Kwa wengi wetu limeanza kuwa jambo la kawaida kupinga kila kitu kwa viongozi wao, kuna vitu ambavyo wanakuwa wanapiga na kusambaza maneno mabaya juu ya kiongozi wao.

Kejeli nyingi na kuzihaki kwingi limekuwa jambo la kawaida kwa watu hao, hakuna kitu kitaongelewa na kiongozi asipinge, hakuna jambo atakalofanya kiongozi asipinge. Kila kitu kwao wanakuwa kinyume na kiongozi.

Hawa watu wapo sana hasa kwenye makundi, viongozi ambao wamepewa dhamana ya kuongoza kundi hilo wanakuwa wanapita kwenye changamoto ngumu sana kutokana na kikundi cha watu wachache wanakuwa wanapanda mbegu mbaya kwa watu wengine wanaowaogoza.

Wapo viongozi wa ngazi za juu, nikiwa na maana kitaifa, awe kiongozi wa kiimani au awe kiongozi wa serikali, wote wanaitwa viongozi. Tunapaswa kuwatii na kuwaheshimu hao viongozi, maana mamlaka waliyonayo imetoka kwa Mungu.

Kuanza kushindana na Askofu wako, utakuwa unashindana na agizo la Mungu, nafasi aliyonayo kiongozi wako ameaminiwa ndio maana yupo kwenye nafasi hiyo ya uongozi. Kiti cha uongozi alichokalia kiongozi huyo ni mamlaka kutoka kwa Mungu.

Wengi huwa tunasema ya nini kuogopa kiongozi fulani, au ya nini kuwa na hofu na kiongozi fulani, au ya nini kumtetemekea kiongozi fulani. Tunaenda mbali zaidi na kusema tunapaswa kumwogopa Mungu pekee na sio mwanadamu, ni kweli hatupaswi kuwa na hofu kwa kiongozi?

Tusiwe tunaongea tu kwa sababu kila mtu anaongea, tunapaswa kuthibitisha hili kwa maandiko matakatifu tujue kweli ni vibaya kuwa na hofu kwa kiongozi? Je ni kweli hatupaswi kuwa na heshima kwa viongozi wetu?

Rejea: Wapeni wote haki zao; mtu wa kodi, kodi; mtu wa ushuru, ushuru; astahiliye hofu, hofu; astahiliye heshima, heshima. RUM. 13:7 SUV.

Sijui kama umeelewa vizuri hilo andiko linavyosema, kila mmoja anapaswa kuheshimiwa kwa nafasi yake ya uongozi aliyonayo. Unaweza ukawa una dharau nyingi kwa kiongozi wako, usifikiri upo salama sana.

Hili suala tunajifunza wote hapa, maana tumekuwa watu ambao tunaona wa kumweshimu ni Mungu pekee ila hawa viongozi tunaona hatuna haja ya kuwapa heshima yao.

Wakati mwingine tumeonyesha dharau zetu waziwazi juu yao, dharau ambazo zimekuwa zikiwaumiza wale wanaotuongoza. Hasa mtu akiwa na uwezo mkubwa kiuchumi kumpita kiongozi wake anakuwa na dharau kwake.

Fahamu kwamba ni agizo la Mungu kuwaheshimu na kuwatii wenye mamlaka, tena mamlaka iliyokuu, haijalishi unamwona huyo mtu ni mdogo sana kwako. Kama amepewa mamlaka iliyokuu huna budi kumtii kwa kile anakuambia.

Rejea: Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na ile iliyopo umeamriwa na Mungu. RUM. 13:1 SUV.

Kama mamlaka hizi za uongozi zinatoka kwa Mungu mwenyewe nina imani haitakuwa kinyume na Mungu, na ikiwa kinyume na Mungu, Mungu mwenyewe atamwondoa huyu mtu kwenye nafasi yake kama tunavyosoma habari za Sauli alivyomkosea Mungu akaondolewa kwenye nafasi yake akapewa Daudi.

Kama huzitii mamlaka au kama huna utii kwa viongozi wakuu, fahamu moja kwa moja huna utii kwa Mungu wako, maana mamlaka hizo zimetoka kwa Mungu mwenyewe. Lazima uwe na heshima kwa kiongozi, sio heshima tu lazima utii kile anakuelekeza.

Sasa kama kazi yako ni kwenda kinyume na yale mamlaka inakuelekeza ufanye, ujue unaenda kinyume na agizo la Mungu wako, na unapoenda kinyume na agizo la Mungu unajipatia hukumu.

Rejea: Hivyo amwasiye mwenye mamlaka hushindana na agizo la Mungu; nao washindanao watajipatia hukumu. RUM. 13:2 SUV.

Hili linaweza likawa jambo gumu kwako kulikubali ila fahamu kwamba maandiko matakatifu yapo wazi kwa hili, ni wewe kuamua kulipokea na kuliweka kwenye matendo au kuendelea na kile ulikuwa unakifanya.

Lakini fahamu kushindana na mamlaka ni kushindana na agizo la Mungu, na wanaoshindana na agizo la Mungu watajipatia hukumu. Sijui kama unaelewa vizuri hapo, nasema hivi; wale waopinga wenye mamlaka, watajipatia hukumu.

Tii mamlaka kuepukana na hukumu ya Mungu, ukishupaza shingo na kuendelea kushindana na wenye mamlaka, utakachokipata utakijua mwenyewe lakini nimekueleza mapema. Kama ni kuacha unapaswa kuacha, na kama kutokufanya kabisa hupaswi kufanya.

Kama bado hujajiunga na kundi la wasap la kusoma Neno la Mungu kila siku, nakusihi sana uungane nalo maana litakusaidia kufika malengo yako ya kusoma Biblia. Tuma ujumbe wako kwa wasap namba +255759808081.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com
+255759808081