Yapo mambo huwezi kuyafahamu kwa kuangalia kwa macho ya nyama, haijalishi una akili nyingi sana, wala haijalishi umesoma sana saikolojia za watu. Hutokaa uyafahamu mambo ya ndani ya moyo wa mtu.

Ndio maana vijana wengi wanafeli kwenye eneo la kupata mke/mume sahihi wa kuishi naye, kwa sababu wengi wao hutazama kwa nje. Anaweza kumwona kaka/dada anampenda sana Yesu kutokana na bidii yake kwa mambo ya Mungu.

Lakini kaka/dada yule anaigiza tu ila matendo yake ni machafu sana anapokuwa mahali pengine nje na kanisani, kwa sababu sehemu kuu ya kukutana na kaka/dada yule ni kanisani au kambini au mahali popote pale penye kusanyiko inakuwa sio rahisi kumjua.

Wengi wamekuwa na maswali mengi sana kuhusu eneo hili la mahusiano, wanajiuliza inakuwaje mtu alikuwa ameokoka alafu ghafla wameingia naye kwenye ndoa anaanza kuonyesha tabia sio nzuri.

Jibu lipo wazi, huyo hakuwa ameokoka, bali alikuwa anaigiza ameokoka wakati hajaokoka, na mmoja wapo angekuwa yupo vizuri na Mungu na akawa amejawa na Roho Mtakatifu. Angeweza kumtambua kirahisi tu, na huenda alikuwa na vyote hivyo ila hakumsikiliza Roho Mtakatifu pale aliposema naye kuhusu huyo aliyekuwa anataka kuanzisha naye mahusiano ya uchumba hadi ndoa.

Ndugu yangu, mambo ya rohoni huwezi kuyafahamu kwa kumtazama mtu kwa nje, mambo yote ya ndani yanafunuliwa na Roho Mtakatifu. Na watu waliojazwa Roho Mtakatifu ndio wanaoweza kufunuliwa hayo, ndio wanaoweza kuyajua mafumbo ya Mungu.

Rejea: Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu. Maana ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu. 1 KOR. 2:10‭-‬11 SUV.

Hapo juu nilikupa mfano wa mahusiano, na watu wengi wamekuwa wakilalamika moyo wa mtu ni kichaka, lakini hicho kichaka kinawekwa wazi na Roho wa Mungu ambaye anakuwa ndani ya mtu.

Wala huna haja kuuliza sana tabia za mchumba wako, kama Roho Mtakatifu yumo ndani yako, na Neno la Mungu lipo la kutosha, nakwambia utayafahamu hata yale ambayo hukutegemea kuyafahamu. Maana Roho Mtakatifu atakufunulia na kuyaweka wazi kwako.

Wala huna haja ya kuwa na wasiwasi kuwa mchumba wako yupo mbali labda atakuwa na mtu mwingine, ukiwa na Roho Mtakatifu ndani yako, uwe na uhakika huyo mchumba wako hakuna kitu ataweza kukuficha. Lazima tabia yake chafu itafunuliwa wazi kwako, na kama umekomaa vizuri kiroho na Mungu akaona unaweza kustahimili utaona upuuzi wake kwa macho yako.

Ni kama naongea vitu ambavyo havipo kabisa au haviwezekani kabisa kuwepo kwenye maisha ya mkristo, uzuri wake nakueleza mambo ambayo yapo kimaandiko na mambo ambayo nimeyaona kwenye maisha yangu.

Ndio maana ni vizuri kuamua kuokoka sawasawa au kujulikana ni mtenda dhambi, kuliko kuwa vuguvugu. Maana unakuwa hueleweki umeokoka au ni mpagani, na kama umeamua kuokoka ni vizuri kuhakikisha unajazwa na Roho Mtakatifu.

Mwisho, kusoma Neno la Mungu ukiwa kama mkristo ni jambo la msingi sana kwako, sijui nikueleze kwa maneno gani ili ujue hili jambo lina umhimu kwako. Ila fahamu ni muhimu, na kama bado hujawa na ratiba ya kusoma Neno la Mungu kila siku nakualika tuwe pamoja kwenye usomaji wa Neno. Tuma ujumbe wako wasap namba +255759808081 utaunganishwa kwenye kundi letu la wasap la kusoma Neno.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com