
Bila shaka umeshuhudia mara nyingi watu wakibishana juu ya jambo fulani ni sahihi kufanywa na mkristo, na jambo fulani si sahihi kufanywa na mkristo. Miongoni mwa mabishano hayo, yupo mtu mmoja wapo anakuwa yupo sahihi na yupo mwingine anakuwa hayupo sahihi.
Mtu aliye dhaifu wa imani au kwa maana nyingine tunaweza kusema yule aliye mchanga wa kiroho, mambo mengi anakuwa haelewi sana. Changamoto ambayo ipo kwa wachanga wengi wa kiroho, huwa hawakubali kuwa hawajui, wao huwa wanajiona wanaelewa.
Imani yao dhaifu huwa hawaioni sana, wanachoona wao wapo sahihi kwa kile wanaamini ni sawa kwao, kwahiyo unaweza kuanzisha mjadala ambao yeye anakuwa hajui chochote kile lakini anakawa anajibu kana kwamba anaelewa.
Kwa kuwa na wewe hujajua kumsoma mtu, utaendelea kung’ang’ana naye kwa kubishana kwa jambo ambalo wewe unaona si sahihi yeye kulifanya, na yeye anakuwa anaona ni sahihi kulifanya.
Wewe unaweza ukawa unaelewa hata ukiwa mkristo kufanya jambo fulani sio vibaya, na yeye akawa anaona kufanya hilo unaloliona wewe ni sahihi kulifanya. Yeye akawa anaona si sahihi kulifanya hilo unalosema haina shida mkristo au mtu aliyeokoka kulifanya.
Unapokutana na mtu aliye dhaifu wa imani usianze kumshambulia sana kwa udhaifu wake, jua namna ya kuendana naye. Ukiona hataki kukuelewa na amesimamia msimamo wake, usikimbilie kusema ni mpumbavu. Maana Mpumbavu yeye hujiona anajua kila kitu, na kumwelimisha Mpumbavu ni kupoteza muda maana hatakaa akuelewe.
Sasa wengine sio wapumbavu bali ni dhaifu wa imani, unapaswa kwenda nao kwa akili, bora kusitisha mazungumzo yenu kuliko kuendelea kushambuliana kwa maneno mengi yasiyofaa.
Rejea: Yeye aliye dhaifu wa imani, mkaribisheni, walakini msimhukumu mawazo yake. RUM. 14:1 SUV.
Unaona hilo andiko linavyosema, linalenga lile lile nililokuwa nakueleza hapa, usimhukumu mawazo yake aliye dhaifu wa imani, wala usimwonyeshe kejeli, nenda naye kwa utaratibu ukimwonyesha maandiko matakatifu yanavyosema juu ya hicho kitu anachoamini si sahihi au ni sahihi.
Kadri atakavyozidi kujua maandiko matakatifu ataanza kutoka kwenye imani yake dhaifu na kuwa mtu anayeijua kweli, na akishatoka kwenye huo uchanga atakuwa mtu mzuri sana anayefaa wengine ambao wana udhaifu wa imani.
Kumshambulia kwa maneno makali mwenye imani dhaifu huwezi kumsaidia kitu, zaidi unaweza kumfanya ashindwe kuelewa kipi afuate na kipi asifuate. Maana hata hicho anachoshikilia kuwa ni sahihi au sio sahihi, mwanzo alipata mafundisho yanayomwambia ni sahihi au sio sahihi.
Ukija kumwambia fanya hivi usifanye hivi lazima mtapishana tu, maana msingi wake wa kwanza alijengwa kuamini kuwa ni sahihi au sio sahihi hicho unachomwambia wewe.
Vizuri kuelewa hili, pale utakaposimama kueleza habari za Yesu Kristo kwa usahihi, hakikisha unajikita zaidi kwenye maandiko matakatifu. Onyesha hatua kwa hatua hicho anachofanya huyo mtu unayemweleza, unamweleza kutokana na imeandikwa mahali fulani (mwonyeshe kabisa andiko linavyosema)
Pamoja na kumwonyesha anaweza asikuelewe kabisa wakati huo ila baadaye akakuelewa, utaona amekuelewa kama hutotanguliza maneno ya kumkashifu na kumwonyesha dharau.
Hii ndio faida ya kulifahamu Neno la Mungu linavyosema, linatusaidia kufahamu mambo mengi sana wasiyoweza kuyafahamu wengine wasiopenda kusoma Neno la Mungu. Hakikisha unasoma Biblia yako kila siku.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com