usiamini kabisa na ukakataa kabisa kutokana na kitu chenyewe kilivyo. Labda tangu ujue sifa ya hicho kitu kikubwa, hukuwahi kufikiri kama kimetokana na kitu ambacho wengi hawakichukulii sana maanani.
Na siku zote ukishajua hichi kikubwa unachokiona kimetokana na kitu ambacho ulikuwa unakichukilia kawaida, lazima utaanza kujenga heshima ndani yako kwa hicho kitu. Utaanza kuona hata wewe mwenyewe unaanza kuwaambia watu wengine kuwa hicho mnachokipuuza kimezaa kitu fulani kikubwa sana.
Sawa na mzazi anaweza akaonekane wa kawaida sana kutokana na mazingira aliyonayo, kama ana watoto wazuri wenye nafasi fulani kubwa serikalini au wana huduma fulani kubwa. Utasikia watu wakisema huyu mama msimwone yuko hivi, watoto wake wana nafasi fulani kubwa serikalini au ni mama wa mtumishi fulani maarufu.
Watu wakishaanza kusikia hivyo, ghafla utaona wale waliokuwa wanamchukulia yule mama kawaida, wataanza kumchukulia kwa namna ya tofauti kabisa. Sio kwamba huyo mama amebadilika, hapana, kilichobadilika ndani yao ni vile wamejua huyo mama ana watoto wanaoheshimika kutokana na nafasi zao.
Sio wote tunaweza kulipokea jambo kwa namna ya kuheshimu, wengine tunaweza kulipokea jambo kwa namna ya dharau. Kutokana na kutojua umhimu au uthamani wa kile kitu ambacho kinasemwa na watu, tunaweza kukichukulia kawaida sana ila wale wanaojua uthamani wake watakichukulia kwa namna ya pekee sana.
Ndio maana wapo watu wanadharau mama zao, inawezekana kabisa kudharau kwao mama zao ni kwa sababu ya ujinga ulio ndani yao. Nasema hivyo kwa sababu mtu yule yule aliyekuwa anamdharau mama yake, akishajua umhimu wa mama, utamwona anabadilika ghafla na kuwa mtu mzuri.
Wakati huo anaweza akawa amejua umhimu wa mama, ikiwa tayari mama yake hayupo tena duniani, utashangaa mtu huyu huyu aliyekuwa anamdharau sana mama yake, mtu huyu huyu aliyekuwa anawachukulia akina mama kawaida. Atageuka kuwa mwalimu mzuri wa kuwafundisha wengine umhimu na uzuri wa mama.
Yupo mtu mwingine unamwona wa kawaida sana kutokana na mwenekano wake, yule yule mtu ukaja kuambiwa ni mtu fulani mwenye nafasi fulani kubwa. Utaanza kumwona kwa namna ya tofauti, lakini muda mchache uliopita ulikuwa unamwona mtu wa kawaida sana.
Kila siku tunasikia watumishi wa Mungu wakisisitiza umhimu wa kusoma Neno la Mungu, lakini wengi wetu bado tunalichukulia Neno la Mungu kama kitu cha kawaida sana. Nasema tunakichukulia kitu cha kawaida kwa sababu huwezi kumkuta mtu anaumia kiasi kwamba anakosa hamu ya kula kwa ajili ya siku ilipita bila kusoma Neno la Mungu.
Mtu yule yule anaweza kuumia sana kwa sababu timu yake ya mpira imefungwa, lakini huwezi kumkuta akiumia kwa sababu ana wiki/mwezi mzima hajasoma Neno la Mungu, mwingine hakumbuki mwaka gani alisoma Neno la Mungu zaidi ya kubeba Biblia siku za jumapili.
Sasa leo nataka kukufahamisha kwamba kile ambacho ulikuwa unakichukulia kawaida, kile ambacho ulikuwa huoni umhimu wake sana pamoja na kusikia sana habari zake. Hicho ndicho kilichosababisha ulimwengu huu uonekane hivi ulivyo, vyote vinavyoonekana na visivyoonekana viliumbwa na kwa Neno la Mungu.
Neno la Mungu unalolidharau au unalolichukulia kawaida au unalolipuuza na kuliona la kawaida sana, usome usisome unaona kawaida tu, ulijue usilijue unaona kawaida tu, uwe na Biblia usiwe nayo unaona sawa tu.
Fahamu kwamba hilo ndilo limeumba ulimwengu huu, ikiwa Neno la Mungu limeumba ulimwengu huu unaonekana na usioonekana, hebu tafakari unaweza kufahamu namna ya kuenenda sawasawa na mapenzi ya Mungu pasipo kulijua Neno la Mungu? Haiwezekani.
Rejea: Kwa imani twafahamu ya kuwa ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, hata vitu vinavyoonekana havikufanywa kwa vitu vilivyo dhahiri. EBR. 11:3 SUV.
Kama ni kuwekeza muda wako mwingi kwenye kupata maarifa sahihi, unapaswa kuwekeza muda wako mwingi kwenye Neno la Mungu. Maana vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana kwenye ulimwengu havikufanywa kwa vitu vilivyo dhahiri bali kwa Neno la Mungu.
Kwa namna nyingine tunaweza kusema kwamba ulimwengu wote umetokana na Neno la Mungu, kilichosababisha ulimwengu huu uonekane au uwepo ni Neno la Mungu.
Kwahiyo vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana kwa macho ya nyama kwenye ulimwengu huu vimetokana na Neno la Mungu, Neno la Mungu ndio chanzo cha mambo yote mazuri yanayoonekana na yasiyoonekana.
Wanyama wazuri unaowaona leo walifanyika kwa Neno la Mungu, ndege wazuri na wanaovutia sana walifanyika kwa Neno la Mungu, hewa nzuri unayoifurahia leo ilifanyika kwa Neno la Mungu, na vyote unavyoviona na usivyoviona, na vyote unavyovijua na usivyovijua viliumbwa kwa Neno la Mungu.
Rejea: Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake. Wakolosai 1:16.
Neno la Mungu ambalo unaliona la kawaida kabisa, huna muda nalo, usipolisoma wala hushtuki, siku ikipita bila kulisoma wala huumii, hujawahi kusoma kwa mtiririko mzuri hata kitabu kimoja ndani ya Biblia ukamaliza. Lakini una amani ya kutosha, lakini unashinda kwenye mitandao ya kijamii kwa muda wa kutosha au unakaa tu.
Mtu akikugusa kuhusu kusoma Neno la Mungu unakuwa tayari umeshaandaa sababu nyingi sana, lakini ukija kwenye ukweli unakuwa na muda mwingi sana kwa siku unaupoteza kwa vitu ambavyo havina umhimu wowote kwenye maisha yako ya kiroho.
Baada ya kufahamu ulimwengu huu umeumbwa kwa Neno la Mungu, nini ndani yako imejengeka siku ya leo, najua umeambiwa sana usome Neno la Mungu. Leo mimi nakwambia bila Neno la Mungu kuishinda dhambi ni ngumu kwako, maana yake ni kitu usichoweza kukishinda bila Neno la Mungu.
Ulimwengu huu umeumbwa kwa Neno la Mungu, kwahiyo unapaswa kulifahamu vizuri Neno la Mungu ili uweze kuendana nao. Bila kulifahamu vizuri Neno la Mungu utashindwa kumpendeza Mungu wako, kitabu cha maelekezo ya namna ya kuenenda sawasawa katika ulimwengu huu unaonekana na usionekana ni Neno la Mungu.
Kama ulikuwa bado hujajiunga na kundi la wasap la kusoma Neno la Mungu kila siku, nakusihi uchukue hatua haraka sana kwa kutuma ujumbe wako kwa wasap namba +255759808081 utapatiwa maelekezo mengine ya kujiunga na kundi letu.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com