
Bidii ya mtu siku zote haijawahi kumwangusha mtu, matunda yake yanaweza kuchelewa kuonekana haraka ila mtu mwenye bidii lazima atavuna matunda ya bidii yake.
Watu wengi huwa tunashindwa kuelewa hili na tunapoona hatusogei hatua moja kwenda nyingine, huwa tunaanza kumtafuta mchawi. Unakuta mtu ameokoka vizuri kabisa, anaanza kufikiri atakuwa amelogwa ndio maana wengine wanapanda viwango vya juu zaidi yeye anabaki alivyo.
Muda mwingine huwa tunasingizia vitu visivyo na msingi kabisa, kumbe ni uvivu wa mtu unakuwa umemfunga aendelee kubaki hatua hiyo hiyo kila siku. Watakuja watu wapya watamwacha Kwenye hatua ile ile, bila kujua shida ni nini ataendelea kubakia analalamika tu.
Unaweza kumwona mtu wa kawaida kabisa, nikiwa na maana hana elimu kubwa sana kama ya kwako au sio kama ya mtu fulani ila ukawa unamwona anazidi kupanda viwango vya juu zaidi.
Wakati wengine wanapambana kuomba Mungu watoke hatua moja kwenda hatua nyingine, kumbe shida waliyonayo ni kukosa maarifa sahihi ya kuwatoa pale walipo. Kwa kuwa hawajui wataendelea kuomba zaidi na zaidi, na hata Mungu anapojaribu kusema nao kuhusu kusoma Neno la Mungu wanakuwa wagumu kuchukua hatua.
Mtu mwenye bidii sana kwa anachofanya, mtu huyo lazima atasimama mbele ya wakuu, watu watatamani kusikia amewezaje kufanikiwa kwa kile anafanya, watu watatamani kupata maarifa kutoka kwake.
Kwa maana nyingine bidii ya mtu inaweza kumletea heshima kubwa mbele za watu, heshima ambayo hawezi kuipata mtu mvivu, mtu anayefanya kazi ya Mungu kwa mikono milegevu, mtu anayefanya kazi zake za mikono kwa ulegevu, mtu asiyejali kwa lile anafanya.
Heshima haipo kwa hao watu, sio kana kwamba watu wanakuonea hapana, hiyo ni kanuni ya Mungu, watu wenye bidii watasimama au waketi pamoja na wakuu. Kuokoka tu haitoshi, kama upo duniani unapaswa kuwa mtu mwenye bidii sana.
Sio kwa sababu umeokoka, unaajiriwa ofisi ya mtu unakuwa unafanya kazi kizembe, utashangaa wenzako wanapanda ngazi za juu kwa sababu ya bidii zao za kazi, utashangaa wenzako wanachaguliwa kuhudhuria mikutano maalum na wewe unaachwa hapo.
Rejea: Je! Wamwona mtu mwenye bidii katika kazi zake? Huyo atasimama mbele ya wafalme; Hatasimama mbele ya watu wasio na cheo. MIT. 22:29 SUV.
Nami nakuuliza Je! Unamwona huyo mwanafunzi mwenzako mwenye bidii? Wakati wewe unadhurura mitaani yeye amejifungia ndani kusoma, wakati wewe unakesha kuangalia movies yeye anasoma, wakati wewe unapoteza muda kwa mambo yasiyofaa yeye anasoma.
Je! Unamwona huyo mfanyakazi mwenzako mwenye bidii hapo ofisini kwenu? Wakati wewe unapuuza majukumu madogo madogo unayopewa na kiongozi wako, wewe unayepuuza mwenzako anafanya kwa umakini na uaminifu mkubwa.
Je! Unamwona huyo mfanyabiashara mwenzako hapo jirani mwenye bidii? Wakati wewe unafungua ofisi yako saa tatu asubuhi, ukiwahi sana saa mbili asubuhi, mwenzako anafungua saa kumi na moja alfajiri, akichelewa sana anafungua saa kumi na mbili asubuhi.
Je! Unamwona huyo dada wa kazi kwa jirani yako au hapo ndani kwenu mwenye bidii ya kazi zake hapo nyumbani? Wakati wewe umelala hadi saa mbili asubuhi kwa sababu upo kwenu, dada wa kazi anaamka saa kumi na moja alfajiri anafanya kila kitu. Alafu anakuja kukuamsha ukanywe chai aliyoandaa.
Uwe na uhakika watu hao wote niliokutajia watakuwa na malipo yao hapa hapa duniani, usishangae kumwona yule dada wa kazi aliyekuwa anafanya kazi zake hapo nyumbani kwenu kwa bidii sana. Anapata mwanaume mzuri sana kwa tabia, alafu wewe unaendelea kusota bila kumpata huyo mwanaume mzuri.
Wewe ni shahidi kama umeona wanafunzi waliofanya vizuri kwenye mitahani ya kidato cha nne tumeona wakihojiwa na vyombo vya habari. Utasema ni kitu cha kawaida, kwako ni cha kawaida ila fahamu kwamba hiyo ni kanuni ya kiMungu mwenye bidii anapata heshima yake.
Watu wenye bidii wana heshima yao, haijalishi huyo mtu yukoje, akiwa na bidii kwa kile anafanya lazima apate heshima yake. Mtu ambaye akiondoka kwenye nafasi yake watu wanalia, wanalia kwa sababu wanajua mchango wake.
Ndugu msomaji wangu sijui hapo ulipo una nafasi gani ila nakusihi sana, jambo lolote utakalopata nafasi ya kulifanya, lifanye kwa bidii zako zote, kwa nguvu zako zote, kwa moyo wako wote, na kwa akili zako zote.
Rejea: Lo lote mkono wako utakalolipata kulifanya, ulifanye kwa nguvu zako; kwa kuwa hakuna kazi, wala shauri, wala maarifa, wala hekima, huko kuzimu uendako wewe. MHU. 9:10 SUV.
Hakuna nafasi nyingine tena nje na hapa duniani, huwezi kwenda kufanya kazi kwa bidii baada ya kufa, yote uyafanyalo, yote yapitayo kwenye mikono yako. Hakikisha unafanya kwa bidii zako zote, maliza nguvu zako zote kwa kile unafanya.
Usisome Biblia yako kwa ulegevu, isome Biblia yako kwa bidii, baada ya muda fulani utaona matunda yake. Bila kufanya hivyo huwezi kuona matunda ya usomaji wako, utakuwa mtu tu wa kawaida.
Bidii yako lazima ikuketishe/ikusimamishe mbele ya wafalme au wakuu, bila kujalisha mazingira uliyonayo sasa hivi, hakikisha unafanya kwa bidii kwa kile ulichoamua kufanya au ulichopewa kufanya.
Kama bado hujajiunga na kundi letu la wasap la kusoma Neno la Mungu kila siku, tuma ujumbe wako kwa wasap namba +255759808081 utaunganishwa baada ya kupewa kanuni zetu.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com