Kuna watu hawaonyeki wala hawashauriki wala hawaambiliki, ni watu ambao wanavuruga amani ya vikundi vingi vilivyokusanyika kwa nia njema. Ni watu ambao wamekuwa chachu ya kusababisha mafarakano ndani ya kanisa au familia.

Ni watu ambao ndani ya vikundi vya kwaya wao ndio wamekuwa chachu ya ugomvi, wao ndio wamekuwa wakipinga kila kitu, hata kwa vile vitu vizuri vinavyopangwa na viongozi kwa maslahi ya kwaya. Wao wamekuwa wakianzisha mijadala ya kubomoa, ama wamekuwa watu wa kuhamasisha watu wengine wasishiriki.

Watu ambao wamekuwa wanazusha uongo na baadaye ule uongo kadri unavyozidi kusikiwa na watu wengine wanaona ni kweli, kumbe hakuna ukweli wa aina yeyote bali ni kutengeneza vitu vya kuchafua tu wengine.

Mambo wanayozusha hawa watu, kutokana na nafasi zao, baadhi ya watu hawaamini na kuona wanachoambiwa ni kweli kumbe ni uongo. Kuja kuwaambia watu mlichokuwa mnasikia au mnaambiwa kilikuwa cha uongo inakuwa ni ngumu kueleweka.

Watu hawa wanaopenda mafarakano ndani ya kundi, huwa hawapendi hali ikiwa shwari, wao hupenda watu wakiwa wanagombana. Watu wakiwa wanavutana huku na kule wao ndio wanajisikia vizuri.

Wanaweza kuanzisha mada yeyote ambayo wanajua mwisho au katikati ya hiyo mada itazalisha mafarakano na kutokuelewana ninyi kwa ninyi. Lakini wakati inaanza hiyo mada unaweza usielewe haraka kusudi lake ila ukiwa umetulia utajua lengo ya hiyo mada.

Hasa makundi ya wasap mengi yamevunjika au yamesambaratika kwa sababu ya watu hawa wapenda mafarakano au wazushi kuwemo, hasa pale viongozi wa makundi hayo waliposhindwa kuzuia au kuwaondoa wale ambao walikuwa wanaanzisha mafarakano hayo.

Maandiko matakatifu yanatufundisha kwamba, dawa ya mtu mzushi au kwa maana nyingine tunaweza kusema mtu anayeanzisha mafarakano. Mtu wa namna hiyo unapaswa kumwonya mara ya kwanza na mara ya pili, ukiona hasikii wala hataki kuacha tabia yake, hatua inayofuata mkatae au achana naye.

Rejea: Mtu aliye mzushi, baada ya kumwonya mara ya kwanza na mara ya pili, mkatae; ukijua ya kuwa mtu kama huyo amepotoka, tena atenda dhambi, maana amejihukumu hatia yeye mwenyewe. TIT. 3:10‭-‬11 SUV.

Usipomkataa au usipomwondoa kwenye kundi lenu, uwe na uhakika hilo kundi litasambaratika muda sio mrefu, maana wapo watu ndani ya kundi hawapendi vurugu zisizo na msingi wowote. Na ni mbaya sana kuamka kila siku mkiwa watu wa mafarakano, hata ikiwa nyumbani kwako inakuwa sio nzuri.

Na kama upo kwenye kundi la watu wanaopenda mafarakano, ujue unatenda dhambi, usijione upo salama, fahamu unatenda dhambi mbaya mbele za Mungu. Kwahiyo unaweza kuchagua kuendelea na hiyo tabia yako ya mafarakano au kuamua kuachana nayo.

Mtu mzushi au mtu wa mafarakano sio mtu mwenye Roho Mtakatifu ndani yake, wala si mtu aliyeokoka sawasawa, huwezi kuwa na Roho Mtakatifu ndani yako alafu ukawa mtu unayependa machafuko kila wakati.

Yupo mtu mwingine utamkuta anasema sijaleta fujo siku nyingi sana hadi najisikia vibaya, hicho kitendo cha kutokuleta fujo siku nyingi kwake ni kama hakijampendeza anataka kuanzisha mafarakano ili ajisikie vizuri. Na kweli lazima atimize dhamira yake.

Kama ni kiongozi na una mtu mzushi au mtu wa kuanzisha mafarakano nakusihi uchukue hatua kama maandiko matakatifu yanavyotuelekeza hapo juu. Vinginevyo utalisambaratisha kundi unaloliongoza kwa ajili ya mtu mmoja au watu wachache.

Mwisho, kama bado hujajiunga na kundi la wasap la kusoma Neno la Mungu kila siku, nafasi yako ipo, tuma ujumbe wako kwenda wasap namba +255759808081 utaunganishwa baada ya kupewa kanuni za kundi.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com