Kuna mahali ambapo bado injili inahitajika sana watu wapelekewe habari njema za Yesu Kristo, mahali ambapo watu huwa hawafiki kabisa huko kuhubiri injili ya kweli.

Mahali huko ambapo panahitajika kupelekwa injili sahihi ya Yesu Kristo, huko watu wanakuwa hawafiki, wanafika maeneo yale yale ambayo tayari wengine walishafika mara nyingi.

Kwa hiyo wanaosikia habari za Yesu Kristo ni wale wale ambao tayari walishakubali kuokoka, walishamkubali Yesu Kristo kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yao.

Watu ambao hawahitajiki tena kutumia nguvu nyingi za kuambiwa wamwamini Yesu Kristo, bali wanahitaji tu mwalimu mzuri wa Neno la Mungu wa kuwasaidia kuukulia wokovu, watu ambao wanahitaji mchungaji mzuri wa kuwalea waweze kuendelea kumjua zaidi Yesu Kristo.

Watu hawa waliopata mwelekeo mzuri wa kumpokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wao, wakati mwingine wanashindwa waende wapi na wabaki wapi. Maana pale walipotakiwa kulelewa kiroho, anakuja mtumishi mwingine anawaambia tokeni huko njooni huku ni pazuri.

Wakati wapo watu ambao wanahitaji kupelekewa injili waweze kuokoka, sasa wapo watumishi hawataki kuhubiri injili kwa wale ambao hawajaokoka kabisa. Wao wanahubiri injili kwa wale ambao tayari wameshaokoka na mahali wanaposali wanasali mahali sahihi, nikimaanisha mahali ambapo wanasali wanalelewa vizuri kiroho.

Tukiwa kama wahubiri wa injili, hatupaswi kuwa watu wa kujenga msingi juu ya msingi mwingine, nikiwa na maana kwamba watu tayari wameshaokoka wanachohitaji wao ni kufundishwa Neno la Mungu na kusisitizwa kusoma Biblia kila siku.

Mtu kwenda kanisa analolitaka yeye sio shida na sio somo langu la leo, mimi ninachokisema hapa ni kukazana kuhubiri mahali ambapo kuna mhubiri alihubiri jana, alafu kuna mahali ambapo hapajaguswa kabisa. Na kama pameguswa ni siku nyingi sana watu hawajaenda huko kutangaza habari njema za Yesu Kristo.

Hili tunajifunza kwa mtumishi wa Mungu Paulo, Paulo alikataa kuhubiri injili mahali ambapo wengine walishahubiri, alitaka kuhubiri mahali ambapo palikuwa bado hapajahubiriwa kabisa habari njema za Yesu Kristo aliye hai.

Rejea: Kadhalika nikijitahidi kuihubiri Injili, nisihubiri hapo ambapo jina la Kristo limekwisha kutajwa, nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine. RUM. 15:20 SUV.

Siku za leo inaweza ikawa ngumu kupata mahali ambapo hapajahubiriwa kabisa habari njema za Yesu Kristo ila kuna mahali inaweza ikapita miaka mingi sana hakujahubiriwa habari za Yesu Kristo.

Japo anaweza kuhubiri mtu mwingine watu baadhi wasiokoke, alafu akaja mtu mwingine akahuburi habari za Yesu Kristo wale ambao hawakuokoka wakaokoka. Lakini pamoja na hayo yote bado kuna mahali watumishi hatufiki kabisa kupeleka injili sahihi ya Yesu Kristo, kwa hiyo ni vizuri kufanya kabla hatujaenda.

Sawa na makanisani leo wale tunaoinuka kihuduma, tunapenda tupewe nafasi za kuhubiri kwenye vipindi vya kanisani na tusipopewa nafasi tunakasirika sana. Ila mashuleni huko kwenye vipindi vya dini watoto hawana walimu wa kuwafundisha, maana yake kuna nafasi za kutosha ya mtu mwenye wito kutoa kile ambacho Mungu amempa ndani yake badala yake tumekaa tunatafuta nafasi kanisani.

Lipo kanisa lingine huko shuleni/chuoni linahitaji maneno ya Mungu, kundi ambalo kulipata kwenye vipindi vya kanisani ni vigumu sana. Lakini wakiwa shuleni ni rahisi sana kuwapata maana wanabanwa na kanuni za shule kuingia kwenye vipindi vya dini.

Tunapenda kujenga msingi juu ya msingi mwingine ila kujenga msingi mahali ambapo hapajajengwa hatutaki, hiyo sio nzuri kabisa, yapo maeneo mengi sana bado hajafikiwa vizuri na injili ya Yesu Kristo. Tunapaswa kuyafikia hayo maeneo, na tuende kwa namna ambayo sio ya mazoea.

Na kama Mungu amekupa huduma ya kuchunga watu, anza kutafuta wale ambao ni wapya kabisa, sio kile kile anafanya mwenzako na ukamwona mtu ametulia mahali hapo wewe unataka umtoe aje kwako. Kwanini usitafute wengine ambao wanahitaji kupokea kile ambacho Mungu amekupa kuliko kuhangaika na ambao tayari wapo mahali sahihi kwa kile kile unachotaka uje uwaambie/uwafundishe.

Umeokoka na kusoma Neno la Mungu ni changamoto kwako na hujui ufanyaje, karibu sana kwenye kundi letu la wasap la kusoma Neno la Mungu kila siku. Hii itakuwa nafasi yako nzuri ya kuambatana na watu wanaopenda kusoma Neno kwa vitendo huku ukisimamiwa kuhakikisha na wewe unakuwa msomaji wa Biblia. Tuma ujumbe wako kwa wasap namba +255759808081 utapata maelekezo mengine ya kujiunga.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com