Mtu anapofanya jambo fulani, jambo hilo liwe zuri au liwe baya, mtu huyo anategemea kupata matokeo fulani ya utendaji wa hicho anachofanya. Matokeo yanaweza yakawa mazuri, au matokeo yanaweza yakawa mabaya ila lazima kitu anachofanya mtu kinakuwa na matokeo fulani.

Matokeo hayo mazuri au mabaya mtu huyo anaweza akawa anajua yatatokea hivyo, au anaweza akawa hajui kabisa kama yangeweza kutokea hayo aliyotokea baada ya kufanya jambo hilo.

Mambo mengi tunayofanya mara nyingi katika maisha yetu huwa hatupati matokeo mazuri kama tulivyotarajia tupate, ila yapo mambo tunayofanya yanajulikana mwisho wake yatazalisha matokeo gani.

Ubaya unaomtendea mtu mwingine hahitaji hadi uwe nabii ndio ujue, ubaya siku zote unaomfanyia mtu mwingine mwisho wake huwa mbaya. Hata kama unaona ni mzuri na una matokeo mazuri kwa upande wako, bado huwezi ukasema wewe ni mshindi kwa sababu ipo siku utavuna matunda ya ubaya wako.

Hicho unachofanya sasa unatarajia kupata faida ipi, au faida unayoipata sasa itakupa matokeo gani kwa maisha ya baadaye baada ya kuondoka hapa duniani. Hili ni muhimu sana kulitafakari mapema kabla hujaondoka duniani, uwe umeokoka au uwe hujaokoka, ni muhimu sana kujiuliza hili.

Bila kusubiri watumishi waje wakuambie hiyo tabia unayofanya sio nzuri, jiulize hayo mambo unayofanya yamekupa faida gani ya kiroho tangu umeanza kufanya. Yanazidi kukuimrisha zaidi kiroho au yamekuua kabisa kiroho.

Yanakufanya uzidi kuimarika kiroho na kimwili au yanakufanya upoteze kabisa uhusiano wako na Mungu, jibu unalo, kama yanakufanya uimarike zaidi au kama yanakufanya upoteze zaidi uhusiano wako na Mungu.

Rejea: Ni faida gani basi mliyopata siku zile kwa mambo hayo mnayoyatahayarikia sasa? Kwa maana mwisho wa mambo hayo ni mauti. RUM. 6:21 SUV.

Ndugu, naendelea kukuuliza kama maandiko yanavyosema hapo, faida gani umepata kwa kutokusoma Neno la Mungu, na faida gani umepata kwa kusoma Neno la Mungu kila siku. Au faida gani utapata utaporudia maisha yako ya awali ya kutokusoma Neno la Mungu

Jiulize faida gani umepata tangu uwe mzembe kwa kutoshiriki ibada za kanisani kwako, na faida gani umepata kwa kushiriki ibada za kanisani kwako.

Jiulize faida gani umepata tangu ukatae kumsamehe huyo aliyekukosea, na faida gani umepata tangu umemsamehe huyo aliyekukosea. Kipi umevuna matunda mazuri, na hayo matunda uliyovuna mwisho wake ni uzima wa milele au ni mauti?

Jiulize faida gani umepata tangu uachane na maisha ya dhambi, na faida gani umepata tangu uanze kufanya mambo mabaya yasiyompendeza Mungu. Inawezekana umeokoka ila unajiona haupo huru sana kama ulivyokuwa zamani, hebu jiulize uhuru unaoutaka mwisho wake utakupeleka uzima wa milele au utakupeleka kwenye mauti.

Rejea: Lakini sasa mkiisha kuwekwa huru, na kuwa mbali na dhambi, na kufanywa watumwa wa Mungu, mnayo faida yenu, ndiyo kutakaswa, na mwisho wake ni uzima wa milele. RUM. 6:22 SUV.

Rafiki unayo faida kubwa sana kuwa mtumwa wa Mungu, na unayo hasara kubwa sana kuwa mtumwa wa shetani, maana shetani hana uzima wa milele. Bali mwenye uzima wa milele ni Mungu pekee unayemkataa na kuendelea kuishi maisha yasiyompendeza yeye.

Endelea kutafakari yale unafanya, yapo mambo unafanya kwa bidii sana ila faida yake ni ya kimwili na ya muda mfupi tu. Na yapo mambo unayafanya sasa yanaonekana faida yake ni ndogo ila pamoja na udogo huo yatakufanya uingie uzima wa milele.

Nakusihi sana kama bado hujajiunga na kundi letu la wasap la kusoma Neno la Mungu kila siku kwa mtiririko mzuri usiochosha, nikukaribisha sana. Tuma ujumbe wako kwa wasap namba +255759808081 utapatiwa taratibu za kundi.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com