Hekima ya kiMungu sio kitu ambacho anaweza kuwa nacho mtu yeyote aliyeumbwa na Mungu, nikiwa na maana sio kila mwanadamu anaweza akawa na hekima ya kiMungu ndani yake pasipo utaratibu.

Mtu anaweza kuonekana ana busara nyingi, mwenye kujaa hekima za dunia hii, alafu mtu huyo akakosa hekima ya kiMungu. Hekima ya dunia hii inaweza kufundishwa darasani ila sio hekima ya kiMungu, ni kitu tofauti kabisa ambacho mtu anapewa kama zawadi akiwa ameokoka sawasawa.

Bidii ya mtu kwa mambo ya Mungu, kama vile kusoma Neno la Mungu kwa bidii na kuwa na maisha ya utakatifu, na huku akiwa mtu wa maombi, mtu huyo anaweza kupewa zawadi hii ya hekima ya kiMungu.

Mtu mwenye hekima ya kidunia na mtu mwenye hekima yenyewe ya kiMungu, wakikaa meza moja, lazima paonekana pana utofauti, mtu wa Mungu hawezi kulingana kiwango chake na mtu tu asiye na Yesu moyoni alafu ana hekima ya duniani.

Muhimu sana kuelewa hili, unaweza kukaa na mtu ambaye anajulikana ana hekima nyingi kumbe hekima zake zinazojulikana ni hekima za duniani, na sio hekima za kiMungu. Mtu huyo uwe na uhakika mkianza kusuluhisha jambo lolote lile linalohitaji hekima ya kiMungu mtafika mahali mtapishana tu, maana yeye anatazama mambo kimwili wewe utakuwa unatazama mambo kwa jicho la rohoni.

Kama msingi wako wa imani umeujenga kwenye hekima ya wanadamu, nakushauri ubomoe haraka na ujenge katika nguvu za Mungu. Hekima za wanadamu si kitu mbele za Mungu, maana wapo watu wana hekima za kibinadamu na hawamjui Kristo.

Usijidanganye kuwa una hekima nyingi na imani yako iko imara, kumbe hekima yenyewe na imani yenyewe umeijenga kwenye msingi usiotokana na nguvu za Mungu.

Rejea: Ili imani yenu isiwe katika hekima ya wanadamu, bali katika nguvu za Mungu. 1 KOR. 2:5 SUV.

Ndugu sijui kama unanielewa vizuri, hekima ya kiMungu ni tofauti kabisa, hakuna mtu yeyote anaweza kuipata hivi hivi, haijalishi ni mtawala wa nchi. Kama hana mahusiano mazuri na Mungu, ama kama hajampokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wake, hawezi kuipewa hii hekima ya kiMungu.

Kwahiyo kama unajidanganya una hekima nyingi kutokana na kusoma vitabu mbalimbali visivyohusiana na Neno la Mungu, alafu maisha yako ya kiroho hayapo vizuri. Uwe na uhakika hekima ya kiMungu haimo ndani yako, na wala huijui kabisa hiyo hekima ya kiMungu.

Usifikiri ni maneno yangu, maandiko matakatifu ndivyo yanavyosema yenyewe, sasa kama maandiko yanasema hivyo wewe ni nani uendelee kukataa? Hebu tusome haya maandiko yanavyosema;

Rejea: Bali twanena hekima ya Mungu katika siri, ile hekima iliyofichwa, ambayo Mungu aliiazimu tangu milele, kwa utukufu wetu; ambayo wenye kuitawala dunia hii hawaijui hata mmoja; maana kama wangaliijua, wasingalimsulibisha Bwana wa utukufu. 1 KOR. 2:7‭-‬8 SUV.

Umeona hiyo hekima ya kiMungu ilivyo hapo, sio hekima ya hivi hivi ni hekima iliyo katika siri, tena imefichwa, tofauti kabisa na hekima za wanadamu ambazo unaweza kufundishwa tu ukawa nayo.

Ndiyo hekima aliyoomba mfalme Suleiman akapewa na Mungu, hekima ambayo huwezi kuipata tu hivi hivi, Usijidanganye una hekima nyingi kutokana na mafunzo uliyopata. Elewa hiyo hekima sio ya kiMungu, hekima ya kiMungu inatokana na Neno la Mungu, haipo kwa kila mtu.

Na hekima ya wanadamu na hekima ya kiMungu haziwezi zikapimwa katika usawa, usije ukamwona mtu mwenye hekima ya wanadamu, ana hekima nyingi kuliko mwenye hekima ya kiMungu. Ukiona hivyo ujue Yesu Kristo hayumo ndani yako, uwe na uhakika Roho Mtakatifu hayumo ndani yako.

Epuka sana kujenga msingi wa imani yako kwenye mafundisho yasiyotakana na Neno la Mungu, ukafika mahali ukaanza kumtazama Mungu kwa jinsi ya hekima za kibinadamu. Nakwambia utakuwa umepotea njia, na hekima yako haitakuwa na maana yeyote mbele za Mungu.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com